Home Mchanganyiko MAJALIWA:MAGUFULI AMEACHA ALAMA NCHI NZIMA

MAJALIWA:MAGUFULI AMEACHA ALAMA NCHI NZIMA

0

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza Machi 24, 2021.

Mwili wa hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ukiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Machi 24, 2021.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Mwanza  wakati wa tukio la kuaga mwili wa hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwenye uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza Machi 24, 2021. . 

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulah, akitoa heshima  za mwisho kwa mwili ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwenye uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza Machi 24, 2021. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana,  Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akitoa heshima  za mwisho kwa mwili ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwenye uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza Machi 24, 2021. . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

………………………………………………………………………………..

NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
 WAZIRI Mkuu , Kassim Majaliwa jana amewaongoza maelfu ya waombolezaji na wananchi wa Mkoa na Jiji la Mwanza na mikoa jirani kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Rais John Magufuli akisema ameacha alama kubwa kwa Watanzania.
Akizungumza na maelfu ya waombolezaji kabla ya shughuli ya kuuga mwili kuanza, Majaliwa alisema Rais Magufuli alikuwa kiongozi mahiri aliyeliongoza taifa hili kwa weledi mkubwa na kwamba vilio vya uchungu vya wananchi vinaakisi mazuri aliyoyafanya.

“Hatuna maneno marefu, ni tukio la muda mrefu tangu Machi 20,Rais Samia Suluhu Hassan aliwaongoza wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutoa heshima za mwisho,hii leo ni mwendelezo wa kuamuaga kiongozi wetu,”alisema Majaliwa.

Alisema Mkoa na Jiji la Mwanza ni eneo la kihistoria kwani Rais Magufuli, aliwahi kuishi na kufanya kazi wakati wa uhai wake na amejenga makazi yake.

Waziri Mkuu huyo alisema Hayati Rais Magufuli ameacha alama kubwa mkoani Mwanza na mikoa ya Kanda Ziwa kutokana na kazi alizofanya kwa kutekeleza miradi ya maendeleo lakini pia ameacha alama kwa taifa zima hadi vijiji.

“Watanzania wanalia kwa uchungu kutokana na kazi aliyoifanya, Rais Samia Suluhu Hassan,anawasalimu na anatoa rai katika kipindi hiki kigumu na kututaka tuwe watulivu,tufanye kazi, tushirikiane na kupendana hadi siku atajapopumzishwa kwenye nyumba yake ya milele,”alisema Majaliwa.

Kwa mujibu wa Majaliwa,Rais Samia ana matumaini si siku 26 tu hadi maombolezo, Watanzania watakuwa wamoja na watulivu hivyo wamwombee kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake pema peponi ambapo wananchi wa Busisis Sengerema ambako ni ukweni kwa marehemu watapata fursa ya kuaga kwa dakika 10.

Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuzishukuru kamati ya kitaifa ya mazishi ikiongozwa na yeye mwenyewe, pia kamati ya mazishi za maandalizi za mikoa ya Mwanza, Dar Es Salaam, Dodoma na Zanzibar.

Pia alipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuimarisha ulinzi kuhakikisha zoezi la kumuaga vizuri kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya tano.

Aidha alivishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti tukio hilo kwa kipindi chote tangu kutangazwa kwa kifo cha Rais Magufuli kuwa vimefanya kazi nzuri na serikali inathamini na kutambua mchango wa vyombo hivyo. kipindi chote cha maombolezo

Mwili huo ulizungushwa mara tano kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ili kutoa fursa kwa waombolezaji kutoa heshima za mwisho kisha uliondolewa kupitia Furahisha ukipita barabara ya Makongoro, Gana, Kona ya Bwiru, Nyamanoro, Pasiansi, Kiloleli, Montesori, Maduka Tisa hadi Buzuruga wilayani Ilemela.

Msafara huo baada ya Buzuruga uliingia Barabara ya Nyerere ukitokea kupitia Mabatini, Mlango Mmoja, Natta, Mzunguko wa Mnara wa Mwl Nyerere hadi kwenye makutano ya barabara za Nyerere,Makongoro na Kenyatta

Baadaye uliingia Barabara ya Kenyatta eneo la kituo cha mafuta cha Puma, Picha ya Samaki,Pepsi, Voil, Mkuyuni, Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyashishi,Usagara Misungwi hadi kivuko cha Kigongo na kupandishwa kwenye Pantini hadi Busisi kuelekea Sengerema.