Home Mchanganyiko SPIKA JOB NDUGAI: TUMEFIWA NA MWENZETU, TUMEELEMEWA, TUMECHANGANYIKIWA WATANZANIA TUNALIA

SPIKA JOB NDUGAI: TUMEFIWA NA MWENZETU, TUMEELEMEWA, TUMECHANGANYIKIWA WATANZANIA TUNALIA

0

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Job Yustus Ndugai akizungumza kwa hisia bungeni leo wakati wabunge walipotoa heshima zao za mwisho kwa hayati Dk. John Pombe Magufuli jijini Dodoma leo.

Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza kwa uchungu katika tukio hilo la kuaga ambapo amesemakila anapoona jeneza anaona kama anapigiwa simu na kupewa maagizo.

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli ukiagwa na wabunge bungeni jijini Dodoma.

…………………………………..

*Waziri Mkuu Kassim Majaliwa: kila nionapo Jeneza naona kama napigiwa simu na kupewa maagizo

Mwili wa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli umeagwa rasmi leo Bungeni ambapo viongozi mbalimbali wa bunge wametoa salamu zao wakiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Job Yustus Ndugai ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kongwa mkoani Dodoma.

Akitoa salamu zake Job Ndugai amemzungumzia Hayati Dk. John Pombe Magufuli akisema Mhe. Rais wetu katika historia yake amekuwa mwenzetu hapa bungeni kwa miaka 26, amekuwa sehemu ya jumuiya hii tangu mwaka 1995 kama Mhe. Mbunge, Naibu Waziri, Waziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Leo ni siku ya majonzi makubwa hapa bungeni kwa kuwa tumefiwa na mwenzetu, tumelemewa, tumechanganyikiwa, watanzania tunalia, sisi wabunge tunasema asante Mungu kwa ajili ya Rais John Pombe Magufuli aliyeishi siku zote kwa kumtanguliza Mungu mbele,”. Amesema Job Ndugai

Ndugai amemshukuru Mungu kwa kunipa fursa ya kufanya kazi na Hayati Rais Magufuli kwa miaka 20  bungeni kama rafiki yake, ndugu yake, na kama kiongozi wake, safari imetimia na mwendo ameumaliza, rafiki yake John leo amelala mbele yetu

Amesema Hayati Rais Magufuli ulikuwa mtu mwema, alipanda mbegu, alikuwa mpanzi kama yule mpanzi wa kwenye Biblia naamini mbegu aliyopanda imedondoka kwenye udongo mzuri, amepanda barabara za lami kila sehemu ya nchi yetu, madaraja ambayo hatukuamini kama tungeyaweza, amejenga Masoko, amejenga Meli, viwanja vya ndege, Reli ya kisasa SGR, Bwawa la umeme la Nyerere Rufiji, Shule, Viwanda, Vyuo, Vituo vya afya, Hospitali, AMEJENGA… AMEJENGA…. AMEJENGA.

“Asante Mungu kwa kutupatia Mhe. Rais Samia Suluhu, tunaomba umpe siha njema, awe hodari, mwenye subira, awe mstahimilivu, pia usimpungukie hekima, na sisi wabunge tunaahidi kusimama na Mama Samia,”. Ndugai.

Mhe. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akimzungumzia Hayati Rais John Pombe Magufuli amesema alikuwa¬† mtu mcha Mungu, tumeuona wema wake, lakini kama kitabu cha Mungu ‘Biblia’ kisemavyo kuwa mwanadamu siku zake za kuishi si nyingi basi kazi ya Mungu haina makosa

Amesema hakuna ambaye hakuona yale mazuri na mengi aliyoyafanya Hayati John Pombe Magufuli, kila mtu ni shahidi

“Tuliwachagua viongozi wetu wapendwa Rais Magufuli na Mama Samia, sasa tumeachiwa Mhe. Rais Samia Suluhu tunaamini kuwa atatufikisha Kanaani, hivyo tuna imani naye,”. Amesema Dk Tulia

Amewapa pole watanzania, mke wa Hayati Rais Magufuli, Waziri Mkuu na viongozi wengine wote kwa msiba huu mkubwa kwa taifa la Tanzania.

Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye amesema “Leo ni siku ngumu sana kwangu, nawaza vile alivyokuwa akinipigia simu, akinipa maagizo, kila mtu anatambua namna ambavyo tumefanya naye kazi, ameweka alama kwenye majimbo yetu, vijiji, kata hata Halmashauri na mikoa, kila mmoja wetu ana namna ya kumueleza Rais wetu, tukisema kila mtu amuongelee kwa mazuri yake hatutamaliza,” amesema Mh.Majaliwa

Ameongeza kuwa Dunia nzima imegubikwa na huzuni, Afrika Mashariki, nchi za SADC, kwa sababu kiongozi wetu alikuwa miongoni mwa viongozi wa bara la Afrika, huzuni hii sio sisi tu ndo maana leo tutashuhudia viongozi wa nchi 17 pale uwanjani, hii ni dalili kwamba kiongozi wetu anakumbukwa kwa mema aliyoyatenda, atakumbukwa milele

Waziri Mkuu amesema tuzidi kumuombea mama mzazi wa Hayati Rais Magufuli ambaye amelala kitandani kwa miaka miwili sasa, Mungu amtie nguvu, poleni nyote, poleni Watanzania

Naye Mhe. Zuberi Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar amesema Mh. marehemu Rais John Pombe Magufuli alikuwa mpendwa wa watu, amesimamia na kufanya mengi katika uhai wake hasa mabadiliko makubwa katika Taifa letu ambalo kila mwenye macho haambiwi tazama

Amesema Rais Magufuli alikuwa mwalimu na mtatuzi wa masuala mbalimbali ya nchi, amekuwa akitatua matatizo ya watanzania kila mahali papo kwa papo hata aliposimamishwa na wananchi njiani akiwa katika ziara zake.

Huu ni ushahidi kuwa Rais Magufuli alikuwa ni chaguo la Mungu aliyeamua tuwe naye sisi watanzania, hatuna budi kuyafuata yale aliyoyaanzisha na kubuni mengine mapya na kuifikisha nchi mbali sana kwa kufuata nyayo zake ambazo hakuwaza kujitajirisha yeye binafsi bali alifanya kwa ajili ya wengine huku akisisitiza kuwa. ‘TANZANIA NI NCHI TAJIRI’.