Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera akiangalia uji tayari kwa kuanza kugawia kinamama waliohudhuria katika zoezi la kuandaa chakula cha mtoto
Kinamama wakisubiri cjakula kwa ajili ya watoto wao
Bwana Hassan Kipenyo mmoja wa wazazi wa kiume aliyejitokeza kujifunza namna ya kuandaa chakula cha mtoto akigeuza viazi vilivyochanganywa na nyama na mchicha
……………………………………………………………………………………..
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Kwa mara nyingine tena mkoa wa Katavi umeandaa zoezi la wazi la jinsi ya kupika chakula lishe kwa kinamama wajawazito, wazazi na walezi wenye watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kwa lengo la kuondoa udumavu ambapo mkoa wa Katavi una asilimia 33 ya watoto waliodumaa
Akizungumzia zoezi hilo Afisa Lishe mkoa wa Katavi Bi. Asnath Mrema amesema zoezi hilo linasaidia elimu ya lishe bora kwa watoto kufika kwa watu wengi kwa wakati mmoja hali itakayosaidia kueneza habari za lishe na hivyo kuonekana na changamoto ya watoto wenye lishe duni mkoani Katavi
Bi. Asnath amesema zoezi hilo pia liliendeshwa katika wilaya ya Mlele miezi michache iliyopita ambapo sasa wameamua kufanya katika manispaa ya Mpanda lengo likiwa ni kufikia halamashuri zote za mkoa huu
‘Tunawafundisha namna ya kuandaa uji wa mtoto, na vyakula vingine vinavyopatikana katika maeneo yetu kama vile viazi n.k’ alisema
Bi Sara Msafiri ni mmoja wa wakinamama waliojitokeza katika uwanja wa shule ya msingi Kashato, lilipofanyika zoezi hilo amesema amejifunza kuwa kuchanganya karanga wakati wa kusaga unga wa uji wa mtoto si jambo jema kiafya na badala yake achanganye karanga zilizosagwa peke yake wakati wa kupika uji
‘Binafsi nimefurahia nimejifunza kupika viazi mviringo vilivyopondwa, vimechanganywa na nyama na mchicha nilikuwa sijawahi kuona.alisema Sara
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wanaopinga udumavu mkoani Katavi (MICO) Evarist kabeja ambao wameshiriki katika uandaaji wa zoezi hilo wamesema lengo ni kuiwezesha jamii kufahamu makundi mbalimbali ya chakula
Amesema asasi inafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha mbogamboga, kufundisha mashuleni jinsi ya kulima mboga na matunda ili kuhakikisha jamii inapata mahitaji muhimu ya mwili
‘Unapomfundisha mwanafunzi wa shule ya msingi umuhimu wa mboga na matunda katika mlo hakika atahakikisha wadogo zake wanapata kula kama vyakula hivyo viko nyumbani’ alisema Kabeja
Dk. Yusta Tizeba ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Katavi, amesema hatua hii ya ufundishaji kinamama pia inafanywa katika wodi wanayolazwa watoto wenye udumavu
Ameeleza kuwa sababu kubwa ya watoto kupata udumavu ni tabia ya wazazi kuwaacha watoto wao wakijilea wenyewe wakati wao wakiwa katika sshguli za utafutaji kama kilimo na vibarua mbalimbali
‘Sasa utakuta baba, mama wamehamia shamba wameacha watoto hasa msimu huu wanakuja kurudi mwezi Mei au Juni wakiwa wamevuna mashamba yao, wakati huo wodi huwa inafurika watoto wenye lishe duni’ alisema Dk. Tizeba
Dk. Tizeba ametoa rai kwa jamii kujali familia zao na hasa zenye watoto wa chini ya miaka mitano kwani hao ndio idadi kubwa waathirika wa udumavu
‘Hao ndio waathirika wakubwa lakini watoto wa kuanzia miaka sita hadi nane hatuwapokei sana’ alisema Dk. Tizeba
Ameongeza wazazi walio wengi wa mkoa wa Katavi mtoto akishaaja kunyonya tayari anaingizwa katika kundi la watu wazima hali inayopelekea watoto kudumaa