Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga Shekhe Khamisi Balulisa akisaini kiatabu cha Maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Tanzania Marehemu Joseph Pombe Magufuli jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mjumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga Shekhe Soud Suleiman Kategire akisaini kiatabu cha Maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Tanzania Marehemu Joseph Pombe Magufuli jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela akisaini kiatabu cha Maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Tanzania Marehemu Joseph Pombe Magufuli jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Rasilimali Watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. James Bwana akisaini kiatabu cha Maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Tanzania Marehemu Joseph Pombe Magufuli jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu Shinyanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga Shekhe Khamisi Balilusa amesema taarifa za kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Dkt. John Pombe Magufuli zimeliweka Taifa katika mfadhaiko mkubwa kwa kuwa aliwafanya watanzania waishi katika malengo na makusudio ya mwenyezi Mungu.
Shekhe Balulisa alisema hayo jana alipofika kwenye Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Hayati Rais John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi mwaka huu.
Shekhe Balilusa alisema kuwa utendaji kazi wa aliyekuwa Rais Magufuli uliwafanya watanzania waishi maisha ya makusudio ya Mwenyezi Mungu yakujipatia kipato kutokana na kufanya kazi kwa kuwa Mungu hakumuumba mwanadamu kuishi bure bali ni kwa kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia vipato vya halali.
Aidha Shekhe Balulisa aliongeza kuwa Rais Magufuli aliwafanya watanzania wajitambue na kila mmoja wetu kujua nafasi yake na anawajibika na jambo gani ndio maana kifo chake kumetusonesha sana lakini kwa kuwa ni utashi wa Mwenyezi Mungu hatuna budi kulipokea jambo hilo.
Naye Askofu Raphael Machimu wa Kanisa la EAGT Tanzania amesema kuwa Msiba huu umekuwa mkubwa kutokana na mambo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiyafanya ambayo yamekuwa faraja kubwa hasa kwa watanzania wanyonge lakini kazi ambazo amekuwa akizifanya hakuna eneo ambalo halikuguswa na utendaji wake.
Askofu Machimu aliongeza kuwa Rais Magufuli atakumbukwa kwa yote aliyoyatenda na ameacha alama kubwa na kuongeza kuwa makanisani kote watu wanamuombea ili Taifa libaki katika utulivu wake kwa kuwa ni mshtuko mkubwa umetokea.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela ameviambia vyombo vya habari mkoani Shinyanga kuwa Serikali Mkoani Shinyanga imetenga eneo maalum kwa ajili ya wananchi wote mkoani Shinyanga kufika na kusaini kitabu cha maombelezo ya Hayati Rais Joseph Pombe Magufuli na kwamba kitabu hicho kitakuwepo kwa kipindi chote cha maombolezo hayo.
Bw. Msovela ametoa wito kwa wananchi wote mkoani Shinyanga kufika Ofisi za Mkuu wa Mkoa ili kusaini kitabu cha Maombolezo kwa kipindi hiki kigumu kwa kuungana na watanzania wengine ambao watakuwa wanafanya hivyo katika maeneo mengine kote Nchini.
Aidha Bw. Msovela ametoa pole nyingi kwa familia ya Rais na Wananchi wa mkoa wa Shinyanga kwa kuondokewa na kiongozi wetu mpendwa na kuongeza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetoa eneo la kusaini kitabu cha maombelezo ili kutoa fursa kwa wote watakao pata nafasi ya kufika kusaini kitabu hicho waweze kutoa rambirambi zao kufuatia kifo cha kiongozi wetu mpendwa.
Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na kusaini Kitabu cha Maombolezo lakini pia walitoa dua zao kuliombea Taifa katika kipindi hiki kigumu lakini pia kumuombea Marehemu Rais Joseph Pombe Magufuli ili apokelewe kwa amani Mbunguni.