*********************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WADAU wa madini ya Tanzanite wa kikundi cha Muungano na Mara Group wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameiomba Serikali kuwapiga picha na kuwazuia kuingia watu watakaokamatwa wakitorosha madini ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo.
Wadau hao waliyasema hayo kwenye mkutano wa kutoa elimu kwa jamii juu ya kupiga vita utoroshaji wa madini kilichofanyika Mji mdogo wa Mirerani.
Mwenyekiti wa Mara Group, Godwin Kosodo amesema kila mmoja atimize wajibu wake na mtu akikamatwa na madini achukuliwe hatua kwa kuzuiwa kuingia tena ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite.
“Watu wa Mara ni jamii kubwa akichafuka mmoja tunachafuka wote, hata wakikamatwa wengine hawatajwi kama tunavyotajwa sisi, hivyo hata mmoja akikamatwa anatorosha tunachanganywa wote, tuepuke hayo,” amesema Kosodo.
Askofu wa kanisa la Roho Mtakatifu, Boaz Ambonya ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa Manyara, amesema upekuzi wa kuvuliwa nguo unafanyika kutokana na watu wachache kushiriki wizi huo.
“Watu wanakuwa na watoto wao, kaka zao, baba zao, kisha wanapekuliwa uchi kwa sababu ya watu wachache, elimu inatolewa ila izidi kutolewa ili watu wawe waaminifu,” amesema Ambonya.
Mchuuzi wa madini hayo, Gerald Orinyo alisema mtu mmoja akikamatwa kutorosha asisababishe kuchafua jamii nzima ya Mara na kuonekana wote wanahusika na utoroshaji wa madini.
“Ni bora akapigwa picha na kuzuiliwa kuingia ndani ya ukuta kwani kuna baadhi ya watu wanawarubuni vijana wanatorosha madini badala ya kulipa kodi,” amesema Orinyo.
Hata hivyo, kaimu ofisa madini mkazi wa Mirerani, Ezra Gregory alisema amepokea mapendekezo hayo na atayafikisha kwa kiongozi wao Fabian Mshai.
“Sheria ipo wazi kuwa anayekamatwa akitorosha madini haruhusiwi kuingia ndani ya ukuta ila hawa waliokamatwa wanaomba msamaha Kisha wanaruhusiwa ila tutalifikisha kwa uongozi lifanyiwe kazi,” amesema Ezra.