Home Mchanganyiko TDA WATOA HUDUMA KWA WATOTO YATIMA IRINGA.

TDA WATOA HUDUMA KWA WATOTO YATIMA IRINGA.

0

**************************************

NA DENIS MLOWE, IRINGA

MADAKTARI bingwa kutoka Chama cha Madaktari wa kinywa na Meno nchini(TDA) katika kuelekea kilele Cha maadhimisho ya wiki ya afya ya kinywa na meno duniani wametoa bure matibabu kwa watoto 71 wanaoishi kwenye kituo cha watoto yatima cha Rahma Orphanage Center Cha mjini Iringa ambapo walitoa huduma za uchunguzi, matibabu na elimu kwa watoto hao na walezi wao.

Akizungumza Mara ya kutoa huduma kwa watoto hao, Rais wa Chama Cha Wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania Dk. Deogratius Kilasara alisema ziara hiyo imewapatia fursa madaktari hao kufanya uchunguzi wa kinywa pamoja na kutoa huduma za matibabu pamoja na elimu kwa watoto hao na mkoa wa Iringa kwa ujumla bila malipo.

Alisema miongoni mwa magonjwa yanayosumbua katika kinywa ni pamoja na kuoza na kutoboka kwa meno na ugonjwa wa fizi ambayo yanasababishwa na uchafu unaotokana na kutokupiga mswaki, kukosea kupiga mswaki au kutumia mswaki usiofaa.

Alisema ili wananchi waepukane na magonjwa hayo ya meno wanapaswa kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku na kujenga utaratibu wa kuangalia afya ya kinywa na meno mara kwa mara.

Alisema kuwa Hadi Sasa wamefanikiwa kuwapa huduma watoto 71 katika kituo hicho lakini kwa mkoa wa Iringa wamefanikiwa kuwafikia wananchi 1686 ambao wamepatiwa huduma ya afya ya kinywa na meno na upasuaji wa midomo wazi.

Dk. Kilasara alisema kuwa mikoa 26 inashiriki maadhimisho haya ambayo Ina lengo la kutoa elimu, kufanya uchunguzi na upasuaji wa midomo wazi katika afya ya kinywa na meno na kuwataka wananchi  kujitokeza kupata huduma hizo.

Alisema kuwa changamoto kubwa ni kwa wananchi kujitokeza mapema katika kupata huduma ya afya na kinywa Hali ambayo inaleta ukubwa wa tatizo na gharama kuongezeka tofauti wakiwahi matibabu.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kinywa na Meno wa Mkoa wa Iringa, Dkt Atupele Mandiga alisema kwa mkoa wa Iringa wameweka kambi katika vituo vya afya vya Ngome,Ipogoro na hospitali ya wilaya ya Frelimo ambapo watu wengi wamejitokeza kupata huduma.

Alisema kuwa uwingi wa watu waliojitokeza kupata huduma inatokana na kutoa matangazo sehemu mbalimbali Hali iliyofanya wakati mwingine kuelemewa na wagonjwa wanaotaka huduma ya afya ya kinywa na meno ambapo wananchi kutoka halmashauri zote wamefika.

Naye Mratibu wa Huduma za Afya ya kinywa na meno kutoka wizara ya Afya Tanzania  Dkt. Angelina Sijaona alisema Kama wizara wamejipanga kuboresha huduma za afya ya meno na kinywa kwa wananchi.

Alisema kuwa maadhimisho Kama haya Yana umuhimu mkubwa ikiwa inalenga kuwahamasisha wananchi kuzingatia afya ya kinywa na meno ili kujikinga na magonjwa yanayohusiana na ugonjwa wa meno ikiwemo magonjwa ya kisukari na mengine.

Aidha alitoa wito kwa madaktari wa mikoa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi angalau mara mbili kwa mwezi ili kuwaongezea ufahamu na uelewa wananchi juu ya usafi wa kinywa.