Rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini(TUCTA),Tumaini Nyamhokya akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani katika ofisi za shirikisho hilo Mnazi Mmoja Dar es salaam leo kuhusu kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Dk. John Pombe Magufuli.
Rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini(TUCTA),Tumaini Nyamhokya akijadiliana jambo na viongozi wenzake mara baada ya mkutano huo kumalizika leo kutoka kulia ni James Kalanje Mweka Hazina (TUCTA) na katikati ni Paul Sangezi Mwenyekiti (TUICO) Taifa..
………………………………….
SHIRIKISHO la vyama vya wafanyakazi nchini(TUCTA) ,limepokea taarifa ya msiba wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati John Magufuli kwa masikitiko makubwa.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya wafanyakazi wote nchini leo mkoani Dar es Salaam Rais wa Shirikisho hilo,Tumaini Nyamhokya amesema Hayati Magufuli alikuwa nguzo katika shughuli za wafanyakazi nchini kwa ukizingatia nafasi yake aliyekuwa nayo kama Mkuu wa nchi.
Amesema kwa nafasi ya Hayati Magufuli aliyokuwa mayo kama Mkuu wa nchini lakini alionyesha utu na binadamu katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wafanyakazi.
“Nachukua nafasi hii kutoa pole kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani,familia ya Marehemu na Watanzania wote kwa ujumla,”amesema na kuongeza
“Shirikisho litamkumbuka Hayati Magufuli kwa masuala mbalimbali wakiwemo Punguzo la kodi katika mshahara(PAYE)kwa mwaka 2016 na 2020 pia alisitisha utekelezaji wa kikokotoo kipya ambacho kilikuwa kinaathiri kiwango cha mafao ya uzeeni ya wafanyakazi na kurudisha kazini kwa baadhi ya wafanyakazi wenye elimu ya darasa la saba walioondolewa kwenye utumishi wa umma,”amesema
Aidha amesema pia kipindi cha Hayati Magufuli aliweza kuongeza ushirikishwa wa wafanyakazi sehemu za kazi kupitia UTATU na mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi .
Pia amesema aliweza kuongeza ajira kupitia utekelezwaji wa sera ya viwanda,miradi mbalimbali ya kitaifa na miundo mbinu ya huduma zakijamii nchini.
Amesema Shirikisho linaomba wafanyakazi wawe watulivu na kushiriki kikamilifu katika hatua zote za maombolezo na mazishi nchini huku viongozi wa Shirikisho hilo wanaoshiriki kuaga mwili wa Marehemu Kesho uwanjani wa uhuru na baadae kwenye mazishi.