Home Mchanganyiko Tanzania Kinara Programu ya Ukombozi wa Bara la Afrika

Tanzania Kinara Programu ya Ukombozi wa Bara la Afrika

0

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akielezea faida za Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika
********************************

 

Na Grace Semfuko, MAELEZO

 

Machi 10, 2021.

 

Katika Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika huwezi kuacha kuitaja Nchi ya Tanzania katika harakati zake za kulikomboa bara hilo kutoka kwa Wakoloni ambapo maera baada ya kupata uhuru  ndiyo nchi iliyosimamia kupatikana kwa uhuru katika baadhi ya nchi za bara hilo.

 

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania mara nyingi alizungumzia uhuru wa nchi za Afrika kwa kusema kuwa “Tanzania haitakuwa huru hadi nchi zingine za Afrika zitakapokuwa huru” nah ii ndio iliipa chachu ya nchi kuungana na mataifa mengine ya Afrika katika kuyakomboa kutoka utumwani.

 

Mwalimu na Watanzania waliungana na Wanaharakati wenzake akina Samora Mashel, Nelson Mandela, Kenneth Kaunda, Joaquim Chissano na wengineo wengi na kufanikisha nchi zote za Afrika kuwa huru.

 

Hivyo katika kuenzi historia ya viongozi hawa namna walivyokomboa bara hili kutoka kwa wakoloni, Mwaka 2003 wazo la utekelezaji wa programu hii lilibuniwa na Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lengo likiwa ni kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika hasa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

 

Pamoja na hayo Tanzania ilikuwa ni mwenyeji wa vikundi vingi vya wapigania uhuru na kutoa hifadhi ikiwepo Makao ya Kamati ya Ukombozi ya Bara la Afrika ambayo yapo Jijini Dar es Salaam ambayo iliratibu harakati zote za ukombozi.

Mratibu wa Programu hii ya Ukombozi wa Bara la Afrika iliyopo chini ya Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Boniface Kadili amesema Mwaka 2004 UNESCO iligharamia ujumbe wa Philip Mangula na wenzake ambao walikwenda Angola, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe kupata maoni ya wadau katika nchi hizo juu ya wazo hili.

 

Ujumbe huo ulipokelewa vema na nchi zote tano na ikapendekezwa kwamba mradi huo ujumuishe nchi zote za kusini mwa Afrika na utekelezaji wake usimamiwe na Tanzania kwa sababu, Tanzania ilitambuliwa na inatambuliwa kuwa ni mdau mkubwa wa harakati hizo. 

Bw. Kadili amesema lengo la programu hii ni kuanzisha kituo cha Kikanda cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambacho kwa mujibu wa makubaliano kitajengwa Jijini Dar es Salaam, Tanzania, ambako Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika utatekelezewa, kuenziwa na kuoneshwa kwa ulimwengu. 

Amesema kituo hiki kitakuwa na Makumbusho, Maktaba, Nyaraka, Sehemu ya Watafiti na Ukumbi ambapo katika kituo hicho kutakuwa na uhifadhi kumbukumbu zote (picha, filamu, simulizi, barua, machapisho, maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru, nyimbo, sare, ambapo Tanzania ndio iliyopewa usimamizi wa zoezi hili.

 
Mwaka 2005 nchi 11 ziliungana na Tanzania kuwasilisha pendekezo la kuanzishwa kwa programu hiyo kwa UNESCO, nchi hizo ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho, Mauritius, Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia, Swaziland, Zambia na Zimbabwe na baadae Mwezi Mei, 2010 Viongozi Wakuu wa vyama vya Siasa vilivyokuwa vya kupigania uhuru kusini mwa Afrika walikutana Jijini Dar es Salaam ili kuijadili Programu na hatimaye Mwezi Januari, 2011 Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika waliijadili Programu hii na kuipitisha. 

Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika una faida nyingi ikiwemo kuongeza ajira kwa wananchi, kuongeza pato kupitia Sekta ya Utalii pamoja na Wananchi kujua historia ya nchi zao katika harakati za ukombozi.

Programu hii ilizinduliwa Desemba 8, 2011 na Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete Jijini Dar es Salaam wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

 

Program hii imeandaliwa mpango mkakati wa ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha program katika eneo la Mabwepande Jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni ukusanyaji wa taarifa kwa watu waoshiriki katika harakati za ukombozi katika Bara la Afrika ambapo Wazee kutoka katika maeneo mbalimbali walihojiwa na mahojiano yao yamehifadhiwa kwa njia ya kidigitali.

Jumla ya Maeneo 255 ya kihistoria yanayohusu programu hiyo yamebainishwa hapa nchini na yanaandaliwa utaratibu wa kukarabatiwa ili kuhifadhi historia iliyomo katika maeneo hayo,baadhi ni Mazimbu,Dakawa,Kongwa,Lindi Farm 17,Kihesa Mgagao etc, Pia picha 4000 kuhusu historia ya ukombozi wa bara la Afrika zimekusanywa na kuhifadhiwa na Mafaili 900 yenye nyaraka mbalimbali zinazohusu programu hiyoa yamepatikana na kuhifadhiwa. 

 

Katika kuhakikisha Programu ya Urithi wa Ukombozi inaimarika Zaidi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wanaendelea kukamilisha Mitaala ya vitabu vya masomo ya historia ya Tanzania, ambavyo pamoja na mambo mengine, vitajumuisha mkusanyiko wa historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika na kutoa ufahamu kwa wanafunzi wa jinsi Tanzania ilivyojitoa katika kupigania uhuru wa nchi zingine.

 

Mpango huo pamoja na kusaidia kuendeleza historia ya nchi, pia utasaidia kutambua na kuenzi tamaduni za Tanzania, pamoja na mchango wa nchi katika kupigania uhuru wa nchi za Barani Afrika.

 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa Jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kufanyika kwa kongamano kubwa la kutambua na kuenzi mchango wa historia ya Tanzania, katika ukombozi wa Bara la Afrika, linaloandaliwa na Wizara hiyo kupitia program ya Urithi wa Ukombozi, litakalofanyika Machi 28 mwaka huu, katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere Mkoani Dar es Salaam.

 

Bashungwa amesema mchango wa Tanzania katika kulikomboa Bara la Afrika haupimiki wala kulinganishwa na thamani yoyote, kutokana na kuhusisha Watanzania kujitoa kwa uhai wao, Mali, vitu, na maarifa kwa ajili ya kuliweka Bara la Afrika kuwa huru na kuwataka  Watanzania kujivunia suala hilo.

 

“Mchango wa Tanzania katika kulikomboa Bara la Afrika haupimiki wala kulinganishwa na thamani yoyote, Watanzania tunapaswa kujivunia Utanzania wetu, nasisitiza haya kwa kuwa vijana wengi wa sasa bado hawajafahamu suala hili, ya kuwa Tanzania wakati wa ukombozi ilikuwa kama Macca au Jelusalemu ya Afrika, mchango wetu umetambulika duniani kote” amesema Bashungwa.

 

Amesema kutokana na mchango huo wa Tanzania kwa Afrika, Mwaka 1963 Umoja wa Nchi za Afrika Afrika uliekeleza Tanzania kuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Afrika hadi nchi ya Afrika Kusini ilipopata Uhuru Mwaka 1994 mwaka ambao Nchi zote za Afrika zilikombolewa.

 

“Kutokana na juhudi hizo Mwaka 2011 Umoja wa Afrika uliridhia Tanzania kuanzisha Makao Makuu ya kulinda, kuhifadhi na kuenzi Urithi wa Ukombozi wa Afrika kupitia program ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika  na kuzielekeza nchi wanachama wa umoja wa Afrika kushirikiana na Tanzania katika kuratibu program hii ambayo makao makuu yake ni Jijini Dar es Salaam” amesema.

 

Kongamano hilo la siku moja litajumuisha Wadau wa Ukombozi, wawakilishi wa Baadhi ya nchi zilizosaidiwa na Tanzania katika kupigania uhuru wao pamoja na wadau wengine huku wito ukiwa ni kwa watanzania kushiriki kwa wingi katika kongamano hilo.