Home Mchanganyiko WABUNGE WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI WAPONGEZA MGODI WA TANZANITE WA...

WABUNGE WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI WAPONGEZA MGODI WA TANZANITE WA FRANONE MINING

0
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiwa kwenye mgodi wa kampuni ya madini ya Tanzanite ya Franone Mining Ltd ya Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, walipotembelea eneo hilo.
Wakurugenzi wa kampuni ya mgodi wa madini ya Tanzanite ya Franone Mining Ltd, Onesmo Mbise (kulia) na Vitus Ndakize (kushoto) wakiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula (katikati) alipotembelea mgodi huo na wajumbe wa Kamati hiyo.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakishuka kwenye mgodi wa kampuni ya madini ya Tanzanite ya Franone Mining Ltd ya Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, walipotembelea eneo hilo, kushoto ni Mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo Vitus Ndakize.
*************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wameupongeza uongozi wa kampuni ya madini ya Tanzanite wa mgodi wa Franone Mining Ltd kwa uwekezaji mkubwa wa kisasa wa mgodi huo uliopo katika machimbo ya madini hayo Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Wajumbe hao wameishauri Serikali kuwapa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite ambao ni watanzania katika kuwekeza kuliko kutaka kuwapa wageni wachimbe madini ya vito.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Joseph Musukuma ameishauri Serikali kuwapatia wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani kitalu C, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwani wana uwezo mkubwa wa kuchimba.
Musukuma amesema baada ya kuingia na kutoka kwenye mgodi wa watanzania wazawa wa Franone Mining Ltd ameshuhudia miundombinu bora iliyofanywa na wachimbaji wazalendo hivyo hakuna haja ya kuwapa kitalu C wachimbaji wageni.
“Ukiondoa uwekezaji na hii miundombinu, huwezi kuufananisha mgodi huu na kiwanda cha mchele, vijana wadogo wa Kitanzania wamewekeza kwenye mgodi huu ni uwekezaji mkubwa tunamshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini Watanzania,” amesema Musukuma.
Amesema kutokana na uwekezaji huo uliofanywa na watanzania wazawa inabidi hata eneo la kitalu C ambalo hivi sasa halitumiki wapatiwe wachimbaji wadogo wazawa ili wachimbe na kulipa kodi kwa  serikali.
“Waziri wa madini Dotto Biteko, nakushauri kwenye kitalu C wape leseni wachimbaji wazawa, usiwape wageni kwani hapa kwenye mgodi wa Franone wamewekeza kitaalamu hapa,” amesema Musukuma.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Salimu Omary amesema wameridhishwa na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Franone Mining Ltd hivyo wachimbaji wadogo wapewe Kitalu C.
“Kumbe kuna watanzania wana uwezo mkubwa wa uwekezaji katika madini ya Tanzanite kwa kiasi hiki mimi nilizoea kuona kwenye runinga wachimbaji wa Afrika kusini kipindi kile,” amesema Omary.
Mjumbe mwingine Jesca Msavatavangu amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kupatiwa kitalu C ili wakiendeleze kwani mfano wameuona katika mgodi wa kampuni ya Franone Mining Ltd.
Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Franone Mining Ltd, Vitus Ndakize amesema uwekezaji uliofanywa kwenye mgodi huo ikiwemo miundombinu ni bora kuliko migodi yote ya Tanzanite.
“Tulishirikiana na mkurugenzi mwenzangu Onesmo Mbise kuwekeza katika mgodi huu na wafanyakazi wote ni watanzania hakuna mgeni hata mmoja na tunawashukuru wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa namna wanavyotupa ushirikiano,” amesema Ndakize.
Amesema mgodi huo una urefu wa zaidi ya kilomita moja na mita 200 ambapo huchukua muda wa dakika 13 kuingia mgodini na dakika nyingine 13 kupanda juu ya mgodi huo.
“Tumepata ujasiri baada ya kupata moyo kwa imani tuliyopewa na Rais John Magufuli ambaye amewaamini wachimbaji wadogo wa madini nasi tukafanikiwa,” amesema Ndakize.
Amesema malengo yao makubwa ni kuchimba madini kwenye nchi nyingine zaidi ya Tanzania hivyo watafanikiwa hilo kutokana na nia yao.
“Tulichimba mgodi huu kwa zaidi ya miaka mitano bila kupata uzalishaji ila miaka miwili iliyopita ndipo uzalishaji ukaannza kupatikana na tunalipa kodi Serikalini,” amesema Ndakize.
Amesema wanatarajia kuendelea kuchimba mgodi huo kisasa kwani walipopata nafasi ya wachimbaji wadogo kuaminiwa na Rais John Magufuli na kuwapa moyo kuwa watanzania wanaweza.