- Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka akizindua mradi wa maji wa kijiji cha Nduguti.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka katika picha ya pamoja na wananchi wa kijiji cha Nduguti wakifurahia uzinduzi wa mradi wa maji.
………………………………………………………………………….
Na Mohamed Saif
Hatimaye kero ya ukosefu wa majisafi na salama iliyokuwa ikiwasumbua wananchi wa vijiji vya Nduguti na Maziliga wilayani Mkalama, mkoani Singida imepatiwa ufumbuzi.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida, Mhandisi Jackson Masaka aliyasema hayo Machi 17, 2021 kijijini Nduguti alipokuwa akizindua mradi wa maji wa thamani ya shilingi milioni 980 unaonufaisha zaidi ya wakazi 7,000.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, Mhandisi Masaka aliipongeza Wizara ya Maji kwa utatuzi wa changamoto hiyo ambayo alisema ilichangia kuzorotesha maendeleo kwa wananchi wa Nduguti.
“Mradi huu ninaozindua leo ni ufumbuzi wa changamoto iliyokuwa ikitukwamisha kujiletea maendeo. Sasa hatuna kikwazo, tuchape kazi,” alisema Mhandisi Masaka
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Mkuu wa Wilaya, Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Antidius Muchunguzi alisema uligharamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji.
Mhandisi Muchunguzi alisema umejengwa na Mkandarasi Nyakire Investment Ltd na alibainisha kwamba ulianza kutekelezwa mwezi Juni 2018 na ulikamilika rasmi Desemba, 2020.
Aliongeza kwamba tayari mradi umeanza kutoa maji na wananchi wanapata maji yanayotosheleza, hata hivyo alisema wanaendelea na utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa miundombinu.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa mradi wa maji wa Nduguti inakwenda sambamba na uzinduzi wa miradi na uwekaji wa jiwe la msingi maeneo mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka 2021.
#WikiYaMaji2021