……………………………………………………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Iddi Kimanta ametoa wiki moja kwa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira(AUWSA), mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) pamoja na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kueleza mpango kazi wa kuhakikisha vijiji 86 vya mkoa huo vinapata maji kabla ya 2025.
Kimanta alitoa agizo hilo katika mwendelezo wa kikao cha maji kilichofanyika ofisi kwake na kusema kuwa mkoa wa Arusha una vijiji 390 ambpo kati ya vijiji hivyo vijiji 304 vimeshafikiwa na huduma ya maji huku 86 vikiwa bado na changamoto kubwa.
Alisema kati ya vijiji hivyo 86 ambavyo havina maji vijiji 23 vitashughulikiwa na AUWSA, kumi na moja vikiwa vimepitiwa na mradi mkubwa wa maji wa billion 520 na vijiji 12 vya wilaya mbalimbali ambavyo wamepewa jukumu la kusimamia miradi na wizara ya maji.
Alieleza mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inatakiwa kushughulikia vijiji 12 vilivyopo ndani ya mamlaka hiyo pamoja na RUWASA kushughukia vijiji vilivyobaki kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi.
“Tunataka kuona ni kwa namna gani tutatekeleza maagizo ya serikali kwani Hadi kufikia mwaka 2020 upatikanaji wa maji ulitakiwa uwe asilimia 85 lakini mpaka sasa tupo asilimia 66.2,”Alisema Kimanta.
Alifafanua kuwa kila mmoja anatakiwa kueleza katika eneo lake ni namna gani watahakikisha wananchi wa mkoa wa Arusha wanapata maji kabla ya muda uliopangwa ambapo pia vijiji 15 ambavyo vitashughulikiwa na RUWASA chanzo maji kutakuwa ni mradi mkubwa wa maji.
Kwa upande wake mkurugenzi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Mhandisi Justin Rujomba alisema kuwa katika mradi mkubwa wa maji wa billion 520 lita million 17 zimeshaingia katika mtandao wa maji ambapo wanatarajia kuukamilisha rasmi October mwaka huu.
Mhandisi Rujomba alisema kuwa wamepokea vijiji 23 ambapo baadhi vimeshapata maji na vingine vikiwa wameshapokea mabomba na kuyatandaza ikiwa ni pamoja na namanga na mji mdogo wa Mererani ambako pia wamekabidhiwa jukumu la kuhakikisha maji yanafika katika maeneo hayo.
Naye Meneja wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini Mhandisi Joseph Makaidi alisema kuwa Tatizo kubwa no upatikanaji wa vyanzo vya maji katika maeneo mengi ambapo kwasasa wana vijiji 25 huku 11 vikiwa tayari kwenye mpango.