Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Mamlaka hiyo Mabibo jijini Dar es salaam mara baada ya waandishi hao kufanya ziara ya kimafunzo katika maabara ya TMDA.
Meneja wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)Gaudensia Simwanza akiwatambulisha waandishi wa habari kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo kabla ya mkurugenzi huyo kuzungumza nao.
……………………………………
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ,Adam Fimbo amesema Mamlaka hiyo haiwezi kuanzisha maabara kila mkoa au kanda kwa sababu maabara zilizopo ni bora na zinafanya uchunguzi wa viwango vya juu.
Tunazo maabara mbili kubwa na maabara zingine hamishika 25 ambazo zinatosheleza kwa kwa kutoa huduma bora na umahiri wa kimataifa katika uchunguzi wa kimaabara hapa nchini.
Amesisitiza kuwa kule kwenye mikoa hizi maabara hamishika ndogondogo 25 zinafanya (Screening) kujua kama kuna shida kwenye bidhaa na bidhaa zikigundulika hazijakidhi viwango vya ubora basi sampuli hupelekwa katika maabara kuu za Mwanza na Dar es salaam kwa uchunguzi zaidi.
“Kazi ya maabara hizi hamishika 25 ni kupima sampuli za Bidhaa mbalimbali za dawa na vifaa tiba kwa hatua za awali na kama kuna viashiria vyovyote kuwa bidhaa hizo zimekidhi viwango vya ubora au ziko chini ya kiwango,”amesema Fimbo.
Ameongeza kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa na utaratibu wa kukagua na kuthibitisha umahiri wa hizi maabara mbalimbali Duniani kote ambapo kwa nchi za Afrika Tanzania ni moja kati ya nchi chache iliyothibitishwa kuwa na maabara zenye ubora hivyo kupelekea baadhi ya nchi za Afrika kuleta Sampuli zao kwa ajili ya kuchunguzwa.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TMDA alikuwa akizungumza hayo wakati akijibu moja ya swali la mwandishi katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ofisi za mamlaka zilizopo Mabibo jijini Dar es salaam aliyetaka kujua kama kuna mpango wa kuanzisha maabara zingine katika Kanda zilizobaki na mikoa.
“Tunazo Maabara kubwa mbili ya Kanda ya Ziwa Mwanza na ya Dar es salaam na tunajenga maabara nyingine ndogo jijini Dodoma hivyo tunadhani hizi maabara zinatosha na zinafanya kazi nzuri katika uchunguzi wa kimaabara,” anasema Adam Fimbo.
Amesema kutokana na umahiri na ubora wa maabara za Mamlaka hiyo zimeweza kutoa huduma ya upimaji wa sampuli mbalimbali kutoka Katika nchi tofauti za Afrika.
Ameongeza kuwa Nchi hizo ni pamoja na Zambia, Lesotho, Malawi, Uganga na Kenya na kwamba hilo limewezekana kutokana na kutangazwa na shirika la Afya Duniani (WHO)
“Kuna viwango vilivowekwa na shirika la afya duniani (WHO) ambavyo ukifikia hivyo viwango wanakutangaza na kukupa cheti na sisi tumepewa hii imetufanya kuaminika na nchi nyingine kutaka kujifunza kwetu na kuleta Sampuli zao nchini Tanzania kwa ajili ya uchunguzi,” amesema Fimbo.