Mkuu wa Kitengo cha Fedha benki ya UBA Tanzania Chomete Hussein akichangia mada juu ya jinsi wafanyakazi Wanawake wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi, na kuweka usawa wa maisha ya kawaida na maisha ya kazi ikiwa ni njia ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya Mwanamke duniani ambayo benki hiyo iliandaa kwa wateja, wafanyakazi pamoja na Watanzania kwa ujumla jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Mkuu Mwendeshaji wa UBA, Flavia Kiyanga.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano benki ya UBA Tanzania Brendansia Kileo akichangia mada juu ya jinsi wafanyakazi Wanawake wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi, na kuweka usawa wa maisha ya kawaida na maisha ya kazi ikiwa ni njia ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya Mwanamke duniani ambayo benki hiyo iliandaa kwa wateja, wafanyakazi pamoja na Watanzania kwa ujumla jana jijini Dar es Salaam.
………………………………………………..
KUFUATIA siku ya wanawake Duniani inayoadhimishwa terehe 8 mwezi wa 3 kila mwaka, United Bank for Afrika (UBA) imeandaa mkakati wa kuzisaidia familia kuweka usawa wa maisha ya kawaida na maisha ya kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa kitengo cha Masoko na mawasiliano, Brendansia Kileo alisema katika kuweka usawa wa maisha ya kawaida na maisha ya kazi wamewashirikisha na wanaume ili kuweza kupata mawazo mbalimbali.
“Tumewajumuisha wanaume ili kuweza kupata mawazo wanayoyafikiria katika kushirikiana na kuwaunga mkono wanawake ili kuweza kutimiza ndoto zao na majukumu yao wakati wanapokuwa nyumbani na kazini”.
Aidha Alisema kutokana na baadhi ya wanawake kwenye jamii wanashindwa kutimiza ndoto zao kwa kuzidiwa na majukumu ya kazi hivyo UBA wameandaa mikakati mbalimbali ambayo itawasaidia kufikia malengo ya wakinamama hao.
“Kwenye jamii tunaona wanawake wengi wakishindwa kutimiza ndoto zao au kuzidiwa na majukumu ya kazi, wanaume wengi hawatoi ushirikiano inavyotakiwa kuhakikisha ndoto hizo zinafikiwa, lakini sisi kama Bank ya UBA tunamikakati mbalimbali ya kuwaweka wanawake pamoja kwa ili waweze kushirikiana na kupata ushauri kuweza kutimiza ndoto zao na kutatua changamoto mbalimbali zinazotokea kwenye maisha yao na kuendeleza gurudumu la mafanikio”
Naye Mkuu wa Idara ya fedha, Hussein Chomete alisema ili kuweka usawa wa maisha ya kawaida na maisha ya kazi, kinachotakiwa ni kuweka uwazi kwenye familia, kuwa na ushirikiano wa baba, mama na watoto kwa ujumla ambapo kwa kufanya hivyo majukumu ya utendaji kazi yatakuwa ni marahisi.
Katika hatua nyingine kwenye mjadala huo uliofanywa amabao unahusu usawa wa maisha ya kawaida na maisha ya kazi Chomete alisema kama baba ana jukumu la kuhakikisha mama anaweza kufikia malengo na ndoto za maisha yake.
Aidha aliendelea kwa kuzisihi familia na kusema kuwa zihakikishe zinatoa ushirikiano kwa pande zote ili kuweza kufikia ndoto na familia isiwe chanzo cha kuvunja malengo.
Naye Afisa Mkuu Mwendeshaji wa UBA, Flavia Kiyanga alisema Mama ni mtu ambaye anawajibu mkubwa kwenye familia kwasababu maisha ya Kiafrika mama anatakiwa kuangalia nyumba, watoto na kila kitu kinachotakiwa kwenye familia kuhakikisha kimefanyika vizuri na kwa kiwango ambacho Jamii inategema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Umma Mathias Ninga alisema ni kweli kwamba Baba ni kichwa cha familia lakini kwa upande mwingine Baba na mama wote ni vichwa vya familia, hivyo fedha atakayoipata mama na baba ikiwekwa kwa pamoja ikatumika katika majukumu ya familia itasaidia na kufanya hata ikitokea mmoja wapo siku amepungukiwa fedha mwingine anachukua nafasi yake ipasavyo.