Afisa Sheria wa OSHA, Ally Mwege, akiwasilisha mada katika semina kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi iliyotolewa na OSHA kwa Mawakili wa Serikali katika ofisi za OSHA za Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akifungua semina kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ilitolewa na OSHA kwa Mawakili wa Serikali katika ofisi za Taasisi hiyo za Dar es Salaam.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Andrew Massawe, akifunga semina kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi iliyotolewa na OSHA kwa Mawakili wa Serikali katika ofisi za Taasisi hiyo za Dar es Salaam.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Andrew Massawe (Katikati), Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (Kushoto) na Kamishna wa Kazi, Brigedia Jenerali, Francis Mbindi (Kulia) wakiwa katika semina kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ilitolewa na OSHA kwa Mawakili wa Serikali.
******************************************
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Andrew Massawe, ameziagiza Taasisi chini ya Wizara hiyo kuvihusisha vyombo vya sheria katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta usawa na uwajibikaji miongoni mwa Taasisi husika na wadau wao.
Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Idara ya Kazi, Tume ya Uamuzi na Usuluhishi (CMA), Mfuko wa Hifadhi kwa Jamii wa Sekta Binafsi (NSSF), Mfuko wa Hifadhi kwa Jamii wa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Maagizo hayo ameyatoa alipofunga semina kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ambayo ilitolewa na OSHA kwa Mawakili wa Serikali chini ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP).
Katibu Mkuu huyo amesema Taasisi hizo zinapaswa kushirikiana na vyombo hivyo vya dola kwa kutoa mafunzo kwa watumishi mbali mbali katika vyombo hivyo ili kuleta uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa sheria mbali mbali ambazo utekelezaji wake unasimamiwa na Taasisi hizo.
“Kunakuwa na ugumu endapo kila Taasisi itapambana peke yake katika kushughulikiwa masuala mbali mbali ya kisheria yanayoihusu hivyo ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa sheria zenu ni muhimu sana kuvishirikisha vyombo vya kisheria vya serikali ikiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Wakili wa Serikali (Solicitor General), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Attorney General) na Jeshi la Polisi,” alieleza Katibu Mkuu huyo.
Akifungua semina hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja baina ya OSHA na Mawakili wa Serikali ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria husika.
“Tunaamini kwamba kupitia mafunzo haya ya leo mtapata kufahamu kwa undani dhumuni kuu la Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na pia namna ambavyo OSHA inasimamia utekelezaji wa sheria husika na hivyo tutaweza kushirikiana vizuri katika kuhakikisha kwamba sheria inatekelezwa ipasavyo,” alisema Mwenda.
Baadhi ya Mawakili wa Serikali walioshiriki katika semina wakiwemo Adolf Verandumi, Mkunde Mshanga na Esther Chale wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa kuandaa mafunzo hayo. Aidha, wameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wamejifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia katika kusimamia mashauri mbali mbali yanayohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
“Kimsingi semina hii imetufungua na kutupatia mwanga katika changamoto ambazo tumekuwa tukikumbana nazo katika kushughulikia mashauri yanayohusu Usalama na Afya mahali pa kazi. Kwahiyo, tunashauri semina kama hizi ziweze kuwa endelevu na zifanyike pia kwa makundi mbali mbali na wadau tofauti tofauti,” alieleza Esther Chale ambaye ni Wakili wa Serikali.