**********************************************
Mbunge wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika zoezi la ugawaji wa vifaa vya Michezo kwa vilabu vya mkoa wa Mwanza vinavyojihusisha na michezo ya mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa wavu na mpira wa kikapu linalotarajiwa kufanyika siku ya kesho jumamosi katika viwanja vya Sabasaba wilaya ya Ilemela mapema asubuhi.
Akizungumza akiwa ofisini kwake, Mratibu wa zoezi hilo ambae pia ni Afisa Michezo wa manispaa ya Ilemela Mwalimu Kizito Bahati Sosho amesema kuwa zoezi hilo linatekelezwa kwa ushirikiano wa taasisi tatu zikiwemo Sport Charity Mwanza, The Angeline Foundation na Serikali kupitia manispaa hiyo ambapo vifaa vya michezo ikiwemo mipira vitagawiwa kwa vilabu mbalimbali vya michezo vilivyopo ndani ya mkoa huo ikiwa ni hatua katika kuhakikisha sekta ya michezo inaimarika na kuifanya kuwa sekta rasmi katika kukuza uchumi wa wananchi na kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na vifaa kwa wanamichezo wa mkoa huo
‘.. Kama mnavyojua mbunge wetu ni mdau mkubwa wa michezo, anapenda sana michezo na mara zote tumeshirikiana nae katika kutatua changamoto zinazotukabili katika sekta hii ya michezo hivyo tumemuomba kesho tuwe nae katika kuendeleza michezo ndani ya wilaya yetu na mkoa kwa ujumla ..’ Alisema
Mwalimu Kizito akaongeza kuwa mbali na ugawaji wa vifaa hivyo wataendelea kuendesha mashindano mbalimbali ya michezo ndani ya manispaa ya Ilemela ikiwemo mashindano ya michezo kwa shule za sekondari, shule za msingi, mashindano ya Jimbo cup yanayotoa fursa kwa timu za mtaani na mengineyo ili kuzalisha vipaji vipya sanjari na kuendeleza vile vya zamani ili wilaya hiyo iendelee kuwa kinara kwa kutoa wanamichezo wazuri na tegemezi kwa taifa.