Home Mchanganyiko SIDO YAWANOA MAFUNDI WA MITAANI

SIDO YAWANOA MAFUNDI WA MITAANI

0

Afisa Uendeshaji wa Biashara, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO),mkoa wa Morogoro, Grace Makoye, akizungumza na mafundi nguo jana wilayani Kilosa wakati wa mafunzo kwa mafundi  waliojifunza fani za ufundi katika mifumo isiyo rasmi.

***********************************

NA VICTOR MAKINDA.MOROGORO

Imeelezwa kuwa mafundi wengi waliojifunza ufundi kupitia mifumo isiyo rasmi (mitaani), wanafanya kazi kwa mazoea huku wakiwa hawazijui kanuni  na misingi ya fani husika.

 Haya yalielezwa jana wilayani Kilosa na  Afisa Uendeshaji wa Biashara, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO),mkoa wa Morogoro, Grace Makoye, wakati wa mafunzo kwa mafundi  waliojifunza fani za ufundi katika mifumo isiyo rasmi.

“ Mafundi wengi waliojifunza ufundi kwa mifumo isiyo rasmi, hawajui  misingi, kanuni za ufundi, uzalishaji wa bidhaa bora, huduma bora kwa mteja na nidhamu ya fedha, hivyo wanafanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea ujuzi wao kudumaa na kutopiga hatua kibishara.” Alisema Makoye.

Makoye aliongeza kusema kuwa mafunzo hayo yanayotolewa kwa mafundi waliojifunza katika mifumo isiyo rasmi ni mwendelezo wa mafunzo yaendeshwa na SIDO chini ya Program ya Mafunzo ya ujuzi  na uboreshaji wa bidhaa za mafundi wadogo (Artisan) wa fani mbali mbali.

“ Hapa tunao mafundi  70 kutoka maeneo tofauti wilayani Kilosa ambao ni  mafundi wa fani za uselemala, ushonaji, uchomeleaji na mafundi wa bidhaa za ngozi ambao tunawapa ujuzi na kuwafundisha kanuni  na stadi za ufundi ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa na hivyo wakuze uchumi wao na uchumi wa Taifa kwa ujumla” Aliongeza kusema Makoye.

 Makoye alisema kuwa SIDO ina uzoefu mkubwa wa kufundisha stadi za ufundi hivyo ilibaini kuwa mafundi ambao hawapitii mafunzo rasmi ya ufundi kwenye vyuo vya ufundi wanakosa ufanisi na kutambua misingi ya utendaji kazi na hivyo hufanya kazi kwa mazoea.

 Aliitaja misingi muhimu ya kazi za ufundi kuwa ni pamoja na mafundi kuwa na uwezo wa kuzalishaji  bidhaa zinazokidhi viwango na mahitaji ya soko, mafundi kuwa wakweli kwa wateja na umahiri wa kumuhudumia mteja sambamba na stadi za maisha.

 Alisema kuwa pia mafundi waliojifunza kwenye mifumo isiyo rasmi, hawafuati na hawasimamii masharti na kanuni za viwandani hivyo kupelekea kuhatarisha afya zao na wateja wao sambamba na kutumia gharama kubwa za uzalishaji.

 “ Huwezi kukua kibiashara kama huzingatii kanuni za kibiashara. Mafundi ni wajasiriamali walio katika kundi la wazalishaji wa viwandani hivyo wanapaswa kujua mbinu bora za kijasiriamali ili wazalishe bidhaa zenye ubora na kwa wakati”. Aliongeza kusema Makoye.

 Makoye alisema kuwa katika mafunzo hayo wamelenga kubadili mitazamo ya mafundi juu ya utendaji wa kazi, faida na umuhimu  kujiunga katika vikundi vya wajariamali, namna ya kupata mikopo, stadi za maisha, afya na  nidhamu ya fedha.

Naye Mwasibu wa SIDO Mkoa wa Morogoro,  Chichili Mlambeni, akizungumza  kwenye mafunzo hayo alisema kuwa SIDO haiishii tu kuwafundisha mafundi na wajasiriamali wengine ujuzi, mbinu na kanuni za kibiashara bali pia inatoa  mikopo ya riba nafuu kwa wajasiriamali wa makundi mbali mbali.

“ SIDO tunatoa mikopo yenye riba nafuu na kwa vigezo vyepesi kwa  mjasiriamali mmoja mmoja , makundi ya wajasiriamali wazalishaji wa viwandani, wachuuzi, wanaotaka kufufua na kuendeleza biashara pamoja na wasasiliamali waliokosa vifaa vya uzalishaji “ Alisema Mlambeni.

 Mlambeni aliitaja faida ambayo mjasiriamali ataipata pindi atakapokopa SIDO kuwa ni kupata elimu na maarifa ya kibiashara na  kuunganishwa na taasisi kubwa za kifedha kwa ajili ya mikopo mikubwa.

 Akitoa shukrani zake kwa SIDO, Neema Mathias mmoja wa mafundi kushona wanaohudhuria mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwake kwa kuwa amejifunza mbinu na kanuni ambazo alikuwa hazijui.

“ SIDO wamebadili mtazamo wangu juu ya kazi yangu ya ufundi nguo. Nikirudi nyumbani nitaacha kufanya kazi kwa mazoea, kwa kuwa  nimeongezewa ujuzi, nimefundishwa kanuni na misingi muhimu ya kuzingatia kwenye ufundi sambamba na namna ya kutafuta masoko, kuwa mkweli kwa mteja na kutangaza biashara yangu.” Alisema Neema.