Kaimu Mkurugenzi wa Akiba Commercial Bank Bi. Juliana Swai akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya benki hiyo mtaa wa Ohio jijini Dar es salaam wakati alipomtangaza mbia mpya wa benki hiyo leo jumatano Machi 3,2021, Kushoto ni Dora Saria Kessy Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano.
Kaimu Mkurugenzi wa Akiba Commercial Bank Bi. Juliana Swai na Dora Saria Kessy Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wakinnyanyua mikono yao kwa pamoja kama ishara ya mafanikio kwa benki hiyo mara baada ya kumtangaza mbia wao mpya katika biashara benki ya Malawi.
…………………………………………….
Benki ya Akiba Commercial ya nchini Tanzania (ACB) imepata mbia wa kimkakati yaani (Strategic Investor) ambaye ni National Bank of Malawi (NBM)ya nchini Malawi itakayowekeza katika benki hiyo ili kuongeza mtaji wake.
Hii ni mikakati mbalimbali ya kimaendeleo ndani ya Benki ya Akiba ambayo itapelekea kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya kifedha kwa benki hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya benki hiyo mtaa wa Ohio jijini Dar es salaam leo Kaimu Mkurugenzi wa Akiba Commercial Bank Bi. Juliana Swai amesema Kupitia mbia huyu Benki ya hiyo sasa imeweza kuimarisha mtaji wake na kukidhi vigezo vya Benki Kuu kuhusiana na swala zima la mtaji wa uendeshaji wa Benki ya Biashara baada ya mbia wake NBM kuwekeza kiasi cha shilingi za Kitanzania billion 17.
Amesema lengo kuu la mkakati huu ni kuimarisha mtaji wa Benki. Lakini pia benki imekuwa ikiangalia mahitaji ya soko lake na kuona kuwa kuna haja ya kupata mwekezaji au mbia wa kimkakati kwa ajili ya kuifanya benki iwe imara zaidi na kuweza kuboresha huduma zake na kuanzisha huduma nyingi zaidi ambazo zinahitajika kwenye soko la Tanzania
“Kupitia Ubia huu naomba niwaahidi wateja wetu na Watanzania wote kwa ujumla mabadiliko makubwa na chanya katika huduma zetu na mifumo yetu ya utoaji huduma yanakuja. Tunaamini kuwa tutaweza kuwahudumia wateja wetu kwa weledi zaidi kupitia utalaamu na uzoefu wa taasisi mbili hizi bobezi kwenye sekta ya fedha” amesema Bi Juliana Swai
Ameongeza kuwa benki hiyo inatambua mahusiano mazuri na undugu kati ya nchi hizi mbili ambazo pia zina mahusiano makubwa ya kibiashara na faida mojawapo ya wazi ni kuwepo kwa mazingira wezeshi ya kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili kupitia huduma za kifedha ambazo zitapatikana kwa urahisi zaidi.
Bi Juliana amesema aidha uwekezaji huu utasaidia pia kuwepo kwa mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara kwa nchi ambazo zipo kusini mwa bara la Afrika wakiwepo wanachama wa SADC
Malawi ni moja ya nchi zilizoko kusini mwa Afrika zinazotumia bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la kibishara hii itarahisisha huduma za kifedha kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Malawi wanaotumia bandari ya Dar es Salaam .
NBM ilianzishwa mwaka 1971 baada ya muungano wa Barclays Bank DCO na Benki ya Standard ya Afrika Kusini, ni moja ya benki kubwa nchini Malawi inayotoa huduma za benki ikiwemo rejareja yaani (Personal and Retail banking), wateja wakubwa (Corporate banking), huduma za kibenki za uwekezaji na udalali katika soko la hisa na mitaji.
Sasa Akiba Commercial Benki imekuwa mhimili imara katika sekta ya fedha na imefungua ukurasa mpya kibiashara. Nawakaribisha Watanzania wote wafike Akiba Commercial Bank ili waweze kufaidika na fursa mbalimbali kwa maendeleo ya maisha yao na biasharazao
Akiba Commercial bank ni Benki ya biashara ambayo tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1997 imekuwa ikitoa huduma zake kwa wateja wengi wakiwani wajasiriamali wadogo, wakati na wajuu;yaani Micro, Small and Medium entrepreneurs (MSMEs)
Benki imeweza kuwafikia zaidi ya Watanzania 200,000 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, na Dodoma. Watanzania hawa wameweza kufaidika na huduma za mikopo mbalimbali ya kijasiriamali,pamoja na kuweka amana zao benki kwenye akaunti kulingana na matakwa yao. Aina za akaunti ni kuanzia zawatoto wadogo, vijana,watu wazima, na za biashara na makampuni. Aidha, huduma za benki kupitia simu za mikononi yaani Akiba Mobile zimeleta unafuu na urahisi zaidi katika kuwafikia wateja wetu popote pale walipo.