Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (katikati) akiwasili kukagua hoteli ya Nyota 3 ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania ( TANAPA) inayojengwa wilayani Chato mkoani Geita wakati wa Ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mkoani Geita. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Eng. Charles Kabeho na kulia ni Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Robert Gabriel kuhusu mpango wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa kutaka kuanzisha Utalii wa Madini katika mkoa huo wakati wa Ziara yake ya Kikazi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (kulia) akiwa anashuka kwenye hoteli ya Nyota 3 ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania ( TANAPA) inayojengwa wilayani Chato mkoani Geita wakati wa Ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mkoani Geita. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Eng. Charles Kabeho.
………………………………………………………………………………………………………
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amefanya Ziara katika mkoa wa Geita ambapo pamoja na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali ya Kiutalii inayotekelezwa na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii mkoani humo. Akiwa katika ziara hiyo amefanya mazungumzo na viongozi wa Serikali wa mkoa wa Mwanza na wale wa Taasisi zilizo chini ya Wizara kuhusu namna bora ya kutangaza Vivutio vya Utalii Vinavyopatikana katika mkoa huo.
Aidha, Mhe. Masanja ametembelea Mradi wa Ujenzi wa hoteli ya Kitalii ya Nyota 3 inayojengwa wilayani Chato mkoani Geita na kuagiza ujenzi wa hoteli hiyo ukamilike haraka ili watalii waanze kupata fursa ya kutumia huduma za malazi katika hoteli hiyo na kutembelea Hifadhi mbalimbali zilizopo kanda ya Ziwa.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha shughuli za Utalii zinasonga mbele huku akitoa rai kwa Viongozi hao kuweka mkazo katika zao la asali ambalo amesema likisimamiwa Vizuri litaongeza mapato ” Tuhamasishe zao la asali linalotokana na Nyuki, sasa hivi kuna mnyororo mkubwa wa thamani ambao serikali inaendelea kuupigania kwenye mazao ya Misitu, hii itasaidia wananchi kuongeza kipato pia Pato la Taifa ” Amesema Mhe. Mary
Aidha, ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii iko katika mpango wa kuanzisha Utalii wa Madini ambao kwa Kanda ya Ziwa utasaidia kuongeza idadi ya Watalii na Mapato.