*********************************************
Na Damian Kunambi, Njombe.
Kapteni wa meli ya MV Mbeya Two Nyabunya Nyatororya ameiomba serikali kupitia mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 300 ili waweze kufanya kazi katika mazingira ya usalama zaidi.
Akizungumza hayo mbele ya mbunge huyo, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Wise Mgina pamoja na kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi wilaya walipofanya ziara katika meli hiyo majira ya saa mbili usiku katika bandari ya Manda Nyatororya amesema anaiomba serikali kuwasaidia kupata map reading, minara katika kila bandari inaposimama meli hiyo ikiwemo radio za mawasiliano pamoja na maboya.
Amesema kutokana na mapungufu hayo walipaswa kufanya safari nyakati za mchana tu lakini kutokana na kuwasaidia wananchi kupata huduma na kuwahi maeneo wanayoenda inawalazimu kusafiri hata nyakati za usiku japo ni hatari hivyo inawabidi kutumia hisia na uzoefu katika kutia nanga katika bandari pasipo kujua kina cha maji katika eneo husika kwani hakuna vitendea kazi vya kuwaonyesha mazingira halisi ya kina hivyo serikali iwasaidie .
Ameongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo hasa ya map reading imemlazimu kutumia uzoefu alionao katika shughuli hizo za kuongoza meli ambapo amebuni namna ya kuseti mitambo ili kumsaidia kumpa muongozo hivyo analazimika kutolala usingizi muda wote ili kufuata muongozo huo ambapo kwa ubunifu alioufanya hakuna kapteni yoyote anaweza kutumia muongozo huo.
“Hizi changamoto katika shughuli hii ni kubwa sana na inatufanya tufanye kazi katika mazingira magumu kwani inanilazimu kukaa macho muda wote kwaajili ya kuongoza meli na ninapozidiwa na usingizi ninalazimika kumuweka mtu kwa muda asimamie ili na mimi nijiegeshe kidogo kitu ambacho endepo changamoto hizo zingetatuliwa tungeongoza meli hii katika mazingira yaliyo salama”, Alisema Nyatororya.
Sanjari na changamoto hizo Nyatororya ameipongeza serikali kwa kuleta huduma hiyo ya meli ambayo inahuduma nzuri kuliko meli za maeneo yote hapa nchini hivyo amewaasa wananchi kuitumia vyema bahati hiyo waliyoipata.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema amezepokea changamoto hizo na atapaza sauti yake katika kuzisemea ili ziweze kutatuliwa.
Pia ameishukuru serikali ya rais John Pombe Magufuli kwa kuwasaidia kupata huduma hiyo ya usafiri wa majini kwani katika jimbo lake kuna kata nane ambazo zipo pembezoni mwa ziwa hilo zikiwa na jumla yawakazi 23,552 hivyo usafiri huo ni msaada mkubwa kwao.
Amesema idadi hiyo ya watu ni kubwa sana hivyo anaomba kuongezwa kwa kituo kingine cha abiria ambacho amependekeza kiwepo katika kata ya Makonde kwakuwa kata hiyo ina wakazi zaidi ya 8000 hivyo endapo kitawekwa kituo hicho itawasaidia wakazi hao kusafiri kwa urahisi ikiwemo kusafirisha mizigo.
“Wananchi wangu wa kata ya makonde wamekuwa wakiniomba sana niwaombee kituo cha meli katika kata yao sasa na mimi naanza kuwasilisha ombi hili kwako kapteni na ndiomaana nimekuvizia mpaka masaa haya ili niwasilishe ombi hili na kama utaona huusiki na suala hili niambie niende wapi ilimradi ombi la wananchi wangu liweze kufanyiwa kazi”, Alisema Kamonga.
Nyatororya alikubali ombi hilo kwa kusema kwa upande wake yuko tayari lakini mbunge huyo anapaswa kuwasilisha ombi lake katika uongozi wa meli hiyo kwakuwa yeye ni mwanajeshi aliyekodiwa kwaajili ya kuendesha shughuli hiyo hivyo endapo uongozi wake utakubaliana na ombi hilo yeye yuko tayari kupita katika kituo hicho cha makonde.