Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse akikagua banda la shirika hilo katika maonesho ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika sekta ya Madini Tanzania unaofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere Posta jijini Dar es salaam.
Mmoja wa wachimbajiakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Stamico wakati alipotembelea banda hilo.
……………………………………..
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na kampuni yake tanzu ya STAMIGOLD Biharamulo Mine wameendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wanaoendelea kutembelea banda sambamba na kupokea maoni leo tarehe 22 Februari.
Katika maonesho hayo wadau hasa wachimbaji wadogo wamefurahi kuona STAMICO inatekeleza kwa vitendo dhana nzima ya kuwa mlezi wa wachimbaji wadogo kutokana na misaada wanayoipata mara wanapowasilisha matatizo yao.
Naye Bw. Jariq James mchimbaji kutoka Mirerani alikuwa na haya ya kusema “Hivi sasa STAMICO imekuwa ni rafiki wa wachimbaji wadogo tofauti na ilivyokuwa zamani inasuluhisha matatizo mengi ya wachimbaji wadogo. Ni wakati wa kuendeleza uhusiano huu mzuri ili kukuza sekta ya uchimbaji wadogo.”
Aidha Bw. Maneno J. kutoka Morogoro kwa niaba ya wachimbaji wadogo ameiomba STAMICO iongeze wigo kwa kuwaangalia wachimbaji wa madini katika mikoa yenye madini mengine nchini ukiachana na dhahabu.