Afisa Mawasiliano wa Shirika la Kimataifa Railway Children Africa Henry Mazunda akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiana na watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani namna wanavyoweza kushirikisha jamii kujua kundi hilo ,jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Ulinzi kwa Watoto wa Taasisi ya Baba Watoto Tony Mafiye akizungumza namna wanavyoweza kuwafatilia watoto mitaani kwa kujua mazingira yao,jijini Dar es Salaam.
Afisa Familia wa Taasisi ya Baba Watoto Efransia Kisweka akitoa maelezo wanavyounganisha familia pale mtoto anapotaka kurudi katika familia yake katika kituo cha kufikia Ilala jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watoto na Taasisi ya Baba Watoto wakiwa katika picha pamoja.
Mwanaid Salum akizungumza namna alivyounganishwa na mtoto wake aliyetoloka na Taasisi ya Baba Watoto .
Baadhi ya watoto wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Kituo Cha kufikia Watoto wanaoishi na kufanya kazi ,jijini Dar es Salaam.
……………………………………….
*Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanahitaji kuwezeshwa ili watimize ndoto zao.
Na Chalila Kibuda,Michuzi Tv
Shirika la Kimataifa la Railway Children Africa (RCA) limesema kuwa Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanakosa uangalizi na haki nyingi za msingi.
Shirika la RCA linafanya shughuli zake kwa kushirikiana na wadau wengine katika mikoa ya Arusha, Mbeya, Iringa, Mwanza ,Dodoma na Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanakosa huduma za afya kutokana na kutokuwa na uwezo wa kugharamia huduma hizo na pia kukosa watu wakuwawezesha.
Katika kipindi cha kwa milipuko ya magonjwa ikiwemo Corona watoto hawa huathirika zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Mawasiliano wa RCA, Henry Mazunda, amesema sehemu sahihi kuishi watoto ni nyumbani kwao pamoja na wazazi na ndugu zao lakini watoto wengi wanatoroka nyumbani na kwenda kuishi mtaani kutokana na changamoto mbalimbali hasa unyanyasaji na vitendo vya ukatili dhidi yao.
“Lakini mara nyingi, watoto wakiwa katika mazingira ya mtaani wanafanyiwa vitendo vya unyama zaidi kuliko wakiwa nyumbani kwawo”
Mazunda amesema katika mradi wa USAID- Kizazi Kipya ambao wanautekeleza katika mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Taasisi ya Babawatoto, wameanzisha vituo vya muda ambavyo vinatoa huduma mbalimbali kwa watoto hao zikiwemo chakula, sehemu ya kuoga na kufua nguo, sabuni, vifaa vya kujikinga dhidi ya magonjwa, elimu na ushauri wakitaalam.
Aidha amesema RCA pamoja na wadau wengine wanafanya kazi ya kusaidia kuwaunganisha watoto hao na familia au ndugu zao.
” Ila kwa watoto ambao hawataki kurudi nyumbani tunawawezeshwa kujiunga na vyuo mbalimbali kwa ajili ya kujifunza fani mbalimbali ili waweze kutimiza ndoto zao na kujitegemea baadaye.
Mratibu wa ulinzi wa watoto wa Taasisi ya Babawatoto, Tony Mafiye, amesema watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wakiwa katika kituo cha muda, yaani ‘Drop-in Centre’ wamekuwa ni watoto ambao wanajitambua kutokana na mifumo iliyopo katika usimamizi wa masuala ya watoto.
Amesema kuwa pia watoto hao wanapatiwa huduma za kisheria pale zinapohitajika.
Nae Afisa Mawasiliano na Utetezi wa watoto katika Taasisi ya Babawatoto, Brenda Mlwele, amesema kuwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wakiwa katika vituo vya muda wanajifunza vitu mbalimbali ikiwa ni kuwafanya wajisikie jamii inawajali.
Afisa Saikolojia Asha Salum amesema anapokutana na watoto anawasikiliza na kuongea nao kuangalia namna walivyoathirika kisaikolojia na kutoa ushauri wa kuwajenga upya.
Mwalimu wa Sanaa wa Babawatoto Adam Famba amesema kuwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanavipaji mbalimbali kama kuchora na kuimba.
Afisa wa Familia wa Babawatoto Efransia Kisweka amesema kuwa watoto wangine wamewaunganisha na familia zao ambapo wanaendelea vizuri na wengine wamewezeshwa kwenda katika Mafunzo ya ufundi.
Mmoja wa wazazi wa watoto waliowahi kutoroka nyumbani ameishukuru Taasisi ya Babawatoto kwa kumrudisha nyumbani mtoto wake pamoja na kumjenga kisaikolojia.
Amesema tatizo la mtoto wake lilitokana na familia kumnyanyasa kutokana na kwamba mtoto huyo alizaliwa nje ya ndoa.
Amesema mtoto huyo anaendelea vizuri na sasa ndugu wanaishi naye vizuri kama watoto wengine.
Katika tafiti iliyofanyika na Shirika ya RCA katika mikoa sita ya Tanzania bara, watoto zaidi ya 10,000 wanaishi na kufanya kazi mtaani.
.