……………………………………………………………………………..
Baada ya Mkoa wa Morogoro kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali huku ukishika nafasi ya nane mwaka jana katika matokeo ya darasa la saba kutoka nafasi ya 16 mwaka 2019, ambapo Mkoa huo sasa umekuja na mikakati zaidi ya kuongeza ufaulu Zaidi mwaka 2021
Mkoa huo unatarajia kuanzisha mtihani utakaojulikana kama “MTIHANI WA MKUU WA MKOA” unaolenga kuhamasisha ufaulu kwa kuwaandaa wanafunzi kufanya mitihani yao kwa ufanisi zaidi na watakaofanya vizuri kupewa zawadi ikiwa ni pamoja na kuwatengenezea mazingira mazuri wafikapo Chuo Kikuu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare Februari 20 mwaka huu alipotembelea Shule ya Sekondari ya Dakawa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo kutokana na fedha zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
‘’Nina mpango kama Mkuu wa Mkoa, kutafuta mtihani utakaoitwa MKUU WA MKOA, huo Mkuu wa Mkoa utakuwa unafanywa na madarasa yale ya mitihani ya form six, form four na form two na yataendana na zawadi na huu mtihani unafanywa ndani ya Mkoa na wale wa form six watakaopata division one we grantee them wapate mkopo waingie chuo kikuu tuhakikishe wanapata mkopo’’ amesema sanare
Aidha, Loata sanare amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kuwakwamisha kimasomo ili waweze kutimiza ndoto zao huku akiwasisitiza kufanya vizuri mitihani yao ili kuwa miongoni mwa shule 10 bora zitakazofanya vizuri katika mitihani ijayo.
Wakizungumzia changamoto zilizopo shuleni hapo, wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Octavina Steven ambaye pia ni Dada Mkuu wa shule hiyo ameiomba Serikali kuwajengea uzio kuzunguka shule hiyo hususan mabwenini ili kuwa na uhakika na ulinzi kwao na mali zao .
Naye Salah Justine wa kidato cha sita anayechukua mchepuo wa HKL amesema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitabu na kuomba wasaidiwe vitabu ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Akizungumza na wanafunzi hao Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Albinus Mgonya ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero amewasisitiza wanafunzi hao kutekeleza maagizo aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ikiwa ni pamoja na kutii maelekezo halali ya walimu wao na kuzingatia masomo.
Shule ya Sekondari ya Dakawa ilianzishwa mwaka mwaka 1992 ikiwa ni Shule mchanganyiko (wavulana na wasichna) mwaka 2006 Shule hiyo ilibadilishwa kuwa Shule ya wasichana ikiwa na michepuo ya HGK, HGL, HGE na HKL.
Shule hiyo hadi sasa ina wanafunzi 422 ambapo kidato cha tano ni wanafunzi 209 na kidato cha sita 213, ina walimu 31 na watumishi wasio walimu 3.