…………………………………………………………………….
Na Woinde Shizza , ARUSHA
Serikali imeendelea kuimarisha maisha ya wananchi wenye kipato cha chini, kupitia ruzuku ya fedha zinazotolewa kwa wananchi masikini, walio kwenye mpango wa Kunusu Kaya Masikini, mradi unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF awamu ya III.
Hayo yamethibitishwa na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini halmashauri ya Arusha, walipozungumza na mwandishi wetu, wakati wa zoezi la kupokea ruzuku za wanakaya katika kijiji cha Oloirien kata ya Oloirieni, zoezi lililofanyika kwenye ofisi ya kata ya Oloirieni.
Wanakaya hao wamesema kuwa, kabla ya kupokea fedha hizo za ruzuku kutoka TASAF, maisha yalikuwa magumu sana, huku baaadhi ya wanakaya kuthibitisha kushindwa kumudu kupata mahitaji ya muhimu ya familia kama malazi, chakula na mavazi na kuongeza kuwa fedha hizo zimewasaidia kumudu kupata mahitaji ya familia pamoja na kupata mahitaji ya shule kwa watoto, kwa kuanzisha miradi midogo ya kilimo na mifugo tafauti na hapa awali kabla ya neema ya mpango wa TASAF kuwashukia.
Leonia Nestori (64) mkazi wa kijiji cha Oloirieni na mnufaika wa mpango huo, amethibitisha kuwa fedha hizo za ruzuku ya TASAF zimemuwezesha kumudu kujikimu kimaisha, yeye na wajukuu zake ambao, amelazimika kuishi nao mara baada ya wazazi wao kufariki dunia na kubaki yatima.
“Mimi TASAF imenisaidia sana katika kuendesha maisha ya familia yangu, fedha ninazopokea zimenisaidia kununua mahitaji ya shule ya wajukuu zangu, ambao ni yatima, kabla ya TASAF wajukuu zangu wangeweza hata kuacha shule, nilishindwa hata kuwanunulia nguo, kalamu, daftari na mahitaji mengine ya shule, kwa kweli, tunamshukuru Rais wetu Magufuli, ametuokoa sisi masikini” ameweka wazi Leonia.
Aidha imeelezwa kuwa, kupitia fedha hizo za ruzuku, baadhi ya kaya masikini zimeweza kuanzisha miradi midogo midogo ya ujasiriamali, kilimo na ufugaji, miradi ambayo imewawezesha kupata fedha za kujikimu, kutokana na mazao wanayoyapata kutokana na mifugo na kilimo.
Loisojake Sangeti (74) mkazi wa Olosiva, amesema kuwa, kabla ya mradi huo wa TASAF, maisha yalikuwa magumu sana, lakini sasa TASAF imewezesha kaya nyingi kujikimu kimaisha kwa kutumia fedha hizo kununua kuku, mbuzi, kondoo na kuanza ufugaji, mifugo iliyowafanya kuwa na uhakika wa kupata chakula cha familia, pamoja na kununua mahitaji mengine muhimu kutokana na kuuza mifugo na mazao ya mifugo hiyo kama maziwa na mayai.
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule, amewataka wanakaya hao walioko kwenye mapango wa kunusuru Kaya masikini na wanaopokea ruzuku hiyo, kutumia fedha hizo vizuri kwa kuzingatia, lengo lililokusudiwa na serikali la kupambana na umasikini uliokithithiri sambamba na kuhakikisha kaya hizo zinaweza kujikimu kwa kupata mahitaji ya muhimu ya familia zao.
“Serikali inatoa pesa hizo kwa ajili ya ruzuku ya msingi ya kujikimu, ruzuku ya elimu kwa ajili watoto wanaosoma, kuwapatia mahitaji yao ya shule na kuhakikisha wanahudhuria shuleni bila kukosa, pamoja na ruzuku ya afya kwa watoto wa chini ya miaka mitano, kuhakikisha wanawapeleka kliniki na kupata huduma stahiki za afya ili kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano”. Amesisitiza Mkurugenzi Mtambule.
Mratibu wa TASAF, halamshauri ya Arusha, Grace Makema, amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 423.1 zinatarajiwa kugawiwa kwa kaya 8,223, kwenye vijiji 45 vilivyo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini, ikiwa ni ruzuku ya kipindi cha miezi miwili.
Awali jumla ya kaya 9,107 zilikuwa kwenye mpango wa kunusu kaya masikini Halmashauri ya Arusha, huku jumla ya wanakaya 79 kuondolewa kwa kufariki dunia, kaya 55 kuhama maeneo yao ya awali, kaya 4 kupoteza sifa kwa kuwa viongozi wa seriali, kaya 15 kujitoa kwenye mpango kwa hiari, kwa kuwa tayari zimejiweza na jumla ya kaya 541 hazikuhudhuria kwenye uhakiki awamu mbili zilizofanyika na kubakia kaya 8,223 ambazo zimepokea ruzuku awamu hii.