**********************************************
DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) limeingia mkataba wa miaka mitatu ya kuidhamini timu ya mpira wa miguu Ruvu Shooting kwa Muda wa miaka 3.
Akizungumza hayo wakati wa makubaliano hayo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa kuja kwa NIC katika timu hiyo kutaleta matokeo chanya katika kukuza vipaji na uwezo wa wachezaji wa ndani.
“Kiukweli NIC imejali maslahi mapana ya Taifa kwani kuwekeza kwetu sisi ni kuwekeza Kwenye vipaji vya Tanzania na kupata wachezaji wazuri wa timu yetu ya Taifa” alisema Meja Jenerali Mbuge.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ruvu Shooting Luteni Kanali Peter Elias Mnyali amesema kuwa pesa wanayopata kutoka kwa wadhamini wa ligi ambao ni Azam na Vodacom ilikua haitoshi kuendesha timu hivyo kuja kwa NIC kutasaidia Sana timu hiyo.
“Kiukweli ela tuliyokuwa tunaipata ilikua haikidhi mahitaji ya timu hivyo ujio wa wadhamini wetu wapya NIC naamini tutapiga hatua kutoka hapa tulipo na kuendelea mbele zaidi kihuduma hata kufanya vizuri katika mechi zetu zilizobaki na msimu unaokuja” alisema Luteni Kanali Peter.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Dkt. Elirehema Doriye amesema kuwa Udhamini huo umelenga maeneo matatu katika timu hiyo ikiwa ni Usafiri, Ada ya usajili na Mishahara ya wachezaji.
Aidha Dkt. Doriye amesema kuwa wameamua kuidhamini Ruvu Shooting kwa sababu ni timu yenye mvuto na itasaidia kukuza soka la Tanzania na Timu ya Taifa .
“Tumeamua kuidhamini Ruvu Shooting kwa sababu ni timu yenye mvuto na ni njia moja wapo ya kurudisha fadhila katika jamii ” alisema Dkt. Doriye.
Mbali na hayo Dkt. Doriye amesema kuwa Udhamini huo ni kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Jonh Pombe Magufuli katika kuinua sekta ya michezo nchini na kujenga timu ya Taifa imara kwa kuimarisha vilabu vya mpira nchini .