Home Mchanganyiko POLISI PWANI YAMKABIDHI MADAWATI RC NDIKILO

POLISI PWANI YAMKABIDHI MADAWATI RC NDIKILO

0

********************************************
Na MWAMVUA MWINYI,PWANI
JESHI la Polisi mkoani Pwani limetoa madawati (viti na meza) 50 vyenye thamani ya shilingi milioni nne ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati,Mkoani hapo.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa akikabidhi vifaa hivyo kwa mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameeleza wanaunga mkono jitihada za Rais Dk John Magufuli katika kuboresha na kupambana na changamoto kwenye sekta ya elimu.
Nyigesa alisema nao ni wazazi wanaona jinsi gani watoto wao wanavyotaabika kutokana na upungufu wa madawati.
“Sisi mbali ya kulinda wananchi na mali zao pia tunaisaidia jamii kwenye changamoto mbalimbali zinazowakabili kwani nasi tunamchango wa kuiwezesha jamii,” alisema Nyigesa.
Alieleza,wanakabidhi madawati hayo kwa mkuu wa mkoa ambaye naye atayapeka kwenye shule ambazo zina upungufu mkubwa wa madawati.
“Tunaomba tukukabidhi madawati haya ambayo ni michango yetu kwa lengo la kuisaidia jamii hususani kwenye sekta ya elimu ili kukabili changamoto hiyo ya upungufu wa madawati,” alisema Nyigesa.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alilipongeza jeshi hilo kwa kutoa msaada wa madawati hayo kwani yatasaidia kuboresha sekta ya elimu.
Ndikilo alisema itakuwa chachu kwa wanafunzi kuwa raia wema wanapoona polisi inatoa misaada mbalimbali kwa jamii,na amehimiza jamii kushirikiana na polisi kufichua wahalifu na kutoa taarifa za uhalifu.