*********************************
“DUNIA MPYA, REDIO MPYA”
Ninafuraha kuwasalimu wote katika tasnia ya utangazaji hususani ninaposhiriki kwa mara ya kwanza katika maadhimisho ya siku ya redio duniani. Ninafurahi kuungana na wadau wa utangazaji kwa njia ya redio katika maadhimisho haya ya siku ya redio duniani. Maadhimisho ya mwaka huu Februari 13, 2021 yanabebwa na kauli mbiu isemayo “Dunia Mpya, Redio Mpya”
Tanzania inaungana na dunia kuazimisha siku ya redio duniani, ambayo iliasisiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2011 na kutangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2013. Tunapoadhimisha siku hii tunaangazia mchango wa redio katika kuwafikia watu wengi, kutoa elimu, kuburudisha na kutoa mchango katika maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa.
Katika kipindi cha awamu ya tano, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuwafikia wananchi wengi kwa njia ya redio kwani vituo vya utangazaji kwa njia ya redio vimeongezeka kutoka vituo 106 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 193 Disemba 2020. Vilevile tumeshuhudia mabadiliko ya teknolojia ambapo kwa sasa kuna njia nyingi mbadala za kupokea matangazo kwa njia ya redio zikiwemo miundombinu iliyosimikwa ardhini, intaneti au satellite. Haya yamekuwa mageuzi makubwa ya utangazaji ukilinganisha na kule tunapotoka.
Kama nilivyosema awali, maadhimsho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ya “Dunia Mpya, Redio Mpya”, inayosisitiza matumizi ya teknolojia katika tasnia ya utangazaji kwa njia ya redio. Kauli mbiu hii pia inaangazia suala la mabadiliko katika namna ya utangazaji, ubunifu na kuunganisha jamii kupitia redio. Utangazaji kwa njia ya redio umekuwa na nguvu ya kipekee katika kuleta watu pamoja, kutangaza sera na mipango ya Serikali, kuhamasisha maendeleo ya jamii na pia kukemea uovu. Matumizi ya teknolojia yatawezesha uharaka na urahisi wa matangazo kufika umbali mrefu na kwa watu wengi.
Uhitaji wa Utangazaji kwa njia ya redio umeongezeka kwa kasi na kufanya masafa yanayotumika kurusha matangazo ya redio kuwa haba. Uhaba wa masafa ya redio umeonyesha wazi kuwa kuna haja pia ya kufikiria njia mbadala ya utangazaji wa redio kwa kuhama kutoka kwenye mfumo wa analojia kwenda dijitali. Ikumbukwe kuwa bado matangazo ya redio ya FM yako kwenye mfumo wa analojia ambao unachangamoto ya uhaba wa masafa ya kutangazia. Taasisi nyingi zisizo za kiserikali (NGO), za kidini na Halmashauri za Wilaya zimeona uwepo wa hitaji la kuwa na redio ili ziweze kufikia jamii kwa haraka na kuwashirikisha masuala ya maendeleo na kijamii au ya kiroho.
Kwa kuona ongezeko la uhitaji, maandalizi ya awali yameanza ili tuweze kuhama kutoka kwenye utangazaji wa analojia na kwenda kwenye mfumo wa dijitali. (Digital Sound Broadcasting) ni mfumo ambao utaondoa changamoto ya uhaba wa masafa ya kutangazia na kuweza kukidhi hitaji kwenye soko la utangazaji kwa njia ya redio. Pia utatoa fursa ya uanzishwaji wa vituo vipya vya redio hasa maeneo yenye uhaba wa masafa. Mfumo huu mpya utawezesha uzalishaji wa maudhui na kuleta ushindani kwenye soko ili kuwa na maudhui yanayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadae ambayo yatakuwa yanazalishwa ndani ya nchi ili kuakisi utamaduni na tunu zetu za taifa.
Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya Mwaka 2016 imetungwa katika mfumo unaotekeleza haki na wajibu wa vyombo vya habari. Vyombo vya habari viko huru katika kutafuta, kuhariri na kuchapisha au kutangaza habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa haki yao ya kikatiba (ibara ya 18, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977) lakini pia ikiwa ni kutekeleza haki za kimataifa za uhuru wa habari (kwa mujibu wa Tamko la Haki za Binadamu, 1948, Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Kisiasa na Kiraia, 1966 na Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu na Watu, 1981). Lakini Sheria pia imetungwa katika muktadha wa kutambua kuwa haki hizo pia zinaendana na wajibu ambao vyombo vya habari vinapaswa kuubeba.
Kifungu cha 19 cha Mkataba wa Kimataifa wa 1966 kinaanisha ukomo wa uhuru wa habari ikiwemo wanahabari kutotakiwa kuandika habari za kashfa, kuhatarisha usalama wa nchi,amani ya nchi, afya ya jamii na maadili ya Taifa. Aidha mikataba ya kimataifa pia inataka vyombo vya habari kulinda haki ya usiri na utu. Katika kutekeleza hili Sheria hii imeweka makosa mbalimbali na adhabu kwa wanahabari si kwa nia ovu ya kuzuia haki za binadamu za wanahabari bali kutekeleza matakwa haya ya sheria za kimataifa ambazo zinawapa wanahabari wajibu wa kulinda haki nyingine za raia na usalama wa nchi.
Sheria pia katika kifungu cha 67 ilitoa kipindi cha mpito cha muda wa miaka mitano, ili wale wasio na sifa ya kuanzaia ngazi ya Diploma waweze kujiendeleza. Kipindi hicho cha mpito kinamalizika Disemba, 2021. Nawasihi wanahabari wote tuendelee kujiendeleza kitaaluma na kufikia kigezo hicho ili pindi utekelezaji wa sheria ukianza kusiwe na usumbufu wowote.
Kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kuwahamasisha watanzania kuchangamkia fursa ya matumizi ya teknolojia katika kuwekeza kwenye sekta ya utangazaji hasa kuanzisha vituo vipya vya redio, kubuni maudhui mapya yanayoendana na soko la Tanzania na kimataifa, kutumia vituo hivi kukuza mahusiano ya kibiashara na kijamii na kupanua soko la ajira kwa vijana.
Mwisho nitoe rai kwa redio zote zilizosajiliwa nchini kufuata maadili ya utangazaji, kufuata sheria na kuhamasisha umoja wa kitaifa. Tutumie teknolojia katika kuboresha, kukuza na kusaidia tasnia ya utangazaji kwa njia ya redio kuwa chombo cha amani, umoja na mshikamano.