Home Mchanganyiko TAKUKURU MANYARA YAMSHIKILIA MWENYEKITI MSTAAFU NARAKAUO

TAKUKURU MANYARA YAMSHIKILIA MWENYEKITI MSTAAFU NARAKAUO

0
**********************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU inamshikilia Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Narakauo Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Saruni Sanjiro Kimanjoi, kwa kukutwa na nyaraka za Serikali zinazomuwezesha kuendelea kugawa ardhi kama bado yupo madarakani.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Manyara, Ally Sadiki Hajji, Mwenyekiti huyo mstaafu amekamatwa kwenye operesheni inayoendelea ya TAKUKURU Manyara ya kupunguza migogoro ya ardhi vijijini.
Hajji amesema pia TAKUKURU inamshikilia aliyekuwa ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Saning’o Lokonyo wakati wa kipindi cha uongozi wa Mwenyekiti huyo mstaafu, kwa uchunguzi zaidi juu ya tuhuma hizo.
“Nyaraka zilizokamatwa kwa Sanjiro ni hati 13 za mashamba zinazoonyesha familia yake imegawiwa ekari 520,” amesema Hajji.
Amesema nyaraka nyingine zilizokutwa kwa Mwenyekiti huyo mstaafu ni mihutasari tisa ya mkutano mkuu wa kijiji, muhuri wa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Namelock na wino wa muhuri huo.
“Huu ni mwendelezo wa TAKUKURU Simanjiro kushughulikia uuzwaji wa ardhi za vijiji kinyume cha sheria ya ardhi ya vijiji namba 5/1999 kunakofanywa na wenyeviti wastaafu,” amesema.
Amesema kabla ya operesheni ya Narakauo TAKUKURU ilimkamata Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kimotorok Merubo Parmelo na Daniel Melau kwa makosa kama hayo ya kughushi nyaraka za Serikali na kuendelea kugawa ardhi kama bado wapo madarakani.
“Operesheni hii ni ya kudumu Hadi hapo tutakapojiridhisha kwamba wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria,” amesema Hajji.
Ametoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Simanjiro na Kiteto waendelee kutoa taarifa ya wenyeviti wastaafu wanaoendelea kuwa na nyaraka za Serikali na kuuza ardhi kinyume cha sheria ili hatua zichukuliwe dhidi yao.