Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wafugaji katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro na kuwataka wafugaji wafuge kisasa na kuwahakikishia kuwa wizara itaendelea kusimamia maslahi ya wafugaji nchini.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akisalimiana na baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimaasai mara baada ya kuzungumza nao alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kilimanjarao.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na uongozi wa Wilaya ya Siha, na baadhi ya kinamama wa jamii ya kimaasai mara baada ya kuzungumza na baadhi ya wafugaji wa jamii hiyo, alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kilimanjarao.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akifafanua jambo kwa Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro Bw. Raymond Lutege (wa kwanza kulia) mara baada ya Waziri Ndaki kufika katika ranchi hiyo siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro na kutaka ranchi zote za taifa kutumia teknolojia ya kisasa katika kudhibiti wizi wa mifugo katika ranchi hizo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akipatiwa maelezo ya mbegu bora za mbuzi na Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Dkt. Athuman Nguluma, mara baada ya Waziri Ndaki kutembelea kituo cha taasisi hiyo kilichopo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kuitaka TALIRI ihakikishe matokeo ya tafiti zake yanakuwa na tija kwa wafugaji.
Muonekano wa duka la kuuzia nyama linalomilikiwa na Ranchi ya West Kilimanjaro iliyo chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), ambalo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Siha kufanya uchunguzi wa utendaji kazi wa duka hilo baada ya kutoridhishwa na namna linavyoendeshwa tangu kuanzishwa kwake. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
……………………………………………………………………………….
Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema atazungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii kuhusu kitendo cha baadhi ya watumishi wa umma walio chini ya wizara hiyo, ambao wamekuwa wakiielekeza mifugo kwa makusudi kuingia kwenye hifadhi za taifa ili waikamate na kuwaonea wafugaji kwa kuwalipisha tozo pamoja na kutaifisha mifugo hiyo.
Waziri Ndaki amezungumza hayo jana (09.02.2021) wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro, kwa kuzungumza na baadhi ya wafugaji katika Wilaya ya Siha mkoani humo mara baada ya kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na Ranchi ya West Kilimanjaro zilizopo katika wilaya hiyo ili kujionea namna wanavyotekeleza majukumu yao.
Amesema kitendo hicho cha kifisadi hakiwezi kuvumilika na kwamba watuhumiwa wote watatafutwa na kukamatwa ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.
“Ninajua kuna wakati tunaonewa unakuta ng’ombe wako pembeni ya hifadhi wanapelekwa kwa lazima ndani ya hifadhi, nimesema nazungumza na mwenzangu wa maliasili na utalii na kumwambia huo mtindo hapana, tuwasake watu wako kwa sababu wenye tabia hiyo siyo wafugaji ni watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, hao tunaanza kuwasaka mmoja mmoja maeneo yote wanayokaa karibu na wafugaji tutawabaini na wanachokifanya ni kitendo cha kiharamu na ufisadi kwa sababu una bunduki unamtisha mfugaji halafu unawapeleka kwa lazima ng’ombe kwenye hifadhi hiyo na kusema umewakamata ng’ombe kwenye hifadhi hatutaelewana.” Amesema Mhe. Ndaki
Ameongeza kuwa kitendo hicho lazima kikemewe kwa kuwa kinarudisha nyuma uwekezaji katika Sekta ya Mifugo na kutaka watumishi wa umma pamoja na wafugaji kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi na kwamba lazima kukomesha hatua hiyo kwa sababu inasababisha migogoro kati ya wafugaji na hifadhi za taifa na kwamba kuna wakati wafugaji wanaelewa maeneo ya hifadhi, lakini wakipeleka mifugo karibu na maeneo hayo wananyanyaswa na mifugo yao kulazimishwa kuingia ndani ya hifadhi ili ionekane wameingiza mifugo ndani ya hifadhi.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufikia Jumatano ijayo, iwe imeandaa taarifa ya mifugo iliyopo kwenye ranchi zote hapa nchini, zikiwemo za kiwango cha mifugo inayozaliwa, kufa na aina ya mifugo iliyopo ili kuona kinachoendelea katika ranchi hizo.
Amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kuhakikisha anasimamia zoezi hilo ili taarifa hizo aweze kuzipata siku hiyo ya Jumatano, ikiwa ni lengo la kuhakikisha mifugo ya serikali inakuwa na tija kwa taifa.
“Tunataka rasilimali ya mifugo inufaishe taifa na wananchi hawa hatuwezi kuwa na rasilimali ambayo hatujui iko kiasi gani.” Amefafanua Mhe, Ndaki.
Pia ameitaka NARCO kuhakikisha inatumia teknolojia ya kisasa ya kuwawekea mifugo iliyopo kwenye ranchi zake ili kudhibiti vitendo vya wizi wa mifugo ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika ranchi zake na kuisababishia hasara za mara kwa mara.
Kuhusu uwekezaji wa NARCO katika duka la kuuzia nyama lililopo Kata ya Sanya Juu Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kufanya uchunguzi juu ya utendaji wa duka hilo baada ya kutoridhishwa na taarifa zilizorekodiwa tangu kuanza kwake kazi ya uuzaji nyama.
Waziri Ndaki ameongeza kuwa kumekuwa na taarifa za mauzo kidogo ya nyama ambayo hayalingani na uhitaji wa nyama eneo husika, huku akitaka mmoja wa mawakala ambaye aliwahi kuwa na utaratibu wa kununua nyama katika Ranchi ya West Kilimanjaro kwa bei ya jumla na kwenda kuuza kwenye duka lake kuchunguzwa na kuitaka kamati hiyo kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kuhujumu utendaji kazi wa duka.
Kwa upande wao baadhi ya wafugaji waliohudhuria mkutano huo wamelalamikia uvamizi wa wanyamapori ambao wamekuwa wakiingia katika maeneo yao na kuharibu mazao na malisho ya mifugo hali ambayo imekuwa ikiwarudisha nyuma katika utendaji wao wa kazi.
Wameongeza kuwa kitendo hicho kimeathiri kwa kiasi kikubwa malisho ya mifugo na kuiomba serikali kuangalia hatua ambazo inaweza kuchukua ili kudhibiti kitendo hicho ambacho kimekuwa kikiwarudisha nyuma mara kwa mara pamoja na kufanya mikakati mbalimbali ya kuhakikisha dawa na chanjo za mifugo zinawafikia ili kudhibiti magonjwa ya mifugo ambayo yamekuwa yakiathiri kwa kiasi kikubwa mifugo yao.
Awali kabla ya kikao hicho na baadhi ya Wafugaji wa Wilaya ya Siha, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa katika Ranchi ya West Kilimanjaro inayosimamiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kujionea utendaji kazi wa ranchi hiyo pamoja na kupokea taarifa ya namna ranchi hiyo inafanya kazi kutoka kwa meneja wa ranchi hiyo Bw. Raymond Lutege ambaye amemuambia Waziri Ndaki kuwa ranchi hiyo iko katika hatua mbalimbali za kuhakikisha mbegu bora za mifugo wakiwemo ng’ombe na kondoo zinapatikana ili wafugaji waweze kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo bora.
Waziri Ndaki akiwa katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kituo cha Wilaya ya Siha, mara baada ya kusomewa taarifa ya kituo na Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini Dkt. Athuman Nguluma, waziri huyo ameitaka TALIRI kuhakikisha tafiti inazofanya ziwe na tija kwa wafugaji na taifa kwa ujumla ili tasnia ya ufugaji iweze kubadilika na kuwa ya kisasa zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu amesema anaimani kubwa na utendaji kazi wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kwa namna alivyoanza kusimamia sekta za mifugo na uvuvi na kuonesha nia thabiti ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta hizo.
Ameongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha wafugaji wananufaika kwa kiasi kikubwa pamoja na kuondoa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.