WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeziagiza balozi zote za Tanzania zilizopo katika mataifa mbalimbali zianzishe vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili kwa wageni ili itumike kujenga diplomasia ya uchumi na Watanzania waweze kuajiriwa katika nchi hizo.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 11, 2021) wakati akijibu swali la mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha lugha ya Kiswahili kinakuwa bidhaa ya kukuza diplomasia ya uchumi na kuwa fursa ya ajira kwa watanzania.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa lugha ya Kiswahili imepata nafasi kubwa ya kuzungumzwa kwenye mataifa mbalimbali duniani na pia tayari nchi hizo zimeanza kuandaa vipindi vya radio kwa Kiswahili ni ishara kwamba lugha hiyo inakuwa duniani kote.
”Kiswahili hapa nchini kinazungumzwa kwenye makabila yetu karibu yote na ndio lugha ambayo inatuunganisha Watanzania na tumeanza kukisambaza Kiswahili hiki kwenye ukanda wetu wa Afrika ya Mashariki na wote tumeshuhudia jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kusambaza Kiswahili katika ukanda wa SADC.”
Amesema Rais Dkt. Magufuli amekuwa kinara wa kukuza lugha ya Kiswahili alipoanza kukitumia katika mikutano ya nchi za Jumuiya za Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC) hivyo Serikali imeanza kunufaika kwa kupata fedha zitokanazo na kodi kwa wanaokwenda kufundisha huko.
Waziri Mkuu amesema kuwa lugha ya Kiswahili imekuwa nguzo ya kujivunia kwa kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake kwa sababu nchini kama Ujerumani, Marekani na hata Uingereza na mataifa mengine makubwa yanaendelea kutumia lugha hiyo. Serikali itaendeleza juhudi za kukikuza ili kisambae zaidi duniani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji ipo mbioni kukamilisha sera itakayowezesha kuwepo kwa kiwango kimoja cha gharama za uunganishaji maji nchini kote ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei aliyesema kwamba Serikali imefanya vizuri kwenye Miradi ya Umeme Vijijini (REA) ambako wananchi wanaunganishwa kwa gharama nafuu, lakini kwenye maji hali ni tofauti kila eneo wanatoza gharama zao, je Serikali haiwezi kuwa na gharama moja?.
Dkt. Kimei alisema kwa sasa baadhi ya mamlaka za maji zinatoza kuanzia shilingi 350,000 hadi 600,000 kulipia gharama za kuunganishiwa maji ambazo ni kubwa na zimesababisha baadhi ya wananchi kunywa maji ya miferejini, hivyo alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusiana na suala hilo.
Waziri Mkuu amesema anatambua uwepo wa malalamiko ya gharama kubwa za maji na kwamba Wizara ya Maji inaendelea kuangalia uwezekano wa kuwa kiwango kimoja cha malipo sawa ya kuunganishiwa huduma ya maji katika maeneo yote na ikikamilisha wizara hiyo itatoa taarifa.