Home Siasa CCM SIMANJIRO YATANGAZA NAFASI WAZI

CCM SIMANJIRO YATANGAZA NAFASI WAZI

0
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kimewataka wanachama wake kujitokeza kuchukua fomu za kujaza nafasi zilizo wazi ikiwemo Katibu mwenezi wa Wilaya na Mwenyekiti wa UWT wa Wilaya.
Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Ally Kidunda amesema nafasi tano ngazi ya wilaya zipo wazi na zinatarajiwa kujazwa na wanachama wenye sifa na nafasi mbalimbali  za kata na matawi.
Kidunda ametaja nafasi za wilaya ni katibu wa siasa na uelezi wa wilaya, Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa wanawake (UWT) wa wilaya na nafasi moja ya mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya.
Ametaja nafasi nyingine ni wajumbe wawili wa halmashauri kuu ya CCM mkoa na nafasi moja ya mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM kupitia jumuiya ya wazazi wilaya.
Amesema shughuli za kujaza nafasi zilizo wazi utagusa nafasi zilizo wazi ngazi ya matawi na kata kwa chama na jumuiya zake.
“Nawaagiza viongozi husika wa ngazi ya kata ya chama na jumuiya kutangaza nafasi zote zilizo wazi zibandikwe katika mbao za matangazo na maeneo mbalimbali ya wazi,” amesema Kidunda.
Amesema ratiba ya uchukuaji na urejejeshwaji fomu itakuwa kuanzia Februari 10 hadi 13 mwaka huu kisha mchakato mwingine utaendelea.
Amesema mapendekezo ya vikao vilivyowajadili wagombea wote yatapelekwa makao makuu ya wilaya na taarifa za fomu, mihutasari na mapendekezo zinapaswa kufika Februari 20.