Na.Sophia Kingimali.
Mwananchi na mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, Dk David Msuya, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia lugha ya staha na busara wanapozungumza na wananchi ili kulinda amani ya Tanzania na kuondoa migawanyiko inayoweza kujitokeza kutokana na matamshi ya kisiasa.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari,leo Mei 22,2026 Dk Msuya amesema licha ya siasa nchini kwenda vizuri kwa ujumla, bado zipo changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi, hususan matumizi ya maneno yenye kuibua taharuki na chuki miongoni mwa wananchi.
Amesema baadhi ya kauli kutoka kwa viongozi wa kisiasa zimekuwa zikiumiza mioyo ya Watanzania badala ya kuleta maridhiano na mshikamano wa kitaifa.
Ameeleza kuwa Tanzania ni nchi ya Watanzania wote, hivyo hakuna sababu ya kutumia siasa kuleta migawanyiko wakati wananchi wanahitaji kuona maendeleo ya haraka katika sekta mbalimbali ikiwemo barabara, afya, elimu na uwekezaji. Alisisitiza kuwa wananchi wanataka kuona miradi ikikamilika kwa wakati na fedha za maendeleo zikitumika kwa uadilifu.
Dk Msuya alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuendelea kuiombea nchi amani pamoja na kuwashauri viongozi wa kisiasa kuzungumza kwa hekima wanapokutana na wananchi katika mikutano yao ya kisiasa. Aliongeza kuwa maneno ya hasira na mihemko yanaweza kuchochea vurugu na kuathiri mshikamano wa taifa.
Aidha, alisema wawekezaji hawawezi kuwekeza katika mazingira yenye migogoro na vurugu, hivyo Watanzania wanapaswa kuhubiri amani ili kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira kwa vijana. Alitolea mfano wa miradi na viwanda vinavyoendelea kujengwa nchini kuwa ni miongoni mwa maendeleo ambayo wananchi wanapaswa kuyapa kipaumbele.
Katika hatua nyingine, Dk Msuya aliitaka serikali kuendelea kusikiliza maoni ya wananchi na kuchukua hatua pale panapobidi marekebisho kufanyika, akisisitiza kuwa kukosolewa si jambo baya bali ni njia ya kujirekebisha na kuboresha utendaji kwa maslahi ya taifa.
Pia alikumbusha kuwa misingi ya amani, upendo na mshikamano iliyowekwa na Julius Nyerere inapaswa kuendelea kuheshimiwa, huku Watanzania wakitakiwa kutanguliza utaifa badala ya ukabila, dini au tofauti za kisiasa.
Dk Msuya amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kuombeana na kushirikiana katika kujenga taifa lenye umoja, maendeleo na ustawi, huku viongozi wa kisiasa wakiepuka kauli zinazoweza kuchochea taharuki na badala yake kuhubiri amani na matumaini kwa wananchi.
