Baadhi ya wadau sekta maalum kutoka kundi lenye uhitaji wakisikilza mafunzo hayo.
…………………………………………………………………………..
NA DENIS MLOWE,IRINGA
Lengo haswa la mkutano huo ni kutoa uelewa kwa watu wenye mahitaji maalum, kuhusu zoezi la usajili wa laini za simu kwa njia ya mfumo wa alama za vidole ,pia kuangalia changamoto mbalimbali walizonazo katika huduma za Mawasiliano ikiwa ni kuwapa taarifa ya maendeleo ya sekta, haki na wajibu wao kama watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano.
Akizungunza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Kanda Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Nyanda za Juu Kusini Mhandisi Asajile John Mwakisisile alisema kuwa semina hii imekuwa na mafanikio makubwa na walemavu wengi wamepewa taarifa kuhusu kazi za TCRA na wajibu wao kama watumiaji wa mawasiliano katika jamii na wanamini changamoto zingine kama za makosa ya kimtandao yakiwemo pesa mtandaoni, usajili wa laini na yanayofanana na hayo sasa yatakuwa yamepata ufumbuzi.
Mhandisi Mwakisisile alsema kuwa katika mafunzo hayo wamefanikiwa kuwapa maelekezo juu ya utaratibu wa namna ya kuwasilisha malalamiko yao na kufanyiwa kazi na mamlaka ya mawasiliano, na yale yenye malengo ya kijinai yatafanyiwa kazi na Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imelenga kuwafikia watu wa pembezoni pamoja na makundi yenye mahitaji hasa walemavu wa aina zote kwa lengo kuwapa elimu juu ya sekta ya mawasiliano kwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo wengi wao walikuwa hawajui mahala pa kuzipeleka.
”Ila mamlaka ya mawasiliano tunajitahidi kuona ni kwa namna gani tunaweza kuwasaidia ,kwa wenzetu wasioona tunawapa taarifa mbalimbali kupitia vitabu ambavyo vimechapishwa kwa zile alama zao maalum.”
Aidha amewataka watumiaji wa mawasiliano kuona umuhimu wa kujisajili ni kwani watakaposajili kutumia alama za vidole taarifa zao zinafahamika ,sambamba na kuimarisha usalama wanapotumia mawasiliano.
Alisema kuwa moja mafunzo waliyopatiwa makundi hayo ni namna ya kutambua simu halisi au bandia kwa kubonyeza *#06#, ltatokea namba ya tarakimu 15. Kama simu ina laini zaidi ya moja zitatokea namba nyingi, iandike namba hiyo mahali, kisha Itume kama meseji kwenda 15090 baada ya hapo ujumbe utakaokuja utakuambia aina ya simu.
Aidha alisema kuwa mafunzo mengine ni juu ya kuchukua hatua unapoibiwa simu ni pamoja na kuripoti kituo cha polisi haraka, kule utapewa RB namba ni hitaji la kisheria na kuwa na namba ya tambulishi ya simu yako ambayo ni IMEI.
Alisema kuwa Jeshi Ia Polisi kupitia Kitengo cha Uhalifu Mtandaoni watafuatilia shauri hilo. Unaweza pia kuifungia simu hiyo ili isiweze kufanya kazi huko ilipo. Simu ikipatikana unaweza kufuata taratibu za kuifungua.
TCRA imeweka msisitizo mkubwa kuhakikisha huduma za mawasiliano zilizo bora, salama na za gharama wananchi wanazozimudu na zinapatikana kila sehemu kwa makundi yote katika jamii. Mtumiaji una wajibu wa kuwa makini na kutobughudhi watumiaji wengine.
Kwa upande wake mwakilishi wa mgeni rasmi ambaye ni Afisa tawala msaidizi anayesimamia masuala ya elimu,vijana utamaduni na michezo mkoa wa Iringa, Jermana Munga’ho alitoa somo kwa makundi hayo kuwa kuna makosa ya uhalifu wa kimtandao ,watu wasiowaaminifu wanaotuma jumbe za kulaghai wa wananchi, hivyo wanatakiwa kuwa makini katika matumizi ya simu.
Alisema kuwa kutokana na changamoto kama hizo ndio sababu hiyo serikali imeelekeza laini zote za simu zisajiliwe kwa alama za vidole ,hivyo ameipongeza TCRA kwa kuona watu wenye ulemavu kuwa ni sehemu ya jamii ambayo inahitaji elimu kubwa kuhusu suala la changamoto za kwenye mawasiliano.
“Watu hawa wenye mahitaji maalumu wanaachwa mara nyingine kutokana na baadhi ya watu kudhania kwa mawazo yao hasi kwamba ulemavu ni hasara,niseme hujafa huijaumbika,nisisitize hebu tubebane tonane tupo sawa”alisema
Munga’ho alisema kuwa ni muhimu kusajili line za simu ili kuepusha makosa ya uhalifu wa kimtandao, matapeli wanao tuma jumbe na kutoa wito kwa jamii kulitilia uzito swala hili la kusajili laini,na kwa wale ambao hawajapata kitambulisho cha NIDA,Mamlaka husika itawasaidia kupata namba zao,sambamba na wale ambao hawajajiandikisha NIDA wapo tayari kwaajili ya kuwasaidi ili wajiandikishe wapate kitambuluisho cha taifa.
Naye mwenyekiti wa chama cha walemavu wilaya ya Iringa Mjini Haruna Mbilinyi aliishukuru TCRA kwa kuwathamini na kuwapatia mafunzo hayo ya kuwajengea utaalamu katika sekta ya mawasiliano
Alisema moja ya changamoto kubwa katika mawasiliano watu wasioona ni mtu wa kuwasomea ujumbe lazima awepo,hakuna usiri,tunaomba serikali itusaidie uwepo wa simu ,ambazo tunaweza kusoma ujumbe kwa kusikia sauti ,na iwe katika lugha ya kiswahili ambapo itaweza kuondoa utegemezi kwa kiwango kikubwa.
“Changamoto kubwa mtu anakutumia ujumbe hata kama unataka uwe wa siri,inashindikana mpaka utafute mtu mwaninifu aweze kukusomea ujumbe wako,hiyo ndiyo changamoto inayotupata sisi watu wasioona.’
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Nyanda za Juu Kusini inasimamia mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe Iringa na Ruvuma.