………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Konde kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Hatibu Said Haji amempongeza Rais Dk.John Magufuli kwa kulinda Katiba yetu na pia ni Mlinzi wa Demokrasia kwa kukataa kuongeza muda wa Urais.
Pia amesema kuwa Rais nimsikivu sana nashangaa wabunge wa Chama cha Mapinduzi CCM ambao wamekuwa wakishinikiza Rais Dk John Magufuli kuongezewa muda wa Urais.
Kauli hiyo ya Mbunge Hatibu imekuja siku chache tangu Mbunge wa Jimbo la Makambako kupitia CCM, Deo Sanga kuomba Rais kuongezewa muda wake wa uongozi lakini kauli hiyo pia imewahi kutolewa na aliyekuwa Mbunge wa Nkasi CCM, Ally Kessy pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Chemba CCM, Juma Nkamia.
Akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa miaka mitano 2021/22- 2025/26.
Hatibu amempongeza Rais Magufuli kwa kitendo chake cha kumtuma Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kusema kwamba hatoongeza hata dakika moja mara ambapo muda wake wa urais utakapokua umeisha mwaka 2025.
” Nimpongeze sana Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kukataa maoni ya baadhi ya Wabunge wa CCM ya kumtaka kuongeza muda wake wa Urais, kitendo chake cha kusema hatoongeza muda ni kuonesha jinsi gani anaiheshimu Katiba yetu na ni mlinzi wa Demokrasia.
Kitendo chake cha kukataa kuongeza muda kinamfanya aweke rekodi ya kuwa Rais wa kwanza Afrika kuombwa kuongeza muda wa urais na wabunge wa Chama chake na akakataa, muacheni Rais msiseme ooh tutamlazimisha yeye kashasema hatoongeza,” Amesema Hatibu.
Mbunge huyo wa upinzani pia amempongeza Rais Magufuli kwa namna ambavyo ameonesha uwezo mkubwa wa kuthibiti nidhamu kwa watumishi wa umma jambo ambalo limefanya wananchi hata wa hali ya chini kupata huduma hila kubughudhiwa tofauti na miaka ya nyuma.
” Ni lazima tumsifu Rais Magufuli kwa uthubutu wake wa kusimamia nidhamu serikali, leo hii kila mmoja anapata huduma kwa usawa na haki, amedhibiti matumizi mabaya ya madaraka hili ni jambo la kupongezwa sana,” Amesema Hatibu.