Home Mchanganyiko MUSUKUMA AMUOMBA RAIS MAGUFULI KUKUTANA NA WAFANYABIASHARA NCHINI

MUSUKUMA AMUOMBA RAIS MAGUFULI KUKUTANA NA WAFANYABIASHARA NCHINI

0

……………………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Musukuma amemuomba Rais Dk John Magufuli kukutana na wafanyabiashara nchini kama alivyofanya kwa wadau wa madini  ili kutafuta suluhu la changamoto zao za kibiashara.

Ombi hilo ametoa leo Februari 8,2021 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango ya Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo ya Taifa pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa miaka mitano 2021/22-2025/26.

Mhe. Msukuma amesema kuwa ukweli usio na shaka kwamba wananchi wamekuwa wakilalamikia ugumu wa maisha huku wafanyabiashara wakifunga maduka na biashara zao yote hayo akisema yanachangiwa na sheria za kodi ambazo sio rafiki.

” Nimuombe Rais Magufuli kama alivyokaa na sisi wadau wa Madini basi tunamuomba akae na wafanyabiashara wamueleze changamoto zao naamini baada ya hapo watakua wamepiga hatua kubwa sana ya kujua namna gani ya kuinua uchumi wetu.

Hawa vijana wanaomaliza vyuo vikuu wanalalamika hakuna fedha na ajira mitaani , kama tumeweza kuwakopesha elimu kwa kuwapa mikopo ya Chuo kwanini tusiweke mazingira mazuri ya Mabenki yetu kuwakopesha vijana hawa na dhamana yao iwe vyeti vyao? Hiyo itachangia sana kumaliza changamoto ya ajira nchini,” Amesema Musukuma.

Ameishauri Serikali kuacha kutumia fedha nyingi katika miradi ambayo haina manufaa yoyote kwa wananchi na badala yake imekua ikiitia serikali hasara akitolea mfano ujenzi wa Masoko kama Soko la Ndugai jijini Dodoma, Soko la Morogoro na Machinga Complex jijini Dar es Salaam.

” Hatuwezi kupambana kujenga uchumi wa Nchi yetu huku tukiangaika na miradi ambayo haiiletei faida Nchi yetu, masoko kama Soko la Ndugai, Machinga Complex ni hasara kubwa licha ya kutumia mabilioni mengi kuyajenga, ukienda pale hakuna watu niombe serikali iache kufanya miradi ya namna hii,” Amesema Mhe. Musukuma.