Home Mchanganyiko HOTUBA YA MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB.),WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO...

HOTUBA YA MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB.),WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA  MITANO 2021/22 – 2025/26  

0

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/22, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakichukua hoja wakati wa mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/22 yalitowasilishwa bungeni jijini Dodoma na Mhe. Nchemba kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango.

***************************************

DODOMA

8 FEBRUARI,2021

 • UTANGULIZI

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha leo hii kukutana kwa ajili ya kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. Aidha, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kulijalia Taifa letu amani, utulivu, umoja na mshikamano na kutuwezesha kukamilisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 kwa amani na utulivu.

 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kutumia fursa hii kutoa pole kwako wewe Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wote, ndugu, jamaa na marafiki kwa kifo cha Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM). Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake kwa amani.

 1. Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa tena kwa ushindi wa kishindo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha miaka mitano. Vile vile, ninampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassimu M. Majaliwa na Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kuteuliwa kushika nafasi muhimu katika uongozi wa nchi yetu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe pia kwa kuchaguliwa kwa ushindi wa kishindo wa asilimia 99.7 kuwa Spika wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii inaashiria kuwa Waheshimiwa Wabunge wana imani kubwa na utendaji wako katika kuliongoza Bunge hili Tukufu. Aidha, napenda pia kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, nichukue nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini (CCM) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi (CCM), kwa mwongozo wao na maoni waliyotupatia kuboresha Mapendekezo ya Mpango huu. Ushauri wao umezingatiwa kikamilifu katika taarifa ya Mpango ninayowasilisha Bungeni leo.

 1. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 yamezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025; Hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, wakati akizindua Bunge la 11 na 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba, 2015 na 2020 mtawalia; Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/12 – 2025/26; Matokeo ya Tathmini Huru ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21; Sera na Mikakati mbalimbali ya Kisekta; matokeo ya tafiti zilizofanywa na vyuo na taasisi mbalimbali nchini; Dira ya Afrika Mashariki 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika 2050; Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; na Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Mpango huu utakuwa na maeneo makuu matano (5) ya kipaumbele ambayo ni: (i) kuchochea uchumi shindani na shirikishi; (ii) kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; (iii) kukuza biashara; (iv) kuchochea maendeleo ya watu; na (v) kuendeleza rasilimali watu. Aidha, jumla ya shilingi trilioni 114.8 zitahitaji kugharamia miradi na programu zitakazotekelezwa katika Mpango huu kwa kipindi cha muda wa miaka mitano. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 74.2 ni mchango wa sekta ya umma na shilingi trilioni 40.6 ni mchango wa sekta binafsi. 

 

 • TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA PILI WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2016/17 – 2020/21

 

 • Viashiria vya Uchumi Jumla

 

 1. Mheshimiwa Spika, Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 iliyofanywa na Mtathimini Huru (Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii – ESRF) inaonesha kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa Mpango (2016/17 – 2019/20): Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9; mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 4.1 kwa mwaka ikiwa ni ndani ya lengo la kutozidi asilimia 5; akiba ya fedha za kigeni ilitosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.9 ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne (4) ; na nakisi ya bajeti ilikuwa ndani ya lengo la kutozidi asilimia 3 kwa kipindi chote. Katika kipindi hicho, deni la Serikali lilikuwa himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu. Vile vile, Pato la Wastani la Kila Mtu liliongezeka kutoka shilingi 2,225,099 (sawa na dola za Marekani 1,022) mwaka 2016 hadi shilingi 2,577,967 (sawa na dola za Marekani 1,080) mwaka 2019. Kielelezo kikuu cha mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ni Tanzania kufanikiwa kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati cha chini mwezi Julai 2020.

 

 1. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ulikadiriwa kutumia jumla ya shilingi trilioni 107 ambapo shilingi trilioni 59 ni kutoka sekta ya umma na shilingi trilioni 48 kutoka Sekta Binafsi. Katika miaka minne ya utekelezaji wa mpango huo, sekta ya umma imetumia jumla ya shilingi trilioni 34.9, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la miaka minne la shilingi trilioni 45. Aidha, sekta binafsi imetumia jumla ya shilingi trilioni 32.6 sawa na asilimia 85 ya lengo la miaka minne la shilingi trilioni 38.4

2.2  Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda

 1. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 umejikita katika kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan za kilimo, madini na gesi asilia. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ni kama ifuatavyo:

 • (i) Uzalishaji Viwandani: kujengwa kwa jumla ya viwanda vipya 8,477 kati ya mwaka 2015 – 2019 ambapo viwanda vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Ujenzi wa viwanda hivyo umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi viwanda 61,110 mwaka 2019. Viwanda hivyo vimechangia ongezeko la uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa soko la ndani na la nje ikijumuisha bidhaa za ngozi, ujenzi (nondo, mabati, saruji, misumari na rangi), plastiki, zana za kilimo, vinywaji na marumaru. Baadhi ya viwanda vilivyojengwa ni: kiwanda kipya cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd (awamu ya kwanza) katika mkoa wa Kilimanjaro na kuanza maandalizi ya awamu ya pili ya kiwanda cha Nguru kilichopo Mvomero, Morogoro kwa ajili ya kuchakata nyama; kiwanda cha Pipe Industries Co. Limited kinachozalisha mabomba kilichopo Vingunguti, Dar es Salaam; majengo ya viwanda (Industrial Sheds) kwa ajili ya wajasiriamali katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Geita, Mtwara na Ruvuma; kiwanda cha chai cha Kabambe (Njombe); kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd kinachobangua korosho (Mikindani – Mtwara); viwanda vya Goodwill Tanzania Ceramic Co. Ltd na Keda (T) Ceramics Company Ltd vilivyopo mkoa wa Pwani vinavyozalisha marumaru; kiwanda cha Plasco Pipelines Co. Ltd (Dar es Salaam) kinachozalisha bidhaa za plastiki; kiwanda cha Africa Dragon Enterprises Limited (Pwani) kinachozalisha mabati; jengo la kiwanda kipya cha kuunganisha matrekta TAMCO – Kibaha; Kiwanda cha kuchakata mazao katika mkoa wa Dodoma; na kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Tangawizi katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Uwekezaji huo umeleta mafanikio yafuatayo: Kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 7.9 mwaka 2015 hadi asilimia 8.5 mwaka 2019; kukua kwa sekta ya uzalishaji viwandani kwa wastani wa asilimia 8.3 kwa mwaka ambapo kumechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani ikijumuisha saruji, marumaru, nondo na bati; kuzalishwa kwa fursa za ajira kutoka ajira 254,786 mwaka 2015 hadi ajira 482,601 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 47.2; na kuchangia katika mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi kutoka asilimia 13.8 mwaka 2016/17 hadi asilimia 14.2 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 45.3 kimetumika kuboresha na kuendeleza miradi ya uzalishaji viwandani;

 • Kilimo: kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji ambayo imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Kigugu – Mvomero yenye hekta 200 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98, Mvumi – Kilosa yenye hekta 249 (asilimia 100), Msolwa Ujamaa – Morogoro yenye hekta 675 (asilimia 98), Njage – Kilombero yenye hekta 325 (asilimia 100), Shamba la Mbegu Kilangali – Kilosa yenye hekta 400 (asilimia 80); kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 71,000 mwaka 2020; kukamilika kwa ujenzi wa maabara ya mbegu katika Makao Makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo – Morogoro; kuzalishwa kwa kilo 14,700 za mbegu za mpunga za daraja la awali (pre-basic) aina ya TXD 306, TXD 88, Komboka, Tai, Supa na NERICA 1; kuongezeka kwa upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,450 mwaka 2015 hadi tani 727,719 mwaka 2020; kukamilika kwa ujenzi wa maghala matano (5) ya kuhifadhi mpunga kupitia mradi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga – Expanded Rice Production Project; kusambazwa kwa tani 40,592.6 za salfa na lita 1,314,465 za viuatilifu maji kwa wakulima wa korosho; kuendeshwa kwa minada nane (8) ya kahawa katika mikoa ya Kilimanjaro (2), Songwe (4) na Ruvuma (2); na kukaguliwa kwa viwanda 24 na maghala 30 na kutolewa leseni za kuendesha biashara ya kahawa.

 

Hatua hizi zimechangia kupatikana kwa mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuongezeka kwa utoshelevu wa chakula kufikia asilimia 118 mwaka 2019/20; kupungua kwa mfumuko wa bei za chakula kufikia wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2020; na kupungua kwa Umaskini wa Chakula kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia asilimia 8.0 mwaka 2017/18. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 188.9 kimetumika kuboresha na kuendeleza sekta ya kilimo;

 • Mifugo: kujenga kiwanda kipya cha Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd chenye uwezo wa kuzalisha jozi na soli za viatu 1,200,000 kwa mwaka na kuchakata ngozi futi za mraba 13,000,000 kwa mwaka; kuimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC kilichopo USA River Arusha kwa kununua kifaa (Chiller) kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha kimiminika cha naitrojeni; kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati vya nyama vya Tanchoice (Pwani), Elia Food Oversees Limited (Arusha) na Binjiang Company Limited (Shinyanga); kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverage Company Limited (Arusha); kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience Africa Limited (Pwani) chenye uwezo wa kuzalisha chanjo aina 37; na kuendelea kuboresha huduma za malisho ya mifugo na majosho.

Utekelezaji huu umewezesha mafanikio yafuatayo: kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama nchini kutoka 25 mwaka 2015/16 hadi viwanda 32 mwaka 2019/20 na viwanda vya kusindika maziwa kutoka 82 mwaka 2015/16 hadi 99 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usambazaji wa mitamba katika mashamba ya Serikali kutoka mitamba 11,449 mwaka 2015/16 hadi mitamba 18,255 mwaka 2019/20; kuongeza idadi ya majosho ya kuogeshea mifugo kutoka majosho 2,428 mwaka 2015/16 hadi majosho 2,513 mwaka 2019/20; kuongezeka maeneo ya malisho ya mifugo kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2015/16 hadi hekta milioni 2.85 mwaka 2019/20; kuendelea kukamilisha ujenzi wa machinjio ya kisasa Vingunguti; na kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na zao la ngozi kutoka shilingi bilioni 1.73 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 9.1 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano shilingi bilioni 5.66 zimetumika kuboresha na kuendeleza sekta ya mifugo;

 • Uvuvi: kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 362,645 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.48 mwaka 2015/16 hadi tani 497,567 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 2.34 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya sangara kutoka tani 23,000.58 mwaka 2015/16 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda masoko ya Ulaya ambapo katika mwaka 2019/20, jumla ya kilo 777,750.0 za mabondo zilisafirishwa; kuongezeka kwa mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 379.25 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 506.24 mwaka 2019/20; na kuendelea na maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na ununuzi wa meli nne (4) za uvuvi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano shilingi bilioni 5 zimetumika kuboresha na kuendeleza sekta ya uvuvi;

 • Madini: kupitia na kutunga Sheria, Sera na mikataba ya madini; kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzania (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84) ambapo imetoa gawio la shilingi bilioni 100; kusainiwa kwa mkataba wa ubia wa kampuni ya LZ NICKEL na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuendeleza na kuchimba madini ya Nickel ambapo chini ya mkataba huo imeundwa kampuni ya ubia inayoitwa Tembo Nickel Corporation Limited (kwa umiliki wa hisa 84% kwa Kampuni ya LZ Nickel na Serikali ya Tanzania Hisa 16%); kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya kuuzia madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya; kuimarishwa kwa ulinzi wa rasilimali za madini kwa kujenga ukuta wenye mzingo wa kilomita 24 wa Mirerani mkoani Manyara pamoja na kujenga One Stop Centre, kufunga vifaa vya ulinzi ikiwa ni pamoja na taa na CCTV Camera kuzunguka ukuta na barabara ya kuzunguka ukuta wa ndani; kuimarisha taasisi zilizo chini ya Wizara kwa kuzipatia vitendea kazi; na kukamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) vya mfano vya uchenjuaji wa madini ya dhahabu kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Lwamgasa (Geita), Katente (Bukombe) na Itumbi (Chunya).

Hatua hizi zimechangia Sekta ya Madini kukua kwa wastani wa asilimia 8.0 kati ya mwaka 2016 na 2019; mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019/20 kutoka asilimia 4.6 mwaka 2015/16 na kuimarika kwa huduma kwa jamii zinazozunguka migodi. Aidha, mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 1,912 (sawa na shilingi bilioni 4,464.71) mwaka 2015/16 hadi dola za Marekani milioni 2,898.8 (sawa na shilingi bilioni 6,769.0) mwaka 2019/20; na maduhuli kutoka shilingi bilioni 196 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 528.3 mwaka 2019/20 na kukusanya shilingi bilioni 317.5 sawa na asilimia 120.6 ya lengo la shilingi bilioni 263.36 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano shilingi bilioni 82.2 zimetumika kuboresha na kuendeleza miradi ya madini;

 • Maliasili na Utalii: kujengwa na kukarabatiwa viwanja vya ndege; kununuliwa kwa ndege; kuongezwa kwa safari za ndege ndani na nje ya nchi; kudhibiti ujangili, kuongeza idadi ya watalii na mapato kupitia Mradi wa Kujenga Uwezo katika Hifadhi za Taifa, Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Maliasili na Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii kusini mwa Tanzania (REGROW); kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi ambapo jumla watalii 1,171 walitembelea hifadhi hii kati yao 996 ni wa ndani na 175 ni wa nje ambapo jumla ya shilingi 492, 741, 622 zimekusanywa kuanzia Novemba, mwaka 2019 hadi Desemba, 2020; kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo jumla ya watalii 9,938 (6,189 wa nje na 3,749 wa dani) walitembelea Hifadhi tangu mwezi Novemba, 2019 hadi Desemba, 2020 ambapo jumla ya shilingi za kitanzania 1,552,712,660 zimekusanywa; na kuendelea kutangazwa kwa vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani.

Hatua hizi zimechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,527,230 mwaka 2019. Aidha, wastani wa idadi ya siku zinazotumiwa na watalii kukaa nchini zimeongezeka kufikia siku 13 mwaka 2019 ikilinganishwa na siku 10 mwaka 2015. Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.9 (sawa na shilingi bilioni 4,436.7) mwaka 2015 hadi dola za Marekani bilioni 2.6 (sawa na shilingi bilioni 6,071.3) mwaka 2019. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 269.7 kimetumika kuboresha na kuendeleza sekta ya Maliasili na Utalii.

 

 • Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu

 1. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa huduma za afya, maji na elimu, umeongeza kasi ya ufungamanishaji wa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:

 • (i) Afya: Kuendelea kutoa huduma za kupandikiza uloto (bone marrow transplant) na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wodi namba 18 ya Sewa Haji pamoja na ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa binafsi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili; Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la X-ray katika Hospitali ya Rufaa Dodoma; kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru – Dodoma; kununuliwa kwa mashine za digital X-ray na ultrasound, vifaa vya maabara na mashine za uchunguzi wa kifua kikuu kwa kuotesha vimelea BACTEC 960 (Mycobacteria Growth Indicator Tube – MGIT) na Blood culture machine katika Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu – Kibong’oto; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; kujenga na kuboresha miundombinu ikijumuisha: jengo la huduma za upasuaji; radiolojia; jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje; maabara; na jengo la mama na mtoto katika hospitali za rufaa za Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara na kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya na Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Kanda ya Ziwa ya Burigi (Geita).

Vile vile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya ambayo imefikia hatua mbalimbali ikiwemo: kufikia asilimia 98 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala; kukamilika na kuanza kutumika kwa jengo la wagonjwa wa nje na kufikia asilimia 73 ya ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Rufaa Njombe; na ujenzi wa jengo la ghorofa moja la huduma za upasuaji, radiolojia na maabara na kufikia asilimia 50 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Simiyu. Aidha, mafanikio mengine ni pamoja na: ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; na kuongezeka kwa idadi ya zahanati kutoka 4,922 mwaka 2015 hadi 6,120 mwaka 2020, vituo vya afya kutoka 535 mwaka 2015 hadi kufikia vituo 710 mwaka 2020 na Hospitali za Halmashauri za Wilaya kutoka 77 mwaka 2015 hadi 179 mwaka 2020.

Hatua hizi zimechangia: Kuongezeka kwa wastani wa umri wa kuishi kutoka miaka 62 mwaka 2015/16 hadi miaka 66 mwaka 2019/20; kupungua kwa idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka wastani wa vifo 67 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2014/15 hadi vifo 50.3 mwaka 2019/20; kupungua kwa vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kutoka vifo 432 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa watoto wanaozaliwa kwa kuhudumiwa na wahudumu wa afya wenye ujuzi kutoka asilimia 51 mwaka 2015/16 hadi asilimia 80 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 736.67 zimetumika katika utekelezaji wa miradi ya afya;

 • Elimu: Ujenzi wa miundombinu muhimu katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na Sekondari 883), mabweni 547, nyumba za walimu 101, majengo ya utawala 25 na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa maboma 2,815 katika shule za msingi 2,133; kuendelea kugharamia posho ya madaraka kwa walimu wakuu, fidia ya ada kwa wanafunzi na ruzuku ya uendeshaji wa shule ambapo shilingi trilioni 1.22 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila ada; kukarabatiwa shule kongwe 84 kati ya 89; kuboreshwa kwa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi (Folk Development Colleges – FDC); kutolewa kwa mikopo ya elimu ya juu jumla ya shilingi trilioni 2.26; kuanzishwa kwa vituo vya umahiri vya mafunzo katika taasisi za elimu ya ufundi; na kuimarishwa kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji katika taaluma za Anga na Chuo cha Ufundi Arusha katika taaluma ya Nishati; na kukamilika na kuzinduliwa kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja pamoja na hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Hatua hizi zimechangia: Kuongezeka kwa kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi kutoka asilimia 93.3 mwaka 2015 hadi asilimia 110.6 mwaka 2020; kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi stadi kutoka 196,091 mwaka 2015/16 hadi 320,143 mwaka 2019/20 na elimu ya ufundi kutoka 117,067 mwaka 2015/16 hadi 151,379 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini kutoka 65,064 mwaka 2015/16 hadi kufikia  87,813 mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 125,126 mwaka 2015 hadi kufikia 132,392 mwaka 2020. Aidha, kiwango cha ufaulu wa mitihani ya Darasa la Saba kimeongezeka kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 81.5 mwaka 2019 na Sekondari (Kidato cha nne) kutoka asilimia 68 mwaka 2015 hadi asilimia 80.7 mwaka 2019. Vile vile, wanafunzi waliohitimu elimu ya juu walifikia 60,940 mwaka 2019/20, elimu ya mafunzo stadi 90,849 mwaka 2018/19 na elimu ya ufundi 86,547 mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi trilioni 3.15 zimetumika kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu;

 • Maji: Kukamilika kwa miradi 1,423 ya maji iliyotekelezwa mijini na vijijini. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika kwa miradi ya maji katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 90); utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega umefikia asilimia 98; kukamilika kwa asilimia 76 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Mwanza; kukamilika kwa asilimia 62 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Arusha; na kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65. Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na umehusisha maeneo ya Kibamba hadi Kisarawe, Mlandizi hadi Chalinze, Kisarawe-Pugu-Ukonga, Mbezi Luis, Kiluvya, Tegeta, Wazo, Madale, Mivumoni, Mabwepande na Bagamoyo (maeneo ya Vikawe, Zinga, Mapinga na Kerege).

Kwa ujumla miradi yote iliyotekelezwa imewezesha wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma ya maji ambapo wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama  imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020 kwa mijini na kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 70.1 mwaka 2020 kwa vijijini. Aidha, kwa Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa maji safi umeongezeka kutoka asilimia 72 mwaka 2015 hadi asilimia 90 Desemba, 2020. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi trilioni 2.03 zimetumika kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini;

 • Utawala Bora: Kuanzishwa kwa mahakama ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi; ujenzi wa ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi; kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama Kuu mbili (2) katika mikoa ya Mara na Kigoma na ukarabati wa Mahakama Kuu tatu (3) katika mikoa ya Mbeya, Tanga na Rukwa; kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi tano (5) katika mikoa ya Pwani, Geita, Simiyu, Manyara na Njombe; kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za Wilaya 15 katika wilaya za Bagamoyo, Mkuranga, Kigamboni, Ilala, Ngorongoro, Chato, Bukombe, Kilwa, Ruangwa, Kondoa, Chunya, Wanging’ombe, Makete, Longido na Kasulu; kukamilika kwa Ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 18 za Karatu (Arusha), Totowe (Songwe), Robanda (Serengeti), Itinje (Meatu), Old Korogwe na Magoma (Korogwe), Mkunya (Newala), Mvomero, Ngerengere, Mlimba, Mang’ula (Morogoro), Mtae (Lushoto), Msanzi (Laela) na Mtowisa (Sumbawanga), Lugarawa (Ludewa), Uyole (Mbeya) na Mlowo (Mbozi); na kuanzishwa kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

 

Hatua hizi zimechangia kuongezeka kwa idadi ya kesi za rushwa zilizotolewa maamuzi kutoka asilimia 10.4 mwaka 2015/16 hadi asilimia 82.0 mwaka 2019/20; kupungua kwa mlundikano wa mashauri katika mahakama ya Tanzania kutoka asilimia 13 ya mashauri yaliyokuwepo mahakamani mwaka 2015 hadi asilimia tano (5) mwaka 2019; na kuongezeka kwa upatikanaji wa haki karibu na wananchi; uwiano wa halmashauri zilizobandika bajeti kwenye mbao za matangazo za umma ulifikia asilimia 86 ya lengo la halmashauri zote; kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 bila kutegemea misaada kutoka nje ya nchi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 268.5 kilitumika; na kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma ambapo shilingi bilioni 194.5 zimetumika. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 530.8 zilitumika kutekeleza miradi hii; na

 • Ajira: Kutokana na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21 jumla ya ajira 12,773,126 zimezalishwa. Kati ya ajira hizo, ajira za moja kwa moja ni 11,891,772 na ajira zisizo za moja kwa moja ni 881,354. Aidha, jumla ya vijana 65,008 katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi ikiwemo mafunzo ya uanagenzi katika fani za ujenzi, useremala, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, ufundi magari, ufundi bomba, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, uchomeleaji na uungaji vyuma, kilimo na ufugaji, ushonaji, uchorongaji vipuli, uchapaji nyaraka na TEHAMA. Serikali imeendelea kulinda ajira za wazawa kwa kuhakikisha kuwa wageni wanaokuja kufanya kazi nchini  wanakidhi vigezo vilivyoainishwa  katika Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na. 1 ya mwaka 2015.

 • Mazingira Wezeshi kwa Uwekezaji na Uendeshaji Biashara

 1. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika eneo hili ni kama ifuatavyo:

 • (i) Nishati ya Umeme: Kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115 ambapo kwa ujumla utekelezaji umefikia asilimia 25.8. Kwa ujumla kiasi cha shilingi trilioni 85 kimetumika kutekeleza mradi huu.

Hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi mingine ni: Kukamilika kwa asilimia 100 kwa miradi ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I MW 150, Kinyerezi II MW 240 na mradi wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 kutoka Makambako hadi Songea; kukamilika kwa asilimia 73 ya utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme – Rusumo MW 80; kukamilika kwa asilimia 98 ya ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Bulyanhulu – Geita; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 76, kuendelea na utekelezaji wa  mradi wa Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea na mapitio ya usanifu wa miradi ya Kufua Umeme wa Maji ya Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222; na kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kuendelea na uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi.

Utekelezaji wa miradi hiyo umechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa nishati ya umeme kufikia MW 1,602.3 mwaka 2019/20 kutoka MW 1,308 mwaka 2015/16; kiwango cha upotevu wa umeme kupungua kutoka asilimia 19.0 mwaka 2015/16 hadi asilimia 16.4 mwaka 2019/20; na kuunganishwa umeme kwa  jumla ya vijiji 10,018 kati ya vijiji 12,317 hadi Desemba 2020, sawa na asilimia 81.3. Ongezeko la uzalishaji wa nishati ya umeme limepunguza adha ya upatikanaji wa umeme katika shughuli za uzalishaji viwandani. Aidha, usambazaji wa umeme vijijini umewezesha wananchi wa kipato cha chini kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, hususan viwanda vidogo vya kusindika mazao katika maeneo ya vijijini. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, jumla ya shilingi trilioni 2.83 zimetumika kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo;

 • Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,209 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka 2019/20 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa.

Miradi iliyotekelezwa ni pamoja na: Kukamilika kwa ujenzi wa barabara sehemu ya Tabora – Nyahua (km 85), Manyoni – Itigi – Chaya (km 89.35), Kidahwe – Uvinza (km 76.6), Tabora – Ndono (km 42), Ndono – Urambo (km 52) na Kaliua – Kazilambwa (km 56); kukamilika kwa barabara ya Mpanda – Ifukutwa – Vikonge (km 30); kukamilika kwa barabara ya Kidahwe – Kasulu (km 63); kukamilika kwa ukarabati wa sehemu ya Ushirombo – Lusahunga (km 110); kuzinduliwa na kuanza kutumika kwa barabaya ya juu (Interchange) ya Ubungo; kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mfugale (Dar es Salaam); ujenzi wa barabara ya Nyakanazi – Kakonko (km 50) umefikia asilimia 90.8; ujenzi wa barabara ya Makutano – Natta umekamilika kwa asilimia 86.0; ujenzi kwa sehemu ya Mbinga – Mbamba Bay (km 66) utekelezaji umefikia asilimia 85.5 na sehemu ya Mtwara – Mnivata (km 50) asilimia 90; na kukamilika kwa asilimia 92.9 ya upanuzi wa barabara sehemu ya  Kimara – Kiluvya (km 19.2).

Vile vile, kukamilika kwa ujenzi wa madaraja makubwa 12 ambayo ni Magufuli (Morogoro), Nyerere (Dar es Salaam), Magara (Manyara), Kavuu (Katavi), Ruvu Chini (Pwani), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Momba (Rukwa), Lukuledi (Lindi), Lukuledi II (Lindi), Mara (Mara), Sibiti (Singida) na Mtibwa (Morogoro) na kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 95, Daraja jipya la Tanzanite (Dar es Salaam) asilimia 55.2, Kitengule (Kagera) asilimia 50 na New Wami (Pwani) asilimia 41.4 na kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 5.8.

Ongezeko la mtandao wa barabara na ujenzi wa madaraja umerahisisha usafirishaji wa bidhaa na mazao ya kilimo, malighafi na bidhaa za viwandani pamoja na huduma ya usafiri kwa wananchi katika maeneo yaliyokuwa hayafikiki. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi trilioni 8.60 kimetumika kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara na madaraja makubwa; 

 • Reli: Serikali inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railways – SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 49.2, kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km 133). Hadi Desemba 2020, kiasi cha shilingi trilioni 3.79 kimetumika kutekeleza mradi huu.

Aidha, ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam – Isaka (km 970) sehemu ya Dar es Salaam – Kilosa (km 283) umefikia asilimia 94.0 na Kilosa – Isaka (km 687) asilimia 99.8 ambapo katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 334.6 zilitumika na shilingi bilioni 97.0 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 728.3 kimetumika kukarabati miundombinu ya reli ya kati.

Shughuli nyingine zilizofanyika ni pamoja na: kukarabati na kurejesha huduma za reli ya Tanga hadi Arusha (km 439); kurejesha huduma ya kusafirisha shehena za mizigo kwa njia ya reli kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Uganda; kununuliwa kwa vichwa vipya 11 vya treni na kukarabatiwa kwa mabehewa 347 ya mizigo na mabehewa 20 ya abiria. Hatua hizi zimeongeza njia za usafirishaji na zimerahisisha upatikanaji wa huduma za uhakika za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo na kufungua fursa za kibiashara na uwekezaji. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 503.4 kimetumika kuboresha na kurejesha huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya reli kwa kanda ya kaskazini (Dar es Salaam – Tanga – Moshi – Arusha).

Kwa upande wa reli ya TAZARA baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni: Kununuliwa na kuanza kutumika kwa vichwa vipya vinne (4) vya treni ya njia kuu, vichwa vipya vinne (4) vya treni ya sogeza, mabehewa mapya 18 ya abiria, mashine mbili (2) za uokaji, mitambo na vifaa vya usalama, ukarabati wa mabehewa 400 ya mizigo, kununuliwa kwa mitambo ya kupakia na kupakua mizigo mizito, kusafirishwa kwa jumla ya tani 983,941 za mizigo katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi Desemba 2020 na kusafirishwa kwa jumla ya abiria 5,191,806 katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi Desemba 2020. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 171.865 kimetumika kuboresha reli ya TAZARA.

 • Bandari: Katika Bandari ya Dar es Salaam shughuli zilizofanyika ni: Kuboreshwa kwa gati namba 1 – 4 (gati namba 1-3 kwa ajili ya mizigo mchanganyiko na gati namba 4 kwa ajili ya mizigo ya kichele mfano ngano na mbolea); kukamilika kwa ujenzi wa gati la kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na uboreshaji wa gati Na. 5 hadi 7 (gati namba 5 kwa ajili ya mizigo ya kichele na gati namba 6-7 ni kwa ajili ya makontena). Hatua hizi zimechangia kupungua kwa idadi ya siku za meli kukaa bandarini kutoka siku saba (7) hadi siku tano (5) na kuongezeka kwa shehena ya mizigo iliyohudumiwa kutoka tani milioni 15.4 hadi tani milioni 19.52. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 253.7 kimetumika kutekeleza mradi huu.

Katika Bandari ya Mtwara ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia makasha umekamilika. Hadi Desemba 2020, kiasi cha shilingi bilioni 88.6 kimetumika kutekeleza mradi huu tangu ulipoanza. Katika Bandari ya Tanga uendelezaji wa kina cha lango la bandari kutoka mita 4 hadi mita 13 na ujenzi wa gati mbili kwenye kina kirefu umekamilika. Hadi Desemba 2020, kiasi cha shilingi bilioni 86.9 kimetumika kutekeleza mradi huu.

 • Usafiri wa abiria na mizigo katika Maziwa Makuu: Ziwa Victoria na Tanganyika: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400; kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza; kupatikana kwa makandarasi kwa ajili ya ukarabati wa meli za MV. Umoja na MV. Serengeti na kukamilika kwa maandalizi ya mikataba kwa ajili ya ukarabati wa meli hizo; na kukamilika ukarabati wa meli za MV. Clarias na ML. Wimbi. Aidha, shughuli nyingine zilizokamilika ni: Ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero; ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; ukarabati wa majengo na ofisi za bandari za Ziwa Victoria; kuboresha eneo la kushukia abiria Mwanza North; na ukarabati wa ‘Link Span’ ya bandari ya Mwanza South. Aidha, katika Ziwa Tanganyika, mikataba kwa ajili ya Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 imesainiwa pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba; na ukarabati wa meli ya MT. Sangara. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 142.0 kimetumika kuboresha na kuendeleza hali ya usafiri na usafirshaji katika Ziwa Victoria na Tanganyika.

Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja; na ujenzi wa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 umekamilika na kuanza kutoa huduma. Hadi Desemba 2020, kiasi cha shilingi bilioni 17.5 kimetumika kutekeleza mradi huu tangu ulipoanza;

 • Viwanja vya Ndege na Rada: Kukamilika kwa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere – JNIA chenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka; kuendelea na ujenzi wa viwanja vya Geita (asilimia 86), Songea (asilimia 91) na Mtwara (asilimia 49.0); kukamilika kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni 759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga vinavyogharimu Euro milioni 50 sawa na shilingi bilioni 136.85; kuanza kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja wa Musoma; kukamilika kwa ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege na kununuliwa kwa magari mapya matatu (3) ya zimamoto yenye uwezo wa kubeba lita za maji 10,000 kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA); kupanuliwa kwa barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege cha Dodoma; kufungwa kwa mifumo ya kuongoza ndege (AGL) katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Tabora na Mwanza; na kupanuliwa na kukarabatiwa kwa viwanja vya ndege vya Bukoba, Mwanza, Arusha, Nachingwea na Iringa. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 404.0 kimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege.

Kununuliwa kwa rada nne (4) za kuongoza ndege za kiraia na kufungwa katika viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Songwe na Mwanza na hivyo kuongeza kiwango cha usalama wa abiria katika viwanja vya ndani. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 79.8 kimetumika kuimarisha usafiri wa anga nchini;

 

 • Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Kununuliwa kwa ndege mpya 11 kutoka ndege moja (1) iliyokuwepo mwaka 2015 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12; na kupatiwa mafunzo kwa marubani 110, wahandisi 127 na wahudumu wa ndani ya ndege 131. Hatua hizi zimechangia kuimarika kwa huduma za usafiri wa anga kutoka vituo vinne (4) mwaka 2015 hadi vituo 13 vya ndani ya nchi na vituo saba (7) vya nje ya nchi mwaka 2020 na kuongezeka kwa idadi ya miruko ya ndege ndani na nje kutoka 225,103 mwaka 2015 hadi miruko 292,105 mwaka 2019. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi trilioni 1.24 kimetumika kuboresha Shirika la Ndege Tanzania;

 • Mawasiliano na Uchumi wa Kidigitali: Ujenzi wa mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaendelea ambapo: awamu ya tatu ya ujenzi imekamilika ikijumuisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Data cha Dar es Salaam na uunganishwaji wa Zanzibar kwenye Mkongo wa Taifa. Mradi wa mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi unaendelea kutekelezwa ambapo: uwekaji wa miundombinu ya Mfumo umefanyika katika kata za mikoa ya : Dar es Salaam (46), Arusha (8), Dodoma (17), Mwanza(8), Tanga (5), Kilimanjaro (8), Geita (3), Shinyanga (5), Pwani (3), Morogoro (7) pamoja na wadi 8 za Zanzibar ; na ufungaji wa nguzo zenye majina ya barabara umefanyika katika halmashauri 12 za majiji ya Dodoma, Mwanza na Tanga. Mradi wa ujenzi wa kituo cha Kutengeneza Vifaa vya TEHAMA ambapo hatua iliyofikiwa ni: kuanza kwa Programu ya kuendeleza wajasiriamali wadogo wanaotengeneza bidhaa za TEHAMA nchini chini kituo cha Soft Center ambapo kampuni sita (6) za wajasiriamali zimepata mafunzo; na kununuliwa kwa samani na vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kituo. Aidha, Programu ya Miundombinu ya Kikanda

Uwekezaji huu umechangia kuongezeka kwa idadi ya laini za simu kutoka milioni 39 hadi milioni 48.6; idadi ya watumiaji wa mitandao ya simu kuongezeka kutoka milioni 9 hadi milioni 27 na kupungua kwa gharama za kupiga simu za mkononi  kutoka shilingi 274 kwa dakika kwa mwaka 2015 hadi shilingi 70 kwa dakika mwaka 2020. Aidha, huduma za mawasiliano kwa njia ya simu za viganjani zimeenda sanjari na ongezeko la huduma jumuishi za fedha (financial inclusion), na biashara mtandao (e-commerce). Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 874 kimetumika kutekeleza miradi hii;

 

 • Serikali Mtandao na Mifumo ya Kielektroniki: Huduma za Serikali Mtandao zimeimarishwa kwa kuongeza kiwango cha ubora wa huduma zinazotolewa na Serikali kwa wadau mbalimbali ambapo mifumo ya Serikali mtandao imeongezewa mawanda. Mtandao wa Serikali (e-Government) umeunganishwa kwenye ofisi za Taasisi za Serikali 305 ili kuwezesha mawasiliano ya haraka na salama. Aidha, Serikali mtandao kupitia mkongo wa Taifa wa mawasiliano imefikia jumla ya vituo 150 katika makao makuu ya Wilaya, vituo 150 katika hospitali za Wilaya, vituo 121 vya polisi, vituo 65 katika ofisi za posta, vituo 26 katika mahakama na vituo 620 katika shule za sekondari.

Hatua hizi zimechangia mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za miamala, hususan utunzaji wa kumbukumbu za wateja utoaji wa Ankara, kupunguza matumizi ya shajala kurahisisha malipo ya ada, tozo na kodi. Vile vile, huduma mtandao imerahisisha utoaji huduma na kupunguza muda wa kuhudumia wateja. Matumizi ya mifumo mipya ya TEHAMA kama vile Mfumo wa Pamoja wa Ukusanyaji wa Kodi na Maduhuli ya Serikali (Government Electronic Payment Gateway – GePG) umeiwezesha Serikali kuongeza mapato kutokana na kuunganishwa kwa taasisi 682 za Serikali. Aidha, Mfumo wa Kusimamia Simu za Kimataifa (Teletraffic Monitoring System – TTMS) umewezesha kukusanya jumla ya shilingi bilioni 62.1 ikiwa ni mapato ya moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Vile vile, mifumo ya kielekroniki ya usajili wa kampuni, ugomboaji na usafirishaji wa mizigo imeanzishwa ili kuongeza ufanisi na tija katika sekta ya ugomboaji na usafirishaji wa mizigo. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, kiasi cha shilingi bilioni 1.4 kimetumika kuboresha Serikali Mtandao na mifumo ya kielektroniki; na

 • Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint): Jumla ya tozo, ada na adhabu 232 zimefutwa na kupunguzwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, mifugo, uvuvi na maji; kutungwa na kuboreshwa kwa baadhi ya sheria ikiwemo Sheria mpya ya Usuluhishi wa Migogoro (Abitration Act 2020); kufanya maboresho katika mifumo ya kielektroniki ikiwemo kujengwa kwa Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG), mfumo wa usajili na utoaji wa leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na mfumo wa Intergrated Standard, Quality Assurance, Metrology and Testing (ISQMT); kuunganisha mifumo ya kielektroniki katika taasisi ikiwemo mifumo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambao umeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa utoaji wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN), mfumo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa utambuzi wa maeneo ya viwanda; na kufanya marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali ili kuondoa muingiliano wa majukumu ya Taasisi na Mamlaka za udhibiti. Hatua hizo zimeboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuiwezesha Tanzania kushika nafasi ya 141 kati ya nchi 190 mwaka 2020 ikilinganishwa na nafasi ya 144 mwaka 2019.

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ulikabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo: Uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko; kupungua kwa shughuli za kibiashara duniani kulikotokana na athari za COVID-19; na ukwepaji kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu hususan kupitia njia za magendo, uhamishaji wa faida (transfer pricing) kwa kampuni zenye mtandao wa kimataifa na kutokutoa stakabadhi za kielektroniki (EFD receipt) wakati mauzo yanapofanyika.

 1. Mheshimiwa Spika, Hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na: kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na kuimarisha ukaguzi wake; kuendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa biashara duniani ili kutumia fursa zilizotokana na athari za COVID-19 kwa manufaa mapana ya nchi pamoja na kuchukua hatua za kisera na kiutawala kurejesha biashara zilizoathirika; na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kuendelea kuhamasisha umma juu ya matumizi ya stakabadhi za kielektroniki.

 • MAPENDEKEZO YA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2021/22 – 2025/26

 

 1. Mheshimiwa Spika, masuala ya msingi yatakayowezesha kufikia shabaha za uchumi jumla ni pamoja na: Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na nchi jirani; Kuhimili athari za majanga ya asili kama vile mafuriko na magonjwa ya mlipuko; Ushiriki mpana wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi; Hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha ziada; na Kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya kimataifa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Shabaha za Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ni pamoja na:
 • Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka kuongezeka kutoka asilimia 6.0 mwaka 2021 na kufikia wastani wa asilimia 8.0 ifikapo mwaka 2026;

 • Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri kuongezeka kutoka asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 hadi asilimia 16.8 mwaka 2025/26;

 • Mfumuko wa bei kuendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika kipindi cha muda wa kati;

 • Akiba ya fedha za kigeni kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne; na

 • Sekta binafsi kuzalisha ajira mpya zipatazo milioni nane kati ya Julai 2021 na Juni 2026.

 1. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unajengwa katika misingi ya nguzo kuu tatu (3) ambazo ni utawala bora, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu ambazo zinatengeneza maeneo makuu matano (5) ya kipaumbele. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:

 • Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: Eneo hili linajumuisha miradi ambayo itajikita katika: kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kuchochea utulivu wa viashiria vya uchumi jumla; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuchochea uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje; na kuendeleza miundombinu na huduma za reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini na angani, TEHAMA, nishati, bandari na viwanja vya ndege;

 • Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma: Eneo hili linajumuisha miradi ya viwanda inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini. Aidha, eneo hili linajumuisha pia miradi na programu inayolenga kuboresha huduma za utalii, fedha na bima;

 • Kukuza Biashara: Eneo hili linajumuisha programu zitakazoimarisha masoko ya ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimataifa katika kukuza biashara. Aidha, masoko yanayolengwa ni yale yatakayotoa fursa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, ikiwemo bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu;

 

 • Kuchochea Maendeleo ya Watu: Eneo hili linajumuisha utekelezaji wa miradi ambayo inajikita katika kuboresha maisha ya watu ikiwemo: elimu na mafunzo kwa ujumla; afya na ustawi wa jamii; kinga ya jamii; huduma za maji na usafi wa mazingira; mipango miji, nyumba na maendeleo ya makazi; na athari dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi; na

 • Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili linajumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu nchini, kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ikiwemo kuwawezesha vijana kujiajiri. Vile vile, eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vile vile, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 utajumuisha utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kipaumbele. Miradi hiyo ni: Ujenzi wa Reli ya Kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railways – SGR); Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115; kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga; Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Kufua Umeme wa Maji – Ruhudji MW 358; Kufua Umeme wa Maji – Rumakali MW 222; Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa Reli ya Kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railways – SGR) kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga; Magadi Soda – Bonde la Engaruka, Utafutaji wa mafuta katika Vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay Kaskazini; Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa/Barabara za Juu ikijumuisha Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kanda Maalum za Kiuchumi; na Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalumu (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Mpango huu unakadiriwa kugharimu jumla ya shilingi trilioni 114.8 zikijumuisha mchango wa sekta binafsi wa shilingi trilioni 40.6 na sekta ya umma wa shilingi trilioni 74.2. Vyanzo vya fedha vya kugharamia Mpango kutoka Sekta ya Umma ni pamoja na mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, misaada na mikopo. Aidha, vyanzo mbalimbali bunifu vinavyoweza kutumika katika kugharamia shughuli za maendeleo vimeanishwa zikiwemo hati fungani za halmashauri na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

 1. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano yamezingatia maoni yaliyotolewa katika mikutano na mijadala maalum na Kamati ya Uongozi ya Bunge, Wizara, Idara, na Taasisi mbalimbali za Serikali, Washirika wa Maendeleo na sekta binafsi. Mapendekezo ya wadau ni kuwa, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano uandaliwe kwa kuzingatia modeli zinazoendana na uchumi na mazingira ya nchi yetu; maandalizi ya Mpango yazingatie changamoto za mipango iliyopita pamoja na fursa zilizopo sasa; Mpango uainishe sekta na aina za bidhaa ambazo tunalenga kuzikuza kwa ushindani; na kuendeleza juhudi za kurasimisha sekta isiyo rasmi kwa kutumia mifumo ya kidigitali.

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mgawanyo wa majukumu ya utekelezaji wa Mpango, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zitawajabika kutafsiri Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano katika mipango yao ya kila mwaka na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, Baraza la Taifa la Biashara litaratibu na kusimamia ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Mpango. Vile vile, Washirika wa Maendeleo watahamasishwa kushiriki katika utekelezaji wa Mpango kupitia vikao rasmi vya ushirikiano.

 1. Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu Mpango yanapatikana katika Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.

 • HITIMISHO

 

 1. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 yatawezesha nchi kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ikiwemo: kuboresha na kuimarisha hali ya maisha ya wananchi; ukuaji wa uchumi wenye uwezo wa kuhimili ushindani; kuimarika kwa misingi ya uchumi wa viwanda; kudumisha mazingira ya amani, usalama na umoja; kuimarika kwa uongozi bora na utawala wa sheria; pamoja na kujenga jamii iliyoelimika na inayojifunza.

 1. Mheshimiwa Spika, Kitabu cha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kimepangwa katika sura nane (8): Sura ya kwanza ni Utangulizi ambao unaelezea chimbuko na historia ya Dira ya Maendeleo 2025 na Mipango ya Maendeleo; Sura ya Pili inahusu Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa 2016/17 – 2020/21 ambayo yanajenga msingi wa maandalizi ya Mpango wa Tatu ambao unaendeleza mafanikio yaliyopatikana na kutatua changamoto zilizokabili Mpango wa Pili; Sura ya Tatu imejikita katika masuala ya maendeleo ya sekta binafsi msukumo ukiwa ni kuijenga Sekta Binafsi na kuishirikisha katika utekelezaji wa mpango; Sura ya Nne inaelezea dhana ya kujenga uchumi shindani, maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu; Sura ya Tano inaainisha hatua mahususi za kuchukuliwa katika maeneo ya kipaumbele ya Mpango; Sura ya Sita inahusu ugharamiaji wa utekelezaji wa Mpango; Sura ya Saba inaanisha mpangilio wa utekelezaji wa  Mpango; na Sura ya Nane inaainisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango.

 1. Mheshimiwa Spika, hoja ninayowasilisha leo mbele ya Bunge lako Tukufu ina lengo la kuomba maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ili kuboresha Mpango tunaouandaa. Hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wakati wa majadiliano ya Mapandekezo ya Mpango huu, pamoja na mambo mengine, ni vema wakajikita zaidi katika sura tatu (3) ambazo ni: Sura ya Tano inayohusu hatua mahsusi za kuchukuliwa katika maeneo ya kipaumbele; Sura ya Sita inayohusu ugharamiaji wa utekelezaji wa Mpango; na Sura ya Nane inayohusu ufuatiliaji na tathmini ambazo ndio mpango halisi utakaotekeleza Mipango ya Maendeleo kwa Miaka mitano ijayo.

 1. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.