………………………………………………………………………..
SERIKALI inaendelea na ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji Cha Lighwa kilichopo Jimbo la Singida Mashariki ambao unatarajiwa kukamilika Machi,mwaka 2021 ambapo kiasi cha Sh.Milioni 741 kimetolewa.
Hayo ni matokeo ya maombi ya mbunge wa Jimbo hilo Miraji Mtaturu aliyoyatoa mwaka 2019 bungeni ambapo kiasi Cha Shilingi Bilioni mbili kilipelekwa kwenye miradi ya vijiji vitatu vya Kipumbuiko,Lighwa na Kinku ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2021.
Akizungumza na mtandao huu Februari 6 Jijini Dodoma,Mtaturu ameishukuru sana serikali kwa kukubali maombi yake ya kutatua changamoto ya Huduma ya Maji kwenye jimbo lake.
“Pamoja na shukrani hizi niombe serikali kutenga fedha kwa ajili ya visima vilivyochimbwa katika vijiji vya Minyinga, Makiungu, Damankia,Mbwanjiki,Sakaa, Matare, Mang’onyi, Mampando na Mkunguwakihendo ili kujenga miundombinu wananchi wapate huduma ya maji,”alisema.
Wilaya ya Ikungi imeweza kutoa maji kwa Wananchi kwa asilimia 41 na kukamilika kwa miradi hii itaongeza huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 71.