Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Shafi Mpenda akiongea jana kuhusu maendeleo ya Halmashauri hiyo.
Muhidin Amri,
Madaba
WANAFUNZI wa shule mbili za sekondari ya Magingo,na Madaba katika Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma, wameondokana na upungufu wa vyumba vya madarasa kufuatia Halmashauri hiyo kukamilisha mradi wa ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika shule hizo.
Mkuu wa shule ya Magingo Said Kunemka amesishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya kwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Ep4r awamu ya nane ambapo jumla ya shilingi milioni 40 zilipelekwa kwa ajili ya kujenga vyumba viwili.
Kunemka alisema, fedha hizo zililenga kujenga vyumba viwili tu lakini kutokana na ushirikiano waliopata kutoka kwa wazazi na jamii ya kijiji,wamefanikiwa kuongeza ofisi moja, kutengeneza viti 80 na meza 80 kwa ajili ya wanafunzi watakaotumia vyumba hivyo vipya.
“tuko kwenye hatua ya mwisho kumalizia meza kwa ajili ya matumizi ya walimu,kimsingi tunaishukuru sana Serikali kutuletea mradi huu kwani umesaidia sana kumaliza uhaba wa madarasa kwenye shule yetu”alisema.
Alisema, katika ujenzi huo nguvu ya wananchi imetumika kwa kiasi kikubwa kwa kuleta mawe,tofali,kokoto, na kuchimba mtaro ambayo imewezesha kwa kiwango kikubwa ujenzi huo.
Alisema, kati ya milioni 40 walizopokea mpaka sasa wametumia shilingi milioni 35.4 na kubaki milioni 4.6 ambazo zimetumika kulipa meza na viti na kushukuru mwamko mkubwa wa jamii katika kuchangia na kusaidia sekta ya elimu.
Hata hivyo alisema, licha ya kukamilika kwa vyumba vya madarasa lakini shule hiyo inakabliwa na upungufu wa nyumba za walimu,jengo la utawala,Hosteli kwa wanafunzi ambapo shule kwa kushirikiana na wananchi wameanza kujenga bweni 1 kwa ajili ya wanafunzi wa kike.
Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo Mgini Chegenge ameiomba jamii,wazazi na wadau mbalimbali waendelee kujitolea kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo kwani bado ni changa inayohitaji ushiriki wa kila mtu.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari Madaba Emmanuel Mwamasika alisema, serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 25 mwaka 2020 ambazo zimetumika kujenga vyumba viwili vya madarasa na Halmashauri ya wilaya imeongeza shilingi milioni 6,kati ya hizo milioni 4 kujenga darasa 1 na milioni 2 kutengeneza meza na viti.
Alisema mbali na fedha hizo, Serikali ya awamu ya tano imeendelea kupeleka fedha kila mwezi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanaoishi shuleni na kupongeza mpango wa serikali kupeleka fedha za miradi moja kwa moja shuleni badala ya Halmashauri ya za wilaya.
Kwa mujibu wake,fedha hizo zimekwenda kuleta tija kubwa kwa kuchochea, kuongeza taaluma kwa wanafunzi na kuboresha mazingira bora ya kufundishia.
Aidha Mwamasika, ameipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kuboresha mazingira ya elimu na kuwataka wanafunzi wa shule kutumia fursa ya kuboreshwa kwa miundombinu ya shule kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao.
Hata hivyo,ameiomba kuendelea kuangalia kwa jicho la huruma shule hiyo kwani yapo baadhi ya majengo ya muda mrefu ambayo sasa yamechakaa na kutishia maisha ya wanafunzi na walimu pindi wanapokuwa madarasani .
“shule hii ni kubwa na ya muda mrefu sana,kwa hiyo kuna baadhi ya majengo yamechakaa na yanahitaji sana kufanyiwa ukarabati mkubwa”alisema.