Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri za Mkoa wa Tanga katika kikao kazi kilichofanyika jijini Tanga.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo Miriam Luka akisitisha huduma katika moja ya Kituo cha kulelea Watoto mchana kilichopo katika Manispaa ya Jiji la Tanga kwa kutoa huduma ya Malezi kwa watoto bila kusajiliwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Jonathan Budenu akielezea Jinsi Kada ya Ustawi wa Jamii inavyosaidia Jamii katika kutatua changamoto mbalimbali kwenye maisha ya kila siku wakati wa kikao kazi cha Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tanga.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu Tanga
Sakata la uendeshaji wa vituo vya kulelea Watoto Mchana (Day Care Centres) limeendelea kuchukua sura mpya ambapo Mkoani Tanga imebainika kuwa takribani nusu ya vituo Mkoani humo vinaendeshwa kinyemela.
Mafisa kutoka Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii wamefanya ukaguzi katika baadhi ya vituo na kubaini kuwa kati ya vituo 68 vya malezi ya watoto mchana, vituo 33 tu ndivyo vyenye usajili wa kutoa huduma hizo kisheria.
Kufuatia hali hiyo, timu ya Ukaguzi ikiongozwa na Mwakilishi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Miriam Luka ikalazimika kufunga vituo kadhaa vilivyokithiri na kuvitaka kufuata Sheria na Kanuni za uanzishwaji wa Vituo vya Malezi kwa watoto wadogo mchana.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo Miriam Luka amesema Vituo vya malezi kwa watoto mchana vinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zilizopo chini ya Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inayoelekeza namna ya endeshaji wa Vituo hivyo.
“Mimi nazungumza kwa niaba ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii hivi Vituo havifai kwa kutoa huduma kwa watoto wetu, mazingira hayafai kabisa tafuteni sehemu sahihi ndio muanzishe hivi Vituo”
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo Dkt John Jingu akiwa katika kikao kazi na Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tanga, amewaagiza Maafisa hao kote nchini kukagua na kufuatilia uendeshaji wa Vituo vya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (Day Care Centres) na kuona jinsi wanavyotoa huduma za Malezi kwa watoto.
Dkt. Jingu amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kote nchini kuhakikisha wanasimamia uendeshwaji wa Vituo vya Malezi na Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto mchana (Day Care Centers) ikiwemo kukagua maeneo na Huduma zinazotolewa na Vituo hivyo ili vitoe huduma stahili kwa watoto nchini.
“Tusimamie hivi Vituo kwa ukaribu watoto wetu wanaenda huko tuangalie Mazingira yake yakidhi vigezo vilivyowekwa ili tuweze kumpatia mtoto Malezi yanayostahili” alisema
Aidha Dkt. Jingu amesisitiza kuwa Kada ya Ustawi wa Jamii ni muhimu sana katika kuhakikisha Jamii inajengekeka vizuri na kutatua changamoto za jamii husika hasa katika masuala ya saikolojia.
Pia Dkt. Jingu amekemea uanzishwaji holela wa Vituo vya Malezi kwa watoto wadogo bila kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo hivyo amewataka Wamiliki wa Vituo hivyo kuzingatia Sheria ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa Vituo hivyo.
Awali Katibu Mkuu huyo katika kikao kazi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Jonathan Budenu ameiomba Wizara kuratibu ukaguzi wa Vituo hivyo mara kwa mara kwani Vituo vingi havina watoa huduma waliokidhi vigezo vya kutoa huduma ya Malezi kwa watoto.
Aidha amemuhakikishia Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu kusimamia maelekezo yote aliyoyatoa na kuhakikisha yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya Maendeleo ya mtoto.
Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo inaendesha operesheni ya kukagua uendeshwaji wa Vituo vya Makazi kwa watoto Mchana (Day Care Centers) na imeshafanyika katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam na kwa sasa inaendelea katika Mkoa wa Tanga kwa lengo la kuhakikisha Vituo vya Malezi ya Watoto wadogo mchana vinatoa huduma stahiki.