Home Mchanganyiko WAKULIMA 4,000 WA MTAMA KUNUFAIKA NA MRADI WA TBL PLc na WFP...

WAKULIMA 4,000 WA MTAMA KUNUFAIKA NA MRADI WA TBL PLc na WFP MSIMU WA 2021

0

Meneja Kilimo wa TBL Plc, Joel Msechu (katikati) akitoa mafunzo ya mfumo wa matumizi ya teknolojia ya BanQu kwa wakulima wa mtama wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma katika mafunzo yaliyofanyika wilayani humo mwishoni mwa wiki

Baadhi ya wakulima wa mtama wakimsikiliza kwa makini Meneja wa Kilimo wa TBL Plc,Joel Msechu wakai wa mafunzo ya kutumia teknolojia ya BanQu

 ……………………………………………………………………………………….

Kampuni ya Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL Plc) imeongeza makubaliano ya kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula (WFP) katika mradi wa pamoja wa kuendeleza zao la mtama msimu wa mwaka 2021. Mradi utashirikisha wakulima 4,000 ambao wanatarajiwa kuzalisha tani 10 za mtama.TBL Plc imekubali kununua mtama huo kwa bei ya shilingi 550 kwa kilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Plc, Philip Redman,alisema mradi wa mwaka 2021 ni mwendelezo wa mradi wa pamoja wa majaribio uliopata mafanikio makubwa kwa kuongeza mavuno kwa asilimia 70%  zaidi ya mwaka uliotangulia. Alisema pia mradi wa majaribio ulilenga kufanya kazi na wakulima 2,000 kwa kuwapatia elimu ya Kilimo cha kisasa, namna ya kuboresha mavuno na ubora wa mtama sambamba na  kuwapatia soko la uhakika la mazao  watakayozalisha.

Wakulima watawezeshwa kupata mkopo kutoka benki ya NMB Bank na kukata bima kutoka kampuni ya Jubilee na kupatiwa mbegu bora kwa mkopo,mbolea na pembejeo wanazohitaji ambapo gharama hizo zitalipwa wakati wa kipindi cha mwisho cha msimu wa mavuno.

Uzinduzi wa usambazaji wa mbegu za mtama ulifanyika wilayani Kongwa hivi karibuni ambapo maafisa kilimo kutoka TBL waliweza kufanya mikutano na wakulima kujadili changamoto wanazokabiliana nazo na kukutana na mawakala wa huduma ya bima ili kuwapatia wakulima elimu ya bima.

Meneja Kilimo wa TBL Plc Joel Msechu alisema “Msimu huu kampuni imezindua teknolojia ya BanQu  ambayo itawanufaisha wakulima 4,000 kwa kuwa inaongeza uwazi na ufuatiliaji katika katika mnyororo wetu wa ugavi . BanQu itawawezesha wakulima kuwa na rekodi ya kidigitali isiyoweza kubadilika ya miamala yao ya kifedha ,uzalishaji, mauzo, ununuzi (pembejeo), ulipaji, n.k na pia inamwezesha mkulima kulipwa kupitia simu ya mkononi ”.

 Alisema kampuni kwa sasa  inaendesha mafunzo juu ya matumizi ya teknolojia hiyo kwa wakulima, wasimamizi wao na watendaji wa Serikali katika maeneo husika “Mradi  unawahakikishia wakulima usalama wa chakula,kuingia katika mfumo rasmi wa kifedha,kuongeza uzalishaji na TBL kama mnunuzi inakuwa chanzo cha mapato kwao katika kuboresha hali za kipato chao,’’alisema Msechu.

Aliongeza kuwa msimu huu mwitikio  kutoka kwa wakulima ambao wanaotaka mbegu za mtama ni mkubwa ikilinganishwa na msimu uliopita na zoezi ya kuwapatia mbegu yanaendelea kupitia vikundi vyao.

Mmoja wa wakulima wa mtama ambaye pia ni kutoka Katibu wa Kikundi cha Wakulima wa mtama Kijiji cha Sagara B wilayani Kongwa, Theodora Mgaya, akizungumza kwa niaba ya mwenzake wakati wa mafunzo ya matumizi ya teknolojia  ya BanQu yaliyofanyika mwishoni mwa wiki, aliishukuru TBL na washirika wake kwa kuwajengea uwezo kupitia kilimo cha mtama ambacho hapo awali kilikuwa sio cha kibiashara.

TBL Plc kwa sasa inanunua asilimia 74% ya malighafi zake nchini na imedhamiria kuongeza manunuzi ya malighafi ndani ya nchi katika kipindi cha miaka ijayo.Kampuni inanua mtama kwa ajili ya kutengenezea chapa zake za bia zinazotamba kwenye soko na zenye gharama nafuu za Eagle na Bingwa.

Mchango wa TBL Plc kupitia mpango wake wa kununua malighafi nchini na mkakati wake wa kuendeleza  sekta ya mtama unaenda sambamba na  jitihada za Serikali kuwezesha wakulima wadogowadogo sambamba na kukuza uchumi wa nchi.