Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini Dkt Benson Ndiege,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 22,2021 Ofisini kwake wakati akitoa muongozo wa biashara kwa kutumia mfumo stakabadhi za Ghala utakaotumika mwaka huu kwenye Mazao ya Choroko,Soya,Ufuta,Mbaazi na Dengu.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini Dkt Benson Ndiege,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) leo Januari 22,2021 Ofisini kwake wakati akitoa muongozo wa biashara kwa kutumia mfumo stakabadhi za Ghala utakaotumika mwaka huu kwenye Mazao ya Choroko,Soya,Ufuta,Mbaazi na Dengu.
Afisa Mtendaji Mkuu Soko la Bidhaa Tanzania Bw.Godfrey Malekano akielezea jinsi muongozo wa biashara kwa kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa mwaka 2021 kwenye Mazao ya Choroko,Soya,Ufuta,Mbaazi na Dengu leo Januari 22,2021 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala Bw.Asangye Bangu akitoa ufafanuzi kuhusu Muongozo wa biashara kwa kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala utkaotumika mwaka 2021 kwenye Mazao ya Choroko,Soya,Ufuta,Mbaazi na Dengu leo Januari 22,2021 jijini Dodoma
……………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali kupitia tume ya Maendeleo ya Ushirika hapa nchini imetoa muongozo wa biashara kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za maghalani utakao tumika na wakulima kwa mwaka 2021 katika kuuza mazao ya kibiashara kama Choroko, Soya, Ufuta, Mbaazi na Dengu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini Dkt Benson Ndiege amesema mfumo huo ni mzuri ambao utakwenda kuondoa changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo katika mwaka uliopita na kupelekea kufutwa kwa mfumo huo baadhi ya maeneo.
Amesema mwongozo huo unatoa maelekezo mazao yote yanayozalishwa na wakulima yatakusanywa kwenye ghala la vyama vya ushirika na kusafirishwa kwenda kwenye ghala kuu (ghala la mnada) na taarifa zote za mazao zitapelekwa kwenye ghala kuu.
” Mazao yanayokusanywa kwenye vyama vya ushirika yatapelekwa ghala kuu ambapo taarifa za mazao yaliyopokelewa ghala kuu zitatumwa kwenye soko la bidha na kuuzwa kwa mdana kwa njia ya kielektronic” amesema Dkt Ndiege.
Amewataka viongozi wote ngazi ya Mkoa hadi Wilaya ambako mazao hayo yanalimwa kusimamia vizuri zoezi hilo ili kuhakikisha muongozo huo unatekelezwa kikamilifu katika maeneo yao.
Amesema muongozo huo unaelekeza kuwa malipo ya fedha yafanyike ndani ya siku tano(5) baada ya mazao hayo kununuliwa na wafanyabiashara watakao kuwa na bei nzuri kwa mkulima.
Ameongeza kuwa “malipo haya yanafanywa na mnunuzi kwenye akaunti ya soko la bidhaa Tanzania na fedha zitahamishwa kwenda kwenye chama kikuu cha ushirika ndani ya masaa 12, na baada ya siku tano taratibu nyingine ziwe zimekamilika na mkulima apewe fedha zake” amesema.
Amesema ili kuharakisha zoezi la malipo na fedha za mkulima kuwa salama ni lazima kila mkulima na wadau kuwa na akauti yake benki itakayotumika katika malipo hayo.
Aidha amebainisha kuwa kwa mujibu wa muongozo huo lazima awe amesajiliwa na soko la bidha Tanzania ili aweze kushiriki katika minada ambayo itakuwa inafanyika kila wiki na usajili huo unafanyika kuanzia sasa kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya Soko la bidha Tanzania TMX.
Ameongeza kuwa “mfumo wa stakabadhi ghala unawezesha soko la bidha Tanzania kusaidia wakulima kupitia vyama vya ushirika kuuza mazao yao katika soko la ushindani ambapo soko la bidha Tanzania linafanya minada ya wazi kwa njia ya kielektronic,
“Minada ambayo itakuwa inafanyika kila wiki na inawapa fulsa wanunuzi mbalimbali ndani na nje ya nchi kuweza kushiriki na kupata bei shindani kutokana na wanunuzi kushindana” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji bodi ya usimamizi wa stakabadhi ghala bwana Asangye Bangu amesema ukusanyaji wa bidhaa huzingatia sheria kanuni na miongozo iliyopo ili kuhakikisha sifa ya bidhaa zinazofikishwa ghalani zimekidhi vigezo na kuwa na ubora.
Amesema mfumo huo kwa wanaushirika unatimiza dhana nzima ya ushirika ambayo ni kuunganisha nguvu ya pamoja kwa lengo la kuwa na nguvu ya soko hasa kwa wakulima wadogo ili kuepuka kulanguliwa au kuuza bidhaa zao kwa bei ya chini.
Aidha amesema wametoa elimu kuwa stakabadhi hizo ziheshimiwe na wadau hasa mabenki ambapo mkulima anaweza kukopa kupitia stakabadhi hiyo na fedha ikakatwa baada ya mazao yake kuuzwa na wanunuzi.
Nae Mtendaji Mkuu wa Soko la bidhaa Tanzania TMX Godfrey Malekano amesema mbali na faida nyingine za mfumo huo ni kwa wanunuzi kuepuka gharama kwani mfanyabiashara wa Dodoma anaweza kushiriki mnada wa Simiyu kwa njia ya mtandao bila kwenda Simiyu kushiriki mnada.