****************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
ALIYEKUWA mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, wa Babati Mjini Mkoani Manyara kwa mwaka2007/2015, Cosmas Burra Masauda amesema Rais Dkt John Magufuli amechelewa kuwa Rais wa Tanzania kwani amefanikisha maendeleo mengi kwa muda mfupi tangu aliposhika nafasi hiyo.
Masauda ambaye pia aligombea nafasi ya ubunge wa jimbo la Babati Mjini kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015/2020 na mwaka 2020/2025 ila kura zake hazikutosha, amesema Rais Magufuli kwa muda mfupi alioshika nafasi hiyo amesimamia maendeleo makubwa nchini.
Amesema Rais Magufuli amewanufaisha wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na mengineyo na hasa kwa kiasi kikubwa imefanyika hasa vijiji na endapo angeshikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu Tanzania ingekuwa mbali tofauti na sasa.
Amesema Rais Magufuli ni kiongozi mwenye maono na mwenye misimamo isiyoyumba na alichelewa kuwa kiongozi wa watanzania, hivyo anapaswa kupongezwa kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanyika.
“Rais Magufuli amerudisha heshima ya nchi na wezi wote ikiwemo walioiibia nchi na kuficha fedha nje ya nchi hivi sasa meno yao yamepigwa ganzi kutokana na kula nchi,” amesema Masauda.
Amesema Rais Magufuli anachozungumza anakimaanisha kwani hata ukimtazama usoni anaonyesha anamaanisha kweli jambo lolote analolizungumza kuwa limetoka moyoni.
“Watanzania wanawaza mno ni nani anaweza kushikilia nafasi ya Rais Magufuli pindi muda wake wa awamu ya pili ya urais itakapofika tamati mwaka 2025 ili aweze kuyaendeleza aliyoyaanzisha au kuvitunza,” amesema Masauda.
Amesema Rais Magufuli ni kiongozi mwenye maono na vipaji mbalimbali vya uongozi na Baba mwenye maono ambaye hana ubaguzi hata watu wasio na vyama na pia waliokuwa upinzani wamepewa nafasi.
Aliishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kwa kurudisha majina ya wabunge makini wa mkoa wa Manyara, ambao walipogombea na vyama vya upinzani walipitishwa na wananchi.
“Wana Manyara tunamshukuru mno Rais Magufuli kwa kutupa heshima kubwa sisi kwani alipofanya uteuzi wake kwa mbunge wa jimbo la Babati mjini Pauline Gekul kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, tunasema asante na tunamtakia kila la heri binti yetu kwenye nafasi hiyo ya uteule wa Rais,” amesema Masauda.
Hata hivyo, amesema anawashangaa wasomi waliokuwa wanataka katiba mpya ilihali huduma muhimu za kijamii ikiwemo hospitali na dawa, maji, madarasa na miundombinu ya shule, ndiyo muhimu kwa ajili ya maendeleo.
“Viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa wakitimiza vyema wajibu wao kwa kuwahudumia wananchi, hakutakuwa na mtu atakayetaka kuwa na katiba mpya hapa nchini,” amesema Masauda.
Amesema Bunge la Katiba lilitumia gharama kubwa katika kutafuta katiba mpya lakini haikuweza kupatikana ni bora fedha za gharama hizo zingepelekwa kwenye miradi ya maendeleo kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Amesema kwa kutumia fedha za Bunge la Katiba miradi mikubwa ingefanyika hivyo kuwepo na maendeleo kupitia huduma za jamii hususani kwenye vijiji mbalimbali.
Amesema wasomi waliopata madaraka ya kuteuliwa wasimuangushe Rais Magufuli katika kuhudumia wananchi kwani ni bora kufanya maamuzi na matokeo kuonekana kuliko kusema ndiyo na kutofanya maamuzi yoyote.
Amesema anamtakia afya njema Rais Magufuli ili aweze kuwatumikia wananchi wa Tanzania ambao wana matumaini makubwa ya kupata maendeleo kupitia ilani ya uchaguzi wa CCM kwa mwaka 2020 hadi 2025.
Pia, amempongeza Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi kushika nafasi hiyo kwani anafahamu ni kiongozi mahiri mwenye majibu mawili pekee ya ndiyo au hapana.
“Rais Mwinyi wa Zanzibar ni kiongozi mahiri ambaye kama jambo ataweza kufanya anasema ndiyo itawezekana na endapo haiwezekani anasema hapana na siyo kukuzungusha kwa kusema subiri ili hali jambo hilo haliwezekani,” amesema Masauda.