DKT. BASHIRU AKERWA NA KAULI ZA VIONGOZI WA UPINZANI NCHINI
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amekemea vikali tabia za baadhi ya viongozi wa upinzani kutokuwa waungwana kwa kuongea uongo na kupotosha wananchi kwa maslahi yao binafsi akirejea salamu za mwaka mpya zilizotolewa na mmoja wa viongizi wa upinzani, ambapo kiongozi huyo alipotosha umma kwa kueleza kuwa CCM iliiba kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, pia aliendelea kwa kueleza kuwa, CCM inampango wa kumuongezea muda Mhe. Rais John Pombe Magufuli kinyume cha katiba na utamaduni wa Tanzania.
Katibu Mkuu ametoa ufafanuzi wa uzushi huo leo tarehe 8 Januari, 2021, akikagua jengo jipya la CCM tawi la Bomani lililopo Chato Mkoani Geita ambapo yupo njiani akitokea Bukoba akielekea Dodoma.
“Leo nizungumzie suala la uungwana, muungwana ni mtu wa namna gani, kwa tafsiri ya CCM muungwana ni mtu ambaye vitendo vyake na kauli zake, vina manufaa kwa jamii yake na taifa kwa ujumla, sasa vitendo hivyo na kauli hizo ni zipi, Muungwana hasemi uongo, Muungwana sio mzushi, ukimuona kiongozi wa CCM anasema uongo, huyo anakiuka ahadi ya mwana CCM, ‘nitasema ukweli daima, fitina kwangu mwiko’, ndio maana Rais wetu anasema, ‘msema kweli ni mpenzi wa Mungu.’”
Katibu Mkuu akijibu hoja hizo, ameeleza kuwa,
“Nitumie fursa hii kujibu uongo wa kiongozi mmoja wa upinzani aliyekuwa anatoa salamu za mwaka mpya kwa kusema uongo, kuwa CCM imeiba kura, huo ni uongo na sio uungwana, CCM haiwezi kuiba kura, CCM ni Chama cha watu, kina rekodi nzuri ya uongozi, kinakubalika na kimetekeleza ilani vizuri, kina viongozi wenye sifa, CCM inachagulika, uzushi huu wenye nia ovu kwa nchi yetu haukubaliki na wanaCCM msikae kimya kwenye uzushi kama huu.” Dkt. Bashiru amesisitiza.
Ikumbukwe kuwa, kukosekana kwa uungwana kuna haribu siasa za mataifa ya magharibu kwa sasa, na kama viongozi wa namna hii wakiachwa bila kuueleza ukweli watawagawa wananchi kwa maslahi yao binafsi.
Aidha Dkt. Bashiru ameongeza kuwa, uzushi unaozungumzwa na kiongozi huyo wa upinzani kuhusu CCM kutumia wingi wao bungeni kubadilisha Katiba na kumuongezea muda Mhe. Rais Magufuli, ni uongo na unapaswa kupuuzwa kwani Mhe. Rais Magufuli wakati wote ni msema ukweli na ameshasisitiza kuwa anaheshimu Katiba na utamaduni wa Tanzania wa kubadilishana madaraka kwa amani kila baada ya miaka kumi na hana mpango wa kuongeza hata siku moja baada ya mwaka 2025.
“Jambo lingine ambalo kiongozi huyo wa upinzani amesema, eti CCM kwa sababu tumeshinda viti vingi bungeni, eti tunapanga wa kubadilisha katiba kumuongezea Mhe. Magufuli muhula mwingine. Huo ni uongo wa wazi wazi, sio uungwana na haupaswi kuachwa. Rais Magufuli ameshatamka sio mara moja, kwamba yeye anaheshimu Katiba ya nchi, katiba ya CCM, na utamaduni mzuri wa nchi hii wa kubadilishana uongozi wa Urais kila baada ya miaka kumi, na anaenzi uongozi wa Baba wa Taifa wa kuheshimu Katiba, kama Marais wenzake waliomtangulia walivyofanya wakiongowa na Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Mzee Benjamini Mkapa na Mzee Jakaya Kikwete”.
Miaka Kumi ya Rais Magufuli ikiisha, atapatikana kiongozi mwingine na bila shaka yeyote kwa namna watanzania wanavyoendelela kukiamini Chama chetu, Rais ajaye atatoka CCM, Katibu Mkuu ameongeza.
Aidha, Dkt. Bashiru ametumia fursa hiyo kueleza mambo makuu manne ikiwa ndio msingi wa mafanikio ya CCM kuanzia mwaka 2017, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama na kuongeza wigo wa wanachama wapya, kuwepo na mikakati ya Chama kujitegemea, kujenga Chama kuwa kiungo na daraja kati wanancchi na serikali yao, pamoja na kusimamia maadili ndani ya Chama serikali na jamii kwa ujumla , na huu ndio msingi hasa wa kukemea matendo yasio ya kiungwana yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa upinzani kwa maslahi yao binafsi.
Imetolewa na;
Said Said Nguya
Afisa Habari
Ofisi ya Katibu Mkuu
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)