Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake (TAWJA) Mhe Jaji Joaquuine De-Mello akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.
Na Mathias Canal, Wizara ya Katiba na Sheria-Mwanza
Serikali imefurahishwa kwa kazi zinazofanywa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake TAWJA katika kupigania haki za wananchi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akimuwakilisha Mhe Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.
Amewataka majaji hao kuendelea kuongeza na kuimarisha Haki za Wanawake katika suala la Haki Sawa kwa wote; Kukuza Upatikanaji wa Haki kwa Wanawake, Kukuza/Kuendeleza Uongozi wa Mahakama; Kufanya tafiti za kisheria katika Usawa wa Kijinsia na Haki za Binadamu; Kubadilishana taarifa katika masuala tata yanayowahusu Wanawake na kuondoa Upendeleo wa Kijinsia na Ubaguzi wa aina yeyote.
Amesema kuwa mtazamo mkubwa wa TAWJA ni kuhakikisha Majaji Wanawake na Mahakimu pamoja na Maafisa wengine wa Mahakama na Washirika wanaandaliwa kwa kuwapatia nyenzo sahihi na muhimu zinazohitajika katika kukuza Haki Sawa kwa Wote (‘Equal Justice for All’)
“Ninafahamu kuwa mmekuwa mkifanya hivyo bila kuchoka kwa kipindi cha miaka ishirini (20) mfululizo tokea TAWJA kuanzishwa kwake mwaka 2000. Kwa hili niwapongeze sana Wanachama wote, mnatakiwa kujivunia na kutembea kifua mbele kwa kazi nzuri mnazofanya. Naamini kuwa hili lisingewezekana bila msaada mkubwa kutoka kwa Mahakama ya Tanzania Bara na Zanzibar” Alikaririwa Dkt Mwigulu
Dkt Mwigulu amesema ni wazi kuwa sauti zao Majaji na Mahakimu Wanawake ikijumuisha na zile za Wadau wengine nchini zimepelekea utayari, uwazi na hamasa katika kulaani ubaguzi na ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaofanywa na wanajamii katika maeneo yetu.
Waziri Mwigulu amesem akuwa kaulimbiu ya Mkutano huo ni; “Weledi na Ustawi wa Majaji Na Mahakimu Wanawake: Chachu ya Mabadiliko”, imekuja wakati muafaka na mahali sahihi kwani mara nyingi Wanawake Wataalamu hawatilii maanani ustawi wao, na hasa Maafisa wa Mahakama ambao muda wote hutingwa zaidi na majukumu yao ya msingi.
Kutokana na Kaulimbiu hiyo, mtaibua vitu vingine vilivyojificha na vinayowakabili Maafisa wa Mahakama amesisitiza katika mkutano huo kujadiliwa kwa kina kuhusu masuala yahusuyo afya za akili na mwili na kudadavua kuhusu uchumi, masuala ya kisaikolojia sambamba na kuangalia ukuaji katika maeneo ya utoaji haki.
“Maendeleo ya Mwanamke ni maendeleo ya wote. Hivyo ni lazima kumpa mwanamke kipa umbele. Ni muhimu sana kumpa mwanamke nafasi nyingi bila kujali kuwa ni haki yake ya msingi kwani pia ni kuonyesha matumizi mazuri ya uelewa wa uchumi.” Amesisitiza
MWISHO