Home Biashara Arise B.V (Arise) inamiliki 34.9% ya hisa zilizokuwa za Rabobank katika Benki...

Arise B.V (Arise) inamiliki 34.9% ya hisa zilizokuwa za Rabobank katika Benki ya NMB ya Tanzania.

0

 

*************************************************

 

Arise B.V inayo furaha kuwatangazia wadau wake wote kuwa inamiliki 34.9% ya hisa za Benki ya NMB ambayo imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salam. Hisa hizo zilikuwa zinamilikiwa na Rabobank ambayo ni mshirika wa Arise. Mnamo Desemba 28, mwaka 2020, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana nchini Tanzania iliidhinisha zoezi la uhamishaji wa jumla ya hisa 174,500,000 za Benki ya NMB kutoka Rabobank kwenda Arise. Zoezi la uhamishaji hisa lilikamilika rasmi Desemba 31, mwaka 2020.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Arise, Deepak Malik amesema kukamilika kwa zoezi la uhamishaji hisa ni hatua muhimu kwa Arise.

“Lengo kuu la Arise ni kuingia ubia na taasisi endelevu za kifedha za ndani ili kuongeza nguvu na kukuza upatikanaji wa huduma za kifedha – zenye ufanisi na jumuishi –  barani Afrika. Hili litasaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini,” alisema Bwana Malik.

“Arise inaiona Tanzania kama nchi ambayo inafaa kwa uwekezaji katika eneo zima la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na ubia kati yetu (Arise) na Benki ya NMB utakuwa na matokeo chanya katika kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha Barani Afrika,” alisema Bwana Malik.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema kufanikiwa kukamilika kwa uhamisho wa hisa ni uthibitisho tosha wa imani ya wawekezaji katika benki ya NMB na Taifa kwa ujumla. “Ubia huu shirikishi kati ya Arise na Benki ya NMB unalenga kuleta faida kubwa ambayo itazidi matarajio ya wanahisa wetu katika nyanja za utendaji, biashara, muundo na fedha,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa za fedha za benki za robo ya tatu ya mwaka 2020, Benki ya NMB ndiyo inayoongoza kwa ukubwa wa thamani za mali nchini Tanzania.

Ikumbukwe kuwa NMB ni benki kubwa Tanzania kirasilimali kwa mujibu wa taarifa za fedha za robo ya tatu ya mwaka jana. Rasilimali zake ziliongezeka kwa kuweka rekodi hadi kufikia Shilingi trilioni 7.0 kutoka Shilingi trilioni 6.1 kipindi kama hicho mwaka 2019.

Pia NMB ni benki inayoongoza kwa kutengeneza faida kubwa nchini, baada ya kuwa imepata faida ya Shilingi bilioni 145 kipindi cha robo ya tatu ya mwaka ulioishia Septemba 30, 2020, kutoka shilingi bilioni 82 mwaka 2019.

Bila shaka uwekezaji huu wa muda mrefu wa Arise utasaidia matarajio ya ukuaji wa Benki ya NMB na kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa Tanzania kupitia ongezeko la huduma jumuishi za kifedha, na ukuaji wa sekta za biashara ndogo na za kati, kampuni za kijasiriamali na kilimo.

Arise itasaidia sana Benki ya NMB hasa katika kutoa miongozo na ushauri wa uendeshaji wa biashara sambamba na matakwa ya kanuni za kimataifa.

“Ni matumaini yetu kuwa ubia huu utaleta matokeo chanya kwa Benki ya NMB na Arise,” alisema Bwana Malik.