*****************************************
Nteghenjwa Hosseah, Rukwa
Mkurugenzi wa huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Dr. Ntuli Kapologwe amewaagiza waganga wafawidhi wote wa vituo vya kutolea huduma za Afya kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa dawa (Medicine Audit) kila robo mwaka kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Dr. Ntuli ameyasema hayo wakati alipokua akiongea na timu za usimamizi wa huduma za afya Mkoani Rukwa wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi mkoani humo tarehe 02/01/2020.
Akizungumza katika kikao hicho Dr.Ntuli amesema hakutakuwa msamaha kwa kituo cha kutolea huduma ambacho hakitafanya ukaguzi wa dawa na taarifa ya kila Mkoa kuwasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
“ Kwa kufanya ukaguzi wa dawa tutaweza kujua namna dawa zilivyotumika, dawa gani eneo fulani inatumika sana na kwanini na hivyo kubaini mahitaji zaidi kwa wakati unaokuja.
Pia itawezesha kufahamu kiasi cha Fedha kilichopatikana kutokana na mauzo ya dawa ambacho kitatumika tena kurudi kununua dawa MSD’ alisisitiza Dr Ntuli.
Aliongeza kuwa ukaguzi wa dawa ukifanyika kikamilifu itasaidia Kubaini upotevu wa dawa pamoja na wizi wowote uliotokea katika kituo husika.
Dr. Ntuli alisistiza umuhimu wa kufanya ukaguzi wa dawa kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kufanya mlinganisho wa kiasi cha dawa kilichotumika sambamba na wagonjwa halisi waliohidumiwa na kuwa na takwimu halisi za Serikali katika kutoa Fedha za dawa.
Aidha Dr. Ntuli aliwakumbusha wataalam wa afya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Joseph Pombe Magufuli mwezi Novemba 2020 alitoa shilingi Bil. 41 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na fedha hizo zimeelekezwa MSD.
‘Fedha hizo zitawezesha kila kituo kupata dawa za kutosha sasa ni jukumu la kila kituo kuhakikisha kinazungusha(REVOLVE) fedha baada ya kuwa wametoa huduma kwa kurejesha MSD ili upatikanaji wa dawa uwe endelevu na wananchi waweze kupata dawa wakati wote watakapohitaji” alisisitiza Dr Ntuli.