Home Mchanganyiko Wafugaji Wa Ng’ombe wa Maziwa Waanza Mchakato wa Kuunda Ushirika ili Kunusuru...

Wafugaji Wa Ng’ombe wa Maziwa Waanza Mchakato wa Kuunda Ushirika ili Kunusuru Sekta ya Maziwa Njombe

0

***********************************************

NJOMBE

Umoja wa wafugaji wa ng’ombe wa Maziwa NJOLIFA mkoani Njombe umelazimika kuanza mchakato wa kuunda chama kikuu cha ushirika cha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kitakachosaidia kuwaongoza wafugaji na kuwasaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya maziwa Njombe.

Awali wafugaji hao walikuwa chini ya mwamvuli wa chama cha ushirika cha NJORELICU ambacho wanasema kimeshindwa kuwajibika ipasavyo na kuwalazimu kupandisha hadhi umoja wao wa NJOLIFA ambao kwasasa ni chama cha msingi ili kuwa chama kikuu cha ushirika cha wafugaji kitakachopigania maslahi yao.

Walter Mwanyika,Restuta Mlelwa na Maltin Haule ni baadhi ya wa wafugaji ambao wameshiriki katika mkutano mkuu maalumu wa NJOLIFA ulioanzisha mchakato wa uundwaji wa ushirika ukihudhuriwa na maafisa ushirika kutoka halmashauri na bodi ya maziwa nchini pamoja na mkuu wa wilaya ya Njombe ambao wanasema sekta ya maziwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi na kukosa mtetezi hivyo endapo NJOLIFA itakuwa chama kikuu itakuwa mkombozi kwao.

Akizungumzia faida ya kuwa na ushirika hai na namna ya kunusuru sekta ya maziwa mkoani Njombe mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri amesema kupitia chama kikuu cha ushirika cha wafugaji watakuwa sauti moja nakutoa agizo kwa wafugaji kuerejesha imani na kuanza kuuza maziwa katika kiwanda cha Njombe ambacho wao ni sehemu ya wamiliki.

Msafiri amesem kuna kila sababu ya kumuamini meneja aliyopo sasa kwa kuwa amefanya jitihada kubwa kukirejesha kwenye mfumo bora wa uendeshaji kiwanda kwani wakati anafika alikuta kiwanda kinadaiwa zaidi ya bil 1 na wafugaji pamoja na taasisi mbalimbali za serikali kama vile TRA, na NSSF na kuanza kuyalipa madeni hayo ambayo yapo ukingoni kumalizika.
Kwa upande wake meneja wa kiwanda cha maziwa Njombe Shahib Kassim akitolea ufafanuzi kuhusu kiasi kilichobaki kulipa wafugaji amesema walisha anza kulipa waliobaki ni wale wenye changamoto binafsi kama akaunti za benki kutofautiana majina na mfugaji.
Katika hatua nyingine Kassim amesema milango imeanza kufunguka katika sekta ya maziwa kwani kuna wadau wengine kama vile PASS ambao wapo tayari kuwekeza kwenye sekta hiyo hivyo siku zijazo wakulima wataanza kunufaika zaidi na ufugaji wa Ng’ombe wa maziwani¬†
“Kiwanda Kimejipanga vyema kumaliza madeni yote muda mfupi ujao kwakuwa soko la bidhaa zake limefunguka zaidi katika mikoa ya Mbeya,Dar es salaamu na Arusha ambako wanahitaji maziwa kila siku kutoka Njombe” Alisema Shahib Kassim.
Nae afisa ushirika kutoka halmashauri ya mji wa Njombe Harison Nyambo na afisa ushirika ambaye amewakilisha bodi ya maziwa Tanzania ndugu Ndimolwo Laizer wamesema hatua ya kuunda ushirika itakuwa muarobaini wa matatizo mengi na kuwataka viongozi watakaochaguliwa kuwa wabunifu kwa kubuni miradi ya ushirika ili kuwa hai zaidi