****************************************
KUUAWA KWA JAMBAZI NA KUPATIKANA KWA SILAHA.
Mtu mmoja asiyefahamika jina, mwanaume mwenye umri kati ya miaka 30 – 35 amefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwenye majibizano ya kurushiana risasi na Askari Polisi huko maeneo ya Stendi Kuu ya Mabasi Jijini Mbeya.
Ni kwamba usiku wa kuamkia tarehe 05.01.2021 saa 00:10 huko maeneo ya Itiji karibu na Stendi kuu ya mabasi Jijini Mbeya, Jeshi la Polisi lilipata taarifa za siri kuwa kuna watu takribani watano wanaume wamekaa eneo hilo wanatiliwa shaka kuwa ni wahalifu na wanajipanga kwenda kufanya uhalifu.
Kutokana na taarifa hizo, Askari Polisi kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu walifika eneo hilo mara moja na kufanya ufuatiliaji ndipo watu hao walipobaini kuwa wanafuatiliwa walianza kukimbia huku mmoja wao alitoa silaha na kuanza kuwafyatulia risasi askari, Askari Polisi kwa umahiri mkubwa walikabiliana nao kwa kujihami na kufanikiwa kumjeruhi kwa risasi jambazi huyo asiyefahamika jina.
Majeruhi alifariki dunia muda mfupi wakati anakimbizwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu. Eneo la tukio kumepatikana bunduki moja aina ya Shot gun iliyotengenezwa kienyeji inayotumia risasi za shotgun 12 mm, risasi 12 za Shotgun ambazo hazijatumika, maganda 2 ya risasi, kipande kimoja cha nondo na sululu @ Moko na Wallet aina ya guchi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu. Msako mkali unaendelea dhidi ya watuhumiwa wengine wanne waliokimbia.
MSAKO DHIDI YA WATUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawasaka watuhumiwa wawili 1. JUMA SUNZIMA na 2. MERRY DAIMON wote wakazi wa Matundasi Wilaya ya Chunya kwa tuhuma za tukio la mauaji ya JUMA KITEMANGO [48] Mkazi wa Matundasi.
Ni kwamba usiku wa kuamkia tarehe 04.01.2021 huko Matundasi JUMA KITEMANGO [48] alishambuliwa na mtuhumiwa JUMA SUNZIMA kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani, jicho la kushoto na utosini na kumsababishia majeraha hadi kukimbizwa katika Zahanati ya Kijiji cha Matundasi kwa ajili ya kupatiwa matibabu na ilipofika majira ya saa 12:00 mchana alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Chanzo cha tukio hili ni ugomvi uliotokea baina ya marehemu na mtuhumiwa baada ya mtuhumiwa kufumaniwa akiwa na mke wa marehemu aitwaye MERRY DAIMON nyumbani kwa marehemu. Aidha kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita marehemu na mke wake walikuwa na mgogoro wa kimahusiano uliotokana na wivu wa kimapenzi ambapo marehemu alikuwa akimshutumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi n na mtuhumiwa.
Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.
KUPATIKANA NA POMBE KALI ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI.
Sambamba na hilo, katika misako, doria na operesheni zinazoendelea mkoani Mbeya, mnamo tarehe 05.01.2021 majira ya saa 11:00 asubuhi Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilimkamata mtuhumiwa CHRISTOPHER SAMSON NDOMBA [42] Mkazi wa Kyela Kati akiwa na pombe kali aina mbalimbali zilizopigwa marufuku nchini.
Katika upekuzi tulioufanya katika maboksi aliyokutwa nayo mtuhumiwa zilipatikana pombe kali aina ya WIN chupa 80, Right Choice chupa 120 pamoja na Ice Dry London Gin chupa 190 kutoka nchi ya Malawi. Mtuhumiwa alikuwa akisafirisha pombe hizo kwenye Pikipiki yenye namba za usajili MC 793 CQC aina ya Kinglion. Upelelezi unaendelea.
AJALI YA MOTO KUUNGUZA CHUMBA NA KUSABABISHA KIFO NA MAJERUHI.
Mtoto wa miaka 4 aitwaye BRADON WISEMAN amefariki dunia kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata katika ajali ya moto kuunguza chumba kimoja wapo katika nyumba yenye vyumba viwili iliyotokea Kijiji cha Mpandapanda Wilaya ya Rungwe.
Ni kwamba mnamo tarehe 05.01.2021 majira ya saa 22:00 usiku huko Mpandapanda, Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, chumba kimoja katika nyumba mali ya TABU GEORGE MWAKAPILA [42] Mkazi wa Ilongoboto yenye vyumba viwili anacholala yeye na wajukuu zake wawili kiliungua moto na kusababisha kifo kwa mtoto BRADON WISEMAN.
Aidha katika tukio hilo, mtoto ALEN ALLY KADUMA [06] Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kiwira alijeruhiwa kwa moto huo sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na moto huo. Chanzo cha moto ni kibatari kilichokuwa katika chumba hicho kuunguza nguo zilizokuwa chumbani na kusababisha moto kusambaa. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya – Makandana kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.