Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Katikati), Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Rehema Madenge (Kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga wakiwa katika picha na wamiliki wa Hati ya Pamoja Zakaria Michael Mwanga na mke wake Hadija Rashid
Watendaji wa sekta ya ardhi na viongozi wengine wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayuko pichani) wakati wa ziara yake katika mikoa wa Lindi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi tarehe 5 Januari 2021.
*************************************************
Na Munir Shemweta, WANMM LINDI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameiagiza ofisi ya Ardhi mkoa wa Lindi kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi wa mkoa huo ili waone umuhimu, faida na thamani ya kumiliki ardhi kutokana na mkoa huo kuwa nyuma katika umilikishaji ardhi.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo tarehe 5 Januari 2021 mkoani Lindi wakati akigawa hati za ardhi kwa wananchi wa kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo katika halmashauri ya Manispaa ya Lindi akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi mkoani humo.
Dkt Mabula alisema, mkoa wa Lindi uko nyuma kwa wananchi wake kujitokeza kumilikishwa maeneo ya ardhi wànayomiliki na kumbukumbu za mkoa zinaonesha kuna jumla ya hati 7025 zilizotolewa kwa wamiliki wa ardhi na kusisitiza kuwa idadi hiyo ni ndogo kwa kuwa wananchi wengi hawajaamka na kuona thamani ya kumilikishwa.
“Ofisi ya Ardhi Mkoa mkatoe elimu kwa wananchi umuhimu na faida za kuwa na umiliki wa ardhi, maana hapa shida haiko katika kumilikishwa kwa hati za miaka 99 pekee bali hata zile za kimila hivyo lazima mkatoe elimu hata kwa wale wananchi walio vijijini ili wamilikishwe na kupatiwa hati watakayoitumia kwa faida ya maendeleo” alisema Dkt Mabula.
Aliitaka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Lindi kujipanga vizuri na kwenda kwenye maeneo ya kata za mkoa huo kuwaelimisha wananchi faida za kuwa na hati ya ardhi kwa kuwa tangu kuanzishwa ofisi hiyo miezi sita iliyopita ni hati 367 pekee ndizo zilizotolewa idadi aliyoieleza kuwa ni ndogo ukilinganisha na mikoa mingine.
Aliwaeleza wakazi wa kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo katika Manispaa ya Lindi kuwa, mkoa huo una maeneo mengi mazuri ya uwekezaji na iwapo watazembea kumilikishwa kuna hatari wakayauza kwa bei ya chini kwa kwa kisingizio cha kutopimwa au kuhaulishwa.
“Mkizembea kumilikishwa maeneo yenu sasa na kupatiwa hati, mtu akitaka kuwekeza mtampa kwa bei ya chini kwa kisingizio cha kutopimwa na mwingine atalichukua na baadaye ataliuza kwa bei kubwa kwa kuwa ulimuuzia likiwa halijapimwa” alisema Naibu Waziri Dkt Mabula.
Aliwataka wananchi wa mkoa wa Lindi kujitokeza kupima maeneo yao na kuchukua hati na kusisitiza kuwa hata kama maeneo hayo hawayahitaji wanaweza kuyapima ili kuongeza thamani na baadaye watakapotaka kuyauza wauze na kupata fedha za kutosha.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kwa kuwa mapato ya kodi hiyo ndiyo yanayotumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, idara ya ardhi ikisimamiwa vizuri na Wakurugenzi wa Halmashauri wakiiwezesha kwa kuipatia vitendea kazi na bajeti ya kutosha basi inaweza kuingiza mapato mengi kuliko sekta nyingine yoyote kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Lindi Said Kijiji alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na ofisi yake kuhakikisha maeneo mengi ya mkoa huo yanapimwa lakini mwamko wa wananchi ni mdogo.
Alisema, ofisi yake ilishatembelea halmashauri za mkoa huo na kuonana na wakurugenzi kwa lengo la kuendesha zoezi la kupima na kumilikisha maeneo ambapo alisema mafanikio makubwa yalikuwa katika halmashauri ya Mtama.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Mingoyo Manispaa ya Lindi Zakaria Michael Mwanga na Hadija Rashid Magaya waliokabidhiwa Hati ya pamoja walikuwa na haya ya kusema.