*****************************************
Nteghenjwa Hosseah, Mbeya
Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dr.Ntuli Kapologwe amewaagiza Waganga Wakuu wa Halmashauri za Mkoa wa Mbeya kuhakikisha vituo vyote vya Afya vilivyojengwa kwenye maeneo yao vinaanza kutoa huduma kabla ya Januari,30 mwaka 2021.
Dr. Ntuli ametoa kauli hiyo alipokua anaongea na wataalam watendaji wa afya wa Mkoa wa Mbeya wakati wa ziara ya ukaguzi shiriki inayoendelea katika Mkoa huo.
Baada ya kupokea taarifa toka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dr. Ntuli alihoji hali ya utoaji wa huduma katika Vituo vya Afya vilivyojengwa na kuboreshwa katika Mkoa huo ndipo alipostaajabu kujulishwa kuwa vituo vingi bado havijaanza kutoa huduma.
Taarifa hiyo ilimlazimu kuhoji kwa kina kwa kila Halmashauri sababu zinazopelekea kutokufunguliwa kwa vituo hivyo haswa huduma ya upasuaji ambayo inasubiriwa kwa hamu katika maeneo mengi.
Taarifa ya Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya alibainisha kuwa kwa vituo viwili ambavyo vimejengwa Iyunga na Nzovwe vimeanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje tu lakini huduma za upasuaji bado hazijaanza kwa sababu ya ukosefu wa vifaa.
Kutoka Mbeya Dc Mganga Mkuu alisema walipaya vituo vitatu ambavyo ni Ilembo, Santilya na Ikupwe na kituo cha Ilembo tu ndicho kinachotoa huduma za upasuaji na vilivyobakia vinatoa huduma za wagonjwa wa nje.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mbalali aliweka wazi kuwa walipata kituo kimoja tu cha Utengule usangu na kinafanya kazi vizuri kwa kutoa huduma zote stahiki.
Kutoka Chunya vituo ni Lupatingatinga na Mtande na kati ya hivyo hakuna kilichoanza kutoa huduma ya upasuaji, Mtande tu ndicho kinachotoa huduma za wagonjwa wa nje.
Na Katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe vituo ni Ikuti tu ambacho kilishaanza kutoa huduma za upasuaji na Maskuru kikiwa bado hakijaanza kutoa huduma hiyo.
Mganga Mkuu wa Kyela alibainisha kuwa Kituo alichopata ni Ipinda na kimeshaanza kutoa huduma zote na wananchi wanafurahia huduma bora za Afya.
Busokelo ilipata vituo vya Afya vitatu ambavyo ni Mpata, Ntaba na Isange ambavyo vyote mpaka sasa havijaanza kutoa huduma za upasuaji.
Baada ya taarifa hizo Dr Ntuli alifanya jitihada za kukutana na Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Mbeya Dr.Godlove Mbwanji na kumwelezea uhitaji wa vifaa hivyo naye aliahidi kutoa kitandaa cha Upasuaji kwa ajili ya kituo cha Afya Nzovwe na vifaa vingine vitakavyohitajika.
Mwisho Dr.Ntuli aliwagiza waganga wakuu wa maeneo hayo yote kuhakikisha wanatafuta vifaa vonavyokosekana kwa wadau mbalimbali ili vituo hivyo vianze kutoa huduma ya upasuaji kabla ya Tarehe 30 Januari,2021.