Meneja wa Tanroads Mkoani Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa huo (RCC) kilichofanyika mjini Babati.
*********************************************
WABUNGE wa majimbo ya Mkoa wa Manyara, wamewapongeza wakala wa barabara nchini (Tanroads) kwa kukarabati na kujenga miundombinu ya barabara hasa wakati wa mvua hadi kusaidia wao wakachaguliwa kwa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Octoba mwaka huu.
Wabunge hao waliyasema hayo mjini Babati wakiwa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Manyara (RCC).
Mbunge wa jimbo la Mbulu mjini, Zacharia Isaay amesema wananchi wa eneo hilo walitoa kura nyingi kwa wagombea wa CCM kutokana na ukarabati na utengenezaji wa barabara.
“Kwa kweli Tanroads mmechangia kwa kiasi kikubwa CCM tukachaguliwa kuanzia nafasi za madiwani, ubunge na Urais kwa namna mlivyokarabati barabara zetu,” amesema Isaay.
Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay ameishukuru Tanroads ilivyopambana na ujenzi wa barabara hasa wakati wa mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha wakachaguliwa kwa kura nyingi.
“Pamoja na hayo Tanroads mnapaswa kupambana na utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Haydom kutoka Karatu, Mbulu na kupitia Singida iliyopo kwenye ilani ya uchaguzi,” amesema Maasay.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema jitihada za dhati zinapaswa kufanyika ili barabara zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2020/2025 zijengwe.
Ole Sendeka amesema barabara ya lami ya kutoka Mirerani, Orkesumet hadi Dodoma na Arusha hadi Orkesumet zinatakiwa kupewa msukumo ili zianze kujengwa.
Mbunge wa jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma amesema ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Katesh hadi Haydom wilayani Mbulu inatakiwa kutimizwa kwani wakati wa mvua huwa haipitiki.
“Pia kuna ahadi ya Makamu wa Rais mama Samia Suluhu kwenye kampeni alituahidi kilomita 10 za lami kwenye mji mdogo wa Katesh, inapaswa kufuatiliwa,” amesema mhandisi Hhayuma.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Manyara, Simon Lulu amesema miradi ya barabara zote zilizoainishwa katika ilani ya uchaguzi zipewe kipaumbele katika ukamilishaji ili wananchi waongeze imani na serikali yao.
Meneja wa Tanroads mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema baadhi ya barabara zimeanza kufanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa katika hatua ya awali ya ujenzi.
Mhandisi Rwesingisa amesema watahakikisha wanafuatilia katika kukumbusha ujenzi wa barabara zote za mkoa wa Manyara ambazo ni ahadi ya viongozi na zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi wa CCM.